Add parallel Print Page Options

Habari Njema Kuhusu Yesu Kristo

15 Sasa ndugu zangu, ninataka mkumbuke Habari Njema niliyowahubiri. Mliupokea ujumbe huo na endeleeni kuishi kwa kuufuata. Habari Njema hiyo, ujumbe mliousikia kutoka kwangu, ni njia ya Mungu kuwaokoa. Ni lazima mwendelee kuuamini. Ikiwa mtaacha, kuamini kwenu ni bure.

Niliwapa ujumbe nilioupokea. Niliwaambia ukweli muhimu zaidi ya kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama Maandiko yanavyosema; kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama Maandiko yanavyosema na kwamba alimtokea Petro kisha mitume kumi na wawili. Baada ya hilo, aliwatokea waamini wengine zaidi ya mia tano kwa wakati mmoja. Wengi wao bado wanaishi sasa, lakini wengine wamekwisha kufa. Kisha alimtokea Yakobo na baadaye aliwatokea mitume wote. Mwisho wa yote kabisa alinitokea mimi. Nilikuwa tofauti, kama mtoto anayezaliwa wakati usiostahili.

Mitume wengine wote ni wakuu kuliko mimi. Ninasema hivi kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu. Ndiyo sababu sistahili hata kuitwa mtume. 10 Lakini, kwa sababu ya neema ya Mungu, ndivyo hivi nilivyo. Na neema aliyonipa haikupotea bure bila manufaa. Nilifanya kazi kwa bidii kuliko mitume wengine wote. (Lakini, kwa hakika si mimi niliyekuwa nafanya kazi. Ni neema ya Mungu iliyo ndani yangu.) 11 Hivyo basi, si muhimu ikiwa ni mimi au mitume wengine ndiyo waliowahubiri, sisi sote tunawahubiri watu ujumbe huo huo, na hiki ndicho mlichoamini.

Tutafufuliwa Kutoka kwa Wafu

12 Tunamwambia kila mtu kuwa Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu. Hivyo kwa nini baadhi yenu mnasema watu hawatafufuliwa kutoka kwa wafu? 13 Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, basi Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu. 14 Na ikiwa Kristo hakufufuliwa, ujumbe tunaowahubiri ni bure. Na imani yenu ni bure. 15 Nasi tutakuwa na hatia ya kutoa ushuhuda wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumewahubiri watu kuhusu Yeye, kwa kusema kuwa alimfufua Kristo kutoka kwa wafu. Na ikiwa hakuna anayefufuliwa kutoka kwa wafu, basi Mungu hakumfufua Kristo. 16 Ikiwa wale waliokufa hawatafufuliwa, basi Kristo hakufufuliwa pia. 17 Na ikiwa Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu, basi imani yenu ni bure; bado mngali watumwa wa dhambi zenu. 18 Na watu wa Kristo waliokwisha kufa wamepotea. 19 Ikiwa tumaini letu katika Kristo ni kwa ajili tu ya maisha haya hapa duniani, basi watu watuhurumie sisi kuliko mtu mwingine yeyote.

20 Lakini hakika Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu; ndiye wa kwanza miongoni mwa wafu wote watakaofufuliwa. 21 Kifo huja kwa watu kwa sababu ya tendo la mtu mmoja. Lakini sasa kuna ufufuo kutoka kwa wafu kwa sababu ya mtu mwingine. 22 Ndiyo, kwa sababu sisi sote ni wa Adamu, sisi sote tunakufa. Kwa njia hiyo hiyo, sisi sote tulio wa Kristo, tutakuwa hai tena. 23 Lakini kila mmoja atafufuliwa kwa mpango sahihi. Kristo alikuwa wa kwanza kufufuliwa. Kisha atakaporudi, wale walio wake watafufuliwa. 24 Ndipo mwisho utakuja. Kristo atamwangamiza kila mtawala na kila mamlaka na nguvu. Kisha atampa Mungu Baba ufalme.

25 Kristo lazima atawale mpaka Mungu atakapowaweka adui zake wote chini ya udhibiti wake.[a] 26 Adui wa mwisho kuangamizwa ni kifo. 27 Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu ameweka kila kitu chini ya udhibiti wake.”(A) Inaposema “kila kitu” kimewekwa chini yake, hii ni wazi Mungu peke yake ndiye ambaye hayuko chini yake. Mungu ndiye anayeweka kila kitu chini ya udhibiti wa Kristo. 28 Baada ya kuweka kila kitu chini ya Kristo, ndipo yeye mwenyewe, kama Mwana, atawekwa chini ya Mungu. Katika namna hii Mungu atakuwa mtawala mkuu juu ya kila kitu.

29 Ikiwa hakuna atakayefufuliwa kutoka kwa wafu, sasa watu wanafikiri wanafanya nini kwa kubatizwa kwa ajili ya wale waliokufa? Ikiwa wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini watu wanabatizwa kwa ajili yao?

