Add parallel Print Page Options

Makusanyo kwa Ajili ya Waamini Katika Uyahudi

16 Sasa, kuhusu mchango wa pesa kwa ajili ya watu wa Mungu: Fanyeni kama nilivyoyaambia makanisa ya Galatia kufanya. Siku ya kwanza ya kila wiki, kila mmoja wenu achukue kiasi cha pesa kutoka kwenye pesa zake na azitenge. Akusanye kiasi anachoweza kutokana na anavyobarikiwa. Na hivyo hamtahitaji kukusanya nitakapokuja. Nitakapofika, nitatuma baadhi ya watu wapeleke sadaka yenu Yerusalemu. Hawa watakuwa wale ambao ninyi mtakubali kuwa waende. Nitawatuma na barua ya utambulisho. Ikiwa itakuwa vizuri kwangu kwenda pia, basi tutasafiri pamoja.

Mipango ya Paulo

Nimepanga kupitia Makedonia, hivyo nitakuja kwenu baada ya hapo. Pengine nitakaa kwenu kwa muda. Pengine nitakaa kwenu majira yote ya baridi. Hivyo mtaweza kunisaidia katika safari yangu, kila ninapokwenda. Sitaki kuja kuwaona sasa, kwa sababu nitaweza tu kukaa nanyi kwa muda mfupi, kabla haijanilazimu kwenda mahali pengine. Ninategemea kukaa pamoja nanyi kwa muda mrefu, ikiwa Bwana ataruhusu. Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste. Nitakaa hapa, kwa sababu sasa nimepewa fursa nzuri kwa kazi kubwa na inayokua. Na kuna watu wengi wanaopinga.

10 Timotheo atakapokuja kwenu, mjitahidi akae kwa raha na amani akiwa kwenu. Anafanya kazi kwa ajili ya Bwana kama mimi. 11 Hivyo yeyote miongoni mwenu asikatae kumpokea Timotheo. Msaidieni aendelee katika safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu. Ninategemea atakuja kwangu pamoja na ndugu wengine.

12 Na sasa kuhusu Apolo: Ninamsihi sana aje na ndugu wengine kuwatembelea ninyi huko Korintho. Hajataka kuja sasa, lakini atakuja kwenu atakapopata nafasi.

Paulo Amalizia Barua Yake

13 Iweni waangalifu. Simameni imara katika imani yenu. Mwe jasiri na wenye nguvu. 14 Fanyeni kila kitu katika upendo.

15 Mnajua kuwa Stefana na familia yake walikuwa waamini wa kwanza katika Akaya. Wamejitia katika kazi ya kuwahudumia watu wa Mungu. Ndugu zangu, ninawaomba, 16 mjiweke chini ya uongozi wa watu kama hawa na wengine wanaofanya kazi kwa bidii na kutumika pamoja nao.

17 Ninafurahi kwa sababu Stefana, Fortunato na Akaiko wamekuja. Hamko hapa pamoja nami lakini wamejaza nafasi yenu. 18 Wamekuwa faraja kuu kwangu na kwenu pia. Basi, mnapaswa kuitambua thamani ya watu kama hawa.

19 Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Priska wanawasalimu katika Bwana. Na kanisa linalokutana nyumbani mwao linawasalimu pia. 20 Ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kila mmoja wenu kwa salamu maalum ya watu wa Mungu.[a]

21 Hii ni salamu yangu kwa mkono wangu mwenyewe: Paulo.

22 Ikiwa mtu yeyote hampendi Bwana, mwacheni mtu huyo abaki chini ya laana ya Mungu.

Njoo, Ewe Bwana![b]

23 Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja nanyi.

24 Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu.

Footnotes

  1. 16:20 salamu maalum ya watu wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “busu takatifu”.
  2. 16:22 Njoo, Ewe Bwana Hii ni tafsiri ya Kiaramu marana tha.