Add parallel Print Page Options

Wake na Waume

Vivyo hivyo, enyi wake mnapaswa kuwa radhi kuwahudumia waume zenu. Ili hata wale waliokataa kuyapokea mafundisho ya Mungu washawishike na kuamini kutokana na jinsi mnavyoishi. Hivyo hamtahitaji kusema chochote. Waume zenu watayaona maisha safi mnayoishi yanayomheshimu Mungu. Si nywele za gharama, vito vya dhahabu, au nguo nzuri zitakazowafanya mpendeze. Bali, uzuri wenu utoke ndani yenu, uzuri wa roho yenye upole na utulivu. Uzuri huo hautatoweka kamwe. Ni wa thamani sana kwa Mungu.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa wanawake watakatifu walioishi hapo zamani na kumfuata Mungu. Walijipamba kwa jinsi hiyo hiyo kwa kuwahudumia waume zao. Ninazungumza juu ya wanawake kama Sara aliyemtii Ibrahimu, mume wake na kumwita bwana wake. Na ninyi wanawake ni watoto wa kweli wa Sara ikiwa daima mnafanya yale yaliyo sahihi pasipokuwa na hofu.

Vivyo hivyo, enyi waume inawapasa kuishi na wake zenu kwa kuelewa udhaifu alionao mwanamke na matumaini ya Mkristo. Hamna budi kuwapa heshima kwa sababu Mungu kwa sababu Mungu anawapa baraka zile zile anazowapa ninyi, yaani neema ya maisha ya kweli. Fanyeni hivi ili maombi yenu yasizuiliwe.

Kuteseka kwa kutenda haki

Hivyo ninyi nyote mnapaswa kuishi pamoja kwa amani. Mjitahidi kuelewana ninyi wenyewe. Mpendane kama kaka na dada na muwe wanyenyekevu na wema. Msimfanyie uovu mtu yeyote ili kulipa kisasi kwa uovu aliowatendea. Msimtukane mtu yeyote ili kulipiza matusi aliyowatukana. Lakini mwombeni Mungu awabariki watu hao. Fanyeni hivyo kwa sababu ninyi wenyewe mliteuliwa kupokea baraka, 10 Maandiko yanasema:

“Anayetaka kufurahia maisha ya kweli
    na kuwa na siku nyingi njema tu,
aepuke kusema chochote kinachoumiza,
    na asiruhusu uongo utoke kwenye kinywa yake.
11 Aache kutenda uovu, na atende mema.
    Atafute amani, na fanya kila analoweza ili kuwasaidia watu kuishi kwa amani.
12 Bwana huwaangalia wale watendao haki,
    na husikia maombi yao.
Lakini yu kinyume cha wale watendao uovu.”(A)

13 Ikiwa unajaribu kwa bidii kutenda mema, ni nani atakayetaka kukudhuru? 14 Lakini hata ukiteseka kwa sababu kutenda yaliyo haki, unazo Baraka za Mungu. “Msimwogope mtu yeyote, wala msiruhusu watu wawasumbue.”(B) 15 Lakini mjitoe kikamilifu kwa Kristo ambaye ni Bwana wenu pekee. Na daima iweni tayari kumjibu mtu yeyote anayetaka ufafanuzi kuhusu tumaini linaloyaongoza maisha yenu.[a] 16 Lakini wajibuni kwa upole na heshima kwa ajili ya Mungu, mkizitunza dhamiri zenu mbele zake. Ndipo watu watakapoona namna njema mnayoishi kama wafuasi wa Kristo. Na wataaibika kwa kuwanenea mabaya.

17 Ni afadhali kuteseka kwa kutenda mema kuliko kutenda mabaya. Ndiyo, ni bora ikiwa hivyo ndivyo Mungu anavyotaka.

18 Kristo mwenyewe aliteseka alipokufa kwa ajili yenu,
    na kwa kifo hicho kimoja alilipa fidia kwa ajili ya dhambi.
Hakuwa na hatia,
    lakini alikufa kwa ajili ya watu waliokuwa na hatia.
    Alifanya hivyo ili awalete ninyi nyote kwa Mungu.
Kama mwanadamu, aliuawa,
    lakini uhai wake ulifanywa hai na Roho.[b]

19 Na kwa Roho alikwenda akazihubiri roho zilizo kifungoni. 20 Hizo ndizo roho zilizokataa kumtii Mungu hapo zamani wakati wa Nuhu. Mungu alisubiri kwa uvumilivu Nuhu alipokuwa anaunda safina. Na watu wachache tu, yaani wanane kwa jumla ndiyo walioingia katika safina na kuokolewa kwa kuvushwa salama katika gharika hiyo. 21 Na maji yale ni kama ubatizo, unaowaokoa ninyi sasa kupitia ufufuo wa Yesu Kristo kutoka katika wafu na siyo kuondoa uchafu mwilini kwa kuoga. Ni ahadi ya dhati ya kuishi kwa kumcha Mungu. 22 Sasa yupo mbinguni upande wa kuume wa Mungu, na anatawala juu ya malaika, mamlaka na nguvu.

Footnotes

  1. 3:15 linaloyaongoza maisha yenu Kwa maana ya kawaida, “tumaini lililo ndani (au miongoni) mwenu,” Hii inamaana kuwa, “kile kinachothibiti tabia zenu kama waamini.”
  2. 3:18 ulifanywa hai na Roho Au “katika roho”. Pia katika mstari wa 19.