Add parallel Print Page Options

Kuhusu Ndoa

Sasa nitazungumza kuhusu mambo yale mliyoniandikia. Mliuliza ikiwa ni bora mwanaume asimguse mwanamke kabisa. Lakini dhambi ya uzinzi ni ya hatari, hivyo kila mwanaume anapaswa kumfurahia mke wake, na kila mwanamke anapaswa kumfurahia mume wake. Mume anapaswa kumtosheleza mkewe, vivyo hivyo mke amtosheleze mume wake. Mke hana mamlaka kabisa juu ya mwili wake, bali mume ana mamlaka juu ya mwili wa mkewe. Mume hana mamlaka kabisa juu ya mwili wake, bali mke ana mamlaka juu ya mwili wa mumewe. Msinyimane miili yenu. Lakini mnaweza kukubaliana kutojamiiana kwa muda ili mtumie muda huo katika maombi. Kisha mkutane tena ili Shetani asiwajaribu kutokana na kushindwa kujizuia tamaa zenu. Ninasema hivi ili kuwaruhusu mtengane kwa muda tu. Lakini hii siyo amri. Mimi ningependa kila mtu angekuwa kama mimi nilivyo. Lakini Mungu amempa kila mtu uwezo tofauti. Huwafanya wengine kuwa hivi na wengine kuwa vile.

Sasa kwa ajili ya wale ambao hawajaoa ama hawajaolewa na kwa ajili ya wajane ninawaambia ya kwamba ni vizuri mkae bila kuoa au kuolewa kama mimi. Lakini ikiwa mtashindwa kudhibiti tamaa zenu, basi mwoe au muolewe. Ni vyema kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.

10 Na sasa ninawaamuru wale walio katika ndoa. Si amri kutoka kwangu, lakini ndivyo Bwana aliamuru. Mke hapaswi kuondoka kwa mume wake. 11 Lakini ikiwa mke anaondoka, anapaswa kukaa bila kuolewa au arudi kwa mume wake. Na mume hapaswi kumtaliki mke wake.

12 Ushauri nilionao kwa wengine unatoka kwangu. Bwana hajatupa mafundisho mengine kuhusu hili. Ukiwa na mke asiyeamini, usimtaliki ikiwa yuko radhi kuendelea kuishi pamoja nawe. 13 Na kama una mume asiyeamini, usimtaliki ikiwa yuko radhi kuendelea kuishi pamoja nawe. 14 Mume asiyeamini ametengwa kwa ajili ya Bwana kupitia mke wake anayeamini. Na mke asiyeamini ametengwa kwa ajili ya Bwana kupitia mume wake anayeamini. Ikiwa hii si sahihi basi watoto wenu wasingefaa kwa ajili ya kumwabudu Mungu. Lakini sasa wametengwa kwa ajili yake.

15 Lakini mume au mke asiyemwamini akiamua kuondoka katika ndoa. Hili linapotokea, ndugu aliye katika Kristo anakuwa huru. Mungu aliwachagua ili muwe na maisha ya amani. 16 Inawezekana ninyi wake mtawaokoa waume zenu; nanyi waume mtawaokoa wake zenu kwani bado hamjui kitakachotokea baadaye.

Ishini Kama Mlivyokuwa Mungu Alivyowaita

17 Kila mmoja wenu anapaswa kuendelea kuishi katika namna ambayo Bwana Mungu amewapa, kuishi kama mlivyoishi Mungu alipowaita. Ninawaambia watu katika makanisa yote kufuata kanuni hii. 18 Mwanaume asibadili tohara yake ikiwa alikuwa ametahiriwa alipoitwa. Ikiwa hakuwa ametahiriwa alipoitwa, asitahiriwe. 19 Kutahiriwa au kutotahiriwa si muhimu. Kilicho muhimu ni kutii amri za Mungu. 20 Kila mmoja wenu awe katika hali aliyokuwa nayo Mungu alipomwita. 21 Usijisikie vibaya ikiwa ulipochaguliwa na Mungu ulikuwa mtumwa. Lakini ikiwa unaweza kujikomboa, basi fanya hivyo. 22 Kama ulikuwa mtumwa Bwana alipokuita, uko huru sasa katika Bwana. Wewe ni wa Bwana. Vivyo hivyo, kama ulikuwa huru ulipoitwa, wewe ni mtumwa wa Kristo sasa. 23 Mungu alilipa gharama kubwa kwa ajili yako, hivyo usiwe mtumwa kwa mtu yeyote tena. 24 Ndugu zangu, katika maisha yenu mapya pamoja na Mungu, kila mmoja wenu anapaswa kuendelea kuwa katika hali ya tohara kama alivyokuwa Mungu alipowaita.

