Add parallel Print Page Options

Upendo Uwe Dira Yenu

13 Ninaweza kusema kwa lugha zingine, za wanadamu au za malaika. Lakini ikiwa sina upendo, mimi ni kengele yenye kelele na tuazi linalolia. Ninaweza kuwa na karama ya unabii, ninaweza kuzielewa siri zote na kujua kila kitu kinachopaswa kujulikana, na ninaweza kuwa na imani kuu kiasi cha kuhamisha milima. Lakini pamoja na haya yote, ikiwa sina upendo, mimi ni bure. Ninaweza kutoa kila kitu nilichonacho ili niwasaidie wengine na ninaweza hata kuutoa mwili wangu ili niweze kujisifu.[a] Lakini siwezi kupata chochote kwa kufanya haya yote ikiwa sina upendo.

Upendo huvumilia na ni mwema. Upendo hauna wivu, haujisifu na haujivuni. Upendo hauna kiburi, hauna ubinafsi na haukasirishwi kirahisi. Upendo hautunzi orodha ya mambo waliyoukosea. Upendo haufurahi wengine wanapokosa, lakini daima hufurahia ukweli. Upendo kamwe haukati tamaa kwa watu. Kamwe hauachi kuamini, kamwe haupotezi tumaini na kamwe hauachi kuvumilia.

Upendo hautakoma. Lakini karama zote hizo zitafikia mwisho, hata karama ya unabii, karama ya kusema kwa lugha zingine na karama ya maarifa. Hizi zitakoma kwa sababu maarifa haya na nabii hizi tulizonazo sasa hazijakamilika. 10 Lakini ukamilifu utakapokuja, mambo ambayo hayajakamilika yatakoma.

11 Nilipokuwa mtoto, nilizungumza kama mtoto, niliwaza kama mtoto, na kufanya mipango kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima, niliziacha njia za kitoto. 12 Ndivyo ilivyo hata kwetu. Kwa sasa tunamwona Mungu kwa taswira tu kama ilivyo katika kioo. Lakini, baadaye, tutamwona uso kwa uso. Kwa sasa ninajua sehemu tu, lakini wakati huo nitajua kila kitu, kama ambavyo Mungu amenijua mimi. 13 Hivyo mambo haya matatu yanaendelea; imani, tumaini na upendo. Na lililo kuu zaidi ya haya yote ni upendo.

Footnotes

  1. 13:3 kuutoa mwili wangu ili niweze kujisifu Kwa maana ya kawaida, “ili nichomwe moto”, ambayo inapatikana katika nakala za kale na bora zaidi za Kiyunani. Baadhi ya nakala za kale za Kiyunani zimetumia hapa maneno “hata nikichomwa moto”, kwa maana hii ya “Kujisifu”, tazama 2 Kor 12:9-10.