Add parallel Print Page Options

Salamu kutoka kwa Paulo. Mimi ni mtume kwa sababu Kristo Yesu[a] alinichagua. Alinichagua kwa sababu hivyo ndivyo Mungu alitaka. Naandika barua hii kwa msaada wa Sosthenesi[b] aliye kaka yetu katika Kristo.

Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, ninyi ambao mmefanywa watakatifu kwa sababu mmeunganishwa kwa Kristo Yesu. Mlichaguliwa kuwa watakatifu wa Mungu pamoja na watu wote kila mahali wanaomwamini Bwana[c] Yesu Kristo, Bwana wao na Bwana wetu.

Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.

Paulo Amshukuru Mungu

Ninamshukuru Mungu daima kwa sababu ya neema aliyowapa katika Kristo Yesu. Ambaye kwa njia yake Mungu amewabariki sana kwa namna mbalimbali hata miongoni mwenu wapo watu wenye vipawa vya kuzungumza na wengine wana vipawa vya maarifa! Hii ni kwa sababu yale tuliyowaambia kuhusu Kristo yamedhihirika kuwa kweli katikati yenu. Na sasa mna karama zote mnapomsubiri Mungu audhihirishie ulimwengu jinsi Bwana wetu Yesu Kristo alivyo wa ajabu. Ataendelea kuwatia nguvu na hakuna atakayeweza kuwashtaki mpaka siku ya mwisho Bwana wetu Yesu atakaporudi. Mungu ni mwaminifu. Na ndiye aliyewachagua ninyi ili mshiriki uzima pamoja na Mwanaye, Yesu Kristo Bwana wetu.

Acheni Mabishano Miongoni Mwenu

10 Ndugu zangu, kwa mamlaka ya Bwana wetu Yesu Kristo, ninawasihi mpatane ninyi kwa ninyi. Msigawanyike katika makundi. Lakini iweni pamoja tena katika kuwaza kwenu na katika nia zenu.

11 Kaka na dada zangu, baadhi ya jamaa wa Kloe wamenitaarifu kuwa kuna mabishano miongoni mwenu. 12 Baadhi yenu husema, “Mimi ninamfuata Paulo,”[d] na mwingine husema, “Mimi ninamfuata Apolo.” Mwingine husema, “Mimi ninamfuata Petro,”[e] na mwingine husema, “Mimi ninamfuata Kristo.” 13 Kristo hawezi kugawanywa katika makundi. Je, Paulo ndiye alikufa msalabani kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa katika jina la Paulo? 14 Ninashukuru kwa kuwa sikumbatiza mtu yeyote kwenu isipokuwa Krispo na Gayo. 15 Ninashukuru kwa sababu hakuna anayeweza kusema kuwa mlibatizwa katika jina langu. 16 (Niliwabatiza pia watu wote wa nyumbani mwa Stefana, lakini sikumbuki kuwa niliwabatiza watu wengine) 17 Kristo hakunipa kazi ya kubatiza watu. Alinipa kazi ya kuhubiri Habari Njema pasipo kutumia hekima ya maneno, inayoweza kubatilisha nguvu iliyo katika msalaba[f] wa Kristo.

Nguvu ya Mungu na Hekima Katika Kristo Yesu

18 Mafundisho kuhusu msalaba yanaonekana ni ya kipuuzi kwao wao wanaoelekea kwenye uharibifu. Lakini ni nguvu ya Mungu kwetu sisi tunaookolewa. 19 Kama Maandiko yanavyosema,

“Nitaiharibu hekima ya wenye hekima.
    Nitaukanganya uelewa wa wenye akili.”(A)

20 Je, hii inasema nini kuhusu mwenye hekima, mtaalamu wa sheria au yeyote katika ulimwengu huu mwenye ujuzi wa kutengeneza hoja zenye nguvu? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upuuzi. 21 Hii inadhihirisha wazi kuwa, Mungu katika hekima yake aliamua kuwa hawezi kupatikana kwa kutumia hekima ya ulimwengu. Hivyo Mungu aliutumia ujumbe unaoonekana kuwa upuuzi kuwaokoa wale wanaouamini.

