Maagizo Kwa Timotheo

Roho anasema wazi wazi kwamba katika siku za mwisho watu wengine wataiacha imani yao na kusikiliza roho za udanganyifu na mafundisho ya mashetani. Mafundisho hayo yanaletwa na wanafiki waongo ambao dhamiri zao zimekufa kama vile zimechomwa kwa chuma cha moto. Wao wanawazuia watu kuoa; na wanawaamrisha watu wasile vyakula vya aina fulani - ambavyo Mungu aliviumba vipoke lewe kwa shukrani na wale wanaoamini na waliopata kuijua kweli. Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema wala kitu cho chote kisikataliwe kama kinapokelewa kwa shukrani, maana kina takaswa kwa neno la Mungu na kwa sala.

Mtumishi Mwema Wa Kristo

Ukiwapa ndugu mafundisho haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu ambaye amelishwa vema kwa maneno ya imani na yale mafundisho mema uliyoyafuata. Usijishughulishe kabisa na hadithi zisizo za kidini ambazo hazina maana. Jizoeze kuishi kwa kumcha Mungu. Maana japokuwa mazoezi ya mwili yana faida kiasi, kumcha Mungu kuna faida kwa kila hali, kwa sababu kumcha Mungu kuna faida kwa maisha ya sasa na maisha yajayo.

Neno hili ni la kweli na linastahili kupokelewa, 10 na kwa ajili yake sisi tunajitahidi na kutaabika, kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio.

11 Agiza na kufundisha mambo haya. 12 Mtu asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe mfano mwema kwa waamini wote kwa maneno yako, kwa mwenendo wako, katika upendo, imani na usafi.

13 Mpaka hapo nitakapokuja, tumia wakati wako katika kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri, na kufundisha. 14 Usiache kutumia kipawa ulichonacho, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee wa kanisa walipokuwekea mikono. 15 Tekeleza mambo haya. Tumia nguvu zako na wakati wako kuyatimiza ili watu wote waone maendeleo yako.

16 Jilinde sana, na utunze mafundisho yako. Yashikilie, maana kwa kufanya hivyo utajiokoa wewe mwenyewe na wale wanaoku sikiliza.

Maonyo juu ya Walimu wa uongo

Roho anasema wazi wazi kwamba katika siku za mwisho wengine watajitenga na imani. Watazitii roho zinazodanganya, na kufuata mafundisho ya mashetani. Mafundisho hayo yanafundishwa na watu wanaodanganya na kuwafanyia hila wengine. Watu hawa waovu hawapambanui kati ya mema na maovu. Ni kana kwamba dhamiri zao zimeharibiwa kwa chuma cha moto. Wanasema ni vibaya kuoa. Na wanasema kwamba kuna baadhi ya vyakula ambavyo watu lazima wasile. Lakini Mungu aliumba vyakula hivi, na wale wanaoamini na kuelewa ukweli wanaweza kuvila kwa shukrani. Kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, hakuna chakula kitakachokataliwa kama kikikubaliwa kwa shukrani. Kila kitu alichokiumba kiliumbwa kitakatifu kwa namna alivyosema na kwa maombi.

Uwe Mtumishi Mwema wa Kristo Yesu

Waambie haya kaka na dada huko. Hii itakuonesha wewe kuwa ni mtumishi mwema wa Kristo Yesu. Utaonyesha kwamba umefundishwa maneno ya imani na mafundisho mazuri uliyoyafuata. Usitumie muda wowote katika masimulizi ya kipuuzi ambayo hayakubaliani na ukweli wa Mungu. Badala yake jizoeshe mwenyewe kuishi maisha ya kumheshimu na kumpendeza Mungu. Kufanya mazoezi ya mwili wako kuna manufaa kidogo kwako. Lakini kujaribu kumpendeza Mungu kwa njia zote kunakufaa zaidi. Kunakuletea baraka katika maisha haya na maisha ya baadaye pia. Huu ni usemi wa kweli ambao unaweza kukukubaliwa bila kuuliza swali: 10 Tunayo matumaini kwa Mungu aliye hai, Mwokozi wa watu wote. Ambaye hasa, ni Mwokozi wa wale wote wanaomuamini. Na hii ndiyo sababu tunafanya kazi na kupambana.

11 Amuru na kufundisha mambo haya. 12 Wewe ni kijana, lakini usiruhusu yeyote kukufanya wewe kama si mtu muhimu. Uwe mfano kuonesha waamini namna wanavyoweza kuishi. Waoneshe kwa namna unavyosema, unavyoishi, unavyopenda, unavyo amini, na namna ya maisha yako safi.

13 Endelea kusoma Maandiko kwa watu, watie moyo, na uwafundishe. Fanya hivyo mpaka nitakapo kuja. 14 Kumbuka kutumia kipawa ulichonacho, ambacho ulipewa kupitia unabii wakati kundi la wazee lilipo kuweka mikono juu yako. 15 Endelea kufanya haya, na jitoe maisha yako kutenda hayo. Kisha kila mtu anaweza kuona namna ilivyo vema unavyotenda. 16 Uwe mwangalifu katika maisha na mafundisho yako. Endelea kuishi na kufundisha kwa usahihi. Kisha, utajiokoa mwenyewe na wale wanaosikiliza mafundisho yako.