30 Na vipi kuhusu sisi? Kwa nini tunajiweka katika hatari wakati wote? 31 Ninakumbana na kifo kila siku. Ni kweli, ndugu zangu kwamba ninajivuna kwa sababu ninyi ni wa Kristo Yesu Bwana wetu. 32 Niliwapiga wanyama wa porini kule Efeso. Ikiwa nilifanya hivyo kwa sababu za kibinadamu tu, sijapata kitu. Ikiwa hatufufuliwi kutoka kwa wafu, “basi tule na tunywe, kwa sababu tutakufa kesho.”(B)

33 Msidanganywe: “Marafiki wabaya huharibu tabia njema.” 34 Rudieni kuwaza kwenu kwa usahihi na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hamumjui Mungu. Ninasema hivi ili niwafedheheshe.

Tutakuwa na Mwili wa Namna Gani?

35 Lakini mtu mmoja anaweza kuuliza, “Waliokufa wanafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” 36 Haya ni maswali ya kijinga. Unapopanda kitu fulani, ni lazima kife udongoni kabla hakijawa hai na kuota. 37 Na unapopanda kitu fulani, unachopanda hakina “mwili” sawa na ule kitakachokuwa nao baadaye. Unapanda mbegu, pengine ngano au kitu kingine. 38 Na yeye Mungu hutoa mwili kwa kila aina ya mbegu. 39 Vitu vyote vilivyoumbwa kwa mwili haviko sawa: Wanadamu wana aina moja ya mwili, wanyama wana aina nyingine, ndege wana nyingine na samaki nao wana aina yao. 40 Pia kuna miili ya kimbingu na miili ya kidunia. Lakini uzuri wa miili ya kimbingu ni wa aina yake na uzuri wa miili ya kidunia ni kitu kingine. 41 Jua lina uzuri wa aina yake, mwezi una aina yake na nyota zina aina nyingine ya uzuri. Na kila nyota iko tofauti kwa uzuri wake.

42 Ndivyo itakavyokuwa waliokufa watakapofufuliwa na kuwa hai. Mwili “uliopandwa” kaburini utaharibika na kuoza, lakini utafufuliwa katika uhai usioharibika. 43 Mwili hauna heshima “unapopandwa”. Lakini utakapofufuliwa, utakuwa na utukufu. Mwili unakuwa dhaifu “unapopandwa”. Lakini unapofufuliwa, unakuwa na nguvu nyingi. 44 Mwili unaopandwa ni mwili wa kawaida, wa asili. Utakapofufuliwa utakuwa mwili wa ajabu uliopewa uwezo na Roho.

Kuna mwili wa asili unaoonekana kwa macho. Na hivyo kuna mwili wa Kiroho wa ajabu. 45 Kama Maandiko yanavyosema, “Mtu[b] wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe asili kilichokuwa hai.”(C) Lakini Adamu[c] wa mwisho akafanyika roho. 46 Mtu wa kiroho hakuja kwanza. Mtu wa asili anayeonekana kwa macho ndiye alikuja kwanza; kisha akaja wa kiroho. 47 Mtu wa kwanza alitokana na mavumbi ya dunia. Mtu wa pili alitoka mbinguni. 48 Watu wote ni wa dunia. Wako sawa na yule mtu wa kwanza wa dunia. Lakini wale walio wa mbinguni wako kama mtu wa mbinguni. 49 Tumeivaa sura ya mtu aliyetoka mavumbini, pia tutaivaa sura ya mtu aliyetoka mbinguni.

50 Ninawaambia hili ndugu zangu: Miili yetu na nyama na damu haiwezi kuwa na nafasi katika ufalme wa Mungu. Kitu kitakachoharibika hakiwezi kuwa na sehemu katika kitu kisichoharibika kamwe. 51 Lakini sikilizeni, ninawaambia siri hii: Sote hatutakufa, lakini sote tutabadilishwa. 52 Itachukuwa sekunde moja. Tutabadilishwa kufumba na kufumbua. Hili litatokea parapanda ya mwisho itakapopulizwa. Parapanda itakapolia wale waliokufa watafufuliwa ili waishi milele. Na tutabadilishwa sote. 53 Mungu ataibadilisha miili yetu ili isiharibike kamwe. Mwili huu unaokufa utabadilishwa na kuwa mwili usiokufa. 54 Hivyo mwili huu unaokufa utajivika kutokufa. Hili litakapotokea, ndipo Maandiko yatatimilizwa:

“Mauti imemezwa katika ushindi.(D)
55 Ewe kifo, ushindi wako uko wapi?
    Nguvu yako ya kudhuru iko wapi?”(E)

56 Dhambi ni nguvu ya mauti inayodhuru, na nguvu ya dhambi ni sheria. 57 Lakini tunamshukuru Mungu anayetupa ushindi kupitia Yesu Kristo Bwana wetu!

58 Hivyo, kaka na dada zangu, simameni imara. Msiruhusu kitu chohote kiwabadilishe. Jitoeni nafsi zenu kikamilifu kwa kazi yenu katika Bwana. Mnajua ya kuwa chochote mnachofanya kwa ajili ya Bwana hakitapotea bure bila manufaa.

Footnotes

  1. 15:25 chini ya udhibiti wake Kwa maana ya kawaida, “kuweka chini ya miguu”.
  2. 15:45 Mtu Kwa maana ya kawaida, “nafsi”.
  3. 15:45 Adamu Jina Adamu linamaanisha “mtu”. Inaposema “Adamu wa Mwisho” inamaanisha Kristo, “mtu wa mbinguni”.