22 Na hii ndiyo sababu Wayahudi wanataka ishara za miujiza na Wayunani wanataka hekima. 23 Lakini ujumbe tunaomwambia kila mtu unahusu Masihi aliyekufa msalabani. Ujumbe huu ni kikwazo kwa Wayahudi na kwa Wayunani ni upuuzi. 24 Lakini kwa Wayahudi na Wayunani walioteuliwa na Mungu, Masihi huyu aliyesulibiwa ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. 25 Maana upumbavu wa Mungu ni hekima zaidi ya hekima ya kibinadamu, na udhaifu wa Mungu ni nguvu zaidi ya nguvu ya kibinadamu.

26 Kaka na dada zangu, fikirini kuhusu hili kwamba Mungu aliwachagua ili muwe milki yake. Wachache wenu mlikuwa na hekima kwa namna dunia inavyoichukulia hekima. Wachache wenu mlikuwa mashuhuri na wachache wenu mnatoka katika familia maarufu. 27 Lakini Mungu aliyachagua mambo ambayo wanadamu huyachukulia kuwa ya kipumbavu ili ayaaibishe yenye hekima. Aliyachagua mambo yanayoonekana kuwa manyonge ili ayaaibishe yenye nguvu. 28 Aliwachagua wasio kitu ili ayaangamize yale ambayo ulimwengu unadhani ni muhimu. 29 Mungu alifanya hivi ili mtu yeyote asisimame mbele zake na akajisifu kuwa yeye ni bora kuliko mwingine. 30 Lakini Mungu ameyafungamanisha maisha yenu na Kristo Yesu. Yeye alifanywa kuwa hekima yetu kutoka kwa Mungu. Na kupitia kwake tumehesabiwa haki na Mungu na tumefanywa kuwa watakatifu. Kristo ndiye aliyetuokoa, akatufanya watakatifu na akatuweka huru mbali na dhambi. 31 Hivyo, kama Maandiko yanavyosema, “Kila anayejisifu, ajisifu juu ya Bwana tu.”(B)

Footnotes

  1. 1:1 Kristo Yesu Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32: Lk 23:2. Tazama pia Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno.
  2. 1:1 Naandika … wa Sosthenesi Majina yanayotajwa na Paulo katika mwanzo wa barua zake kama vile Timotheo na Sila walimsaidia kuandika barua hizo. Wao ni waandishi wenza wa barua hizo. Hawatumi tu salamu. Uandishi wa barua za Paulo ulifanyika kitimu. Yumkini basi Paulo alijadili yatakayoandikwa katika barua zake na watenda kazi wenzie. Hakuziandika katika faragha. Hii ilikuwa desturi ya uandishi wa barua za Kiyunani.
  3. 1:2 wanaomwamini Bwana Kwa maana ya kawaida, “wanaoliitia jina la Bwana”, yaani kuonesha imani katika yeye kwa kumwabudu au kumwomba yeye unapohitaji msaada.
  4. 1:12 ninamfuata Paulo Ina maana pia kuwa Paulo ndiye mwalimu wangu, nami nayafuata mafundisho yake.
  5. 1:12 ninamfuata Petro Ninamfuata Petro itakuwa na maana kuwa Petro ni mwalimu wangu, nami ninayafuata mafundisho yake. Petro yaani, “Kefa”, ambalo ni jina la Petro kwa Kiaramu, mmoja wa mitume kumi na wawili wa Yesu. Majina yote mawili yanamaanisha “mwamba”. Pia katika 3:22; 9:6; 15:5.
  6. 1:17 msalaba Paulo anatumia msalaba kama kielelezo cha Habari Njema, habari ya kifo cha Kristo kwa ajili ya kuwaweka watu huru mbali na dhambi. Msalaba (Kifo cha Kristo) kilikuwa njia ya Mungu ya kuwaokoa watu.