Maagizo Kwa Timotheo

Roho anasema wazi wazi kwamba katika siku za mwisho watu wengine wataiacha imani yao na kusikiliza roho za udanganyifu na mafundisho ya mashetani. Mafundisho hayo yanaletwa na wanafiki waongo ambao dhamiri zao zimekufa kama vile zimechomwa kwa chuma cha moto. Wao wanawazuia watu kuoa; na wanawaamrisha watu wasile vyakula vya aina fulani - ambavyo Mungu aliviumba vipoke lewe kwa shukrani na wale wanaoamini na waliopata kuijua kweli. Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema wala kitu cho chote kisikataliwe kama kinapokelewa kwa shukrani, maana kina takaswa kwa neno la Mungu na kwa sala.

Mtumishi Mwema Wa Kristo

Ukiwapa ndugu mafundisho haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu ambaye amelishwa vema kwa maneno ya imani na yale mafundisho mema uliyoyafuata. Usijishughulishe kabisa na hadithi zisizo za kidini ambazo hazina maana. Jizoeze kuishi kwa kumcha Mungu. Maana japokuwa mazoezi ya mwili yana faida kiasi, kumcha Mungu kuna faida kwa kila hali, kwa sababu kumcha Mungu kuna faida kwa maisha ya sasa na maisha yajayo.

Neno hili ni la kweli na linastahili kupokelewa, 10 na kwa ajili yake sisi tunajitahidi na kutaabika, kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio.

11 Agiza na kufundisha mambo haya. 12 Mtu asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe mfano mwema kwa waamini wote kwa maneno yako, kwa mwenendo wako, katika upendo, imani na usafi.

13 Mpaka hapo nitakapokuja, tumia wakati wako katika kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri, na kufundisha. 14 Usiache kutumia kipawa ulichonacho, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee wa kanisa walipokuwekea mikono. 15 Tekeleza mambo haya. Tumia nguvu zako na wakati wako kuyatimiza ili watu wote waone maendeleo yako.

16 Jilinde sana, na utunze mafundisho yako. Yashikilie, maana kwa kufanya hivyo utajiokoa wewe mwenyewe na wale wanaoku sikiliza.