Maswali Kuhusu Kuoa au Kuolewa

25 Sasa nitaandika kuhusu suala jingine mliloniandikia mkiuliza kuhusu watu ambao hawajaoa au kuolewa.[a] Sina amri kutoka kwa Bwana kuhusu hili, lakini haya ni maoni yangu. Na ninaweza kuaminiwa kwa sababu Bwana amenipa rehema. 26 Huu ni wakati mgumu. Hivyo nadhani ni vyema mtu akikaa kama alivyo. 27 Ikiwa umefungwa kwa mke, usijaribu kufunguliwa. Ikiwa hujaoa, usijaribu kuoa. 28 Lakini si dhambi ukiamua kuoa. Lakini waliooa watapata dhiki katika maisha haya, nami ninataka msiipitie dhiki hiyo.

29 Kaka zangu nina maana ya kuwa muda uliosalia ni mchache, wale waliooa waishi kama vile hawajaoa.[b] 30 Wale wanaolia wawe kama wasiolia, wenye furaha wawe kama hawana furaha na wale wanaonunua vitu wawe kama hawavimiliki vitu hivyo. 31 Vitumieni vitu vya ulimwengu pasipo kuviruhusu viwe vya muhimu kwenu. Hivi ndivyo mnapaswa kuishi, kwa sababu ulimwengu huu kwa namna ulivyo sasa, unapita.

32 Nataka msisumbuke. Mwanaume ambaye hajaoa hujishughulisha na kazi ya Bwana naye hujitahidi kumpendeza Bwana. 33 Lakini mwanaume aliyeoa hujishughulisha na mambo ya ulimwengu, ili ampendeze mke wake. 34 Ni lazima afikirie mambo mawili; kumpendeza mke wake na kumpendeza Bwana. Mwanamke ambaye hajaolewa au msichana ambaye hajawahi kuolewa hujishughulisha na kazi ya Bwana. Hutaka kuutoa mwili na roho yake kikamilifu kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya ulimwengu ili ampendeze mume wake. 35 Ninasema hili ili niwasaidie. Si kuwawekea vikwazo, lakini ninataka mwishi katika njia sahihi. Na ninataka mjitoe kikamilifu kwa Bwana pasipo kuchukuliwa katika mambo mengine.

36 Mwanaume anaweza kudhani kuwa hamtendei haki mchumba wake. Mchumba wake huyo anaweza kuwa ameshapita umri mzuri wa kuolewa.[c] Hivyo mwanaume anaweza kujisikia kuwa anapaswa kumwoa mchumba wake huyo. Basi na afanye anachotaka. Si dhambi kwao wakioana. 37 Lakini mwanaume mwingine anaweza kuwa na uhakika akilini mwake ya kuwa hakuna haja ya ndoa, hivyo yuko huru kufanya anachotaka. Ikiwa ameamua moyoni mwake kutomwoa mchumba wake, anafanya jambo sahihi. 38 Hivyo mwanaume anayemwoa mchumba wake anafanya jambo jema, na mwanaume asiyeoa anafanya vyema zaidi.

39 Mwanamke anapaswa kuishi na mume wake kipindi chote mumewe anapokuwa hai. Lakini mume akifa, mwanamke anakuwa huru kuolewa na mwanaume yeyote. Lakini mwanaume huyo lazima awe yule wa Bwana. 40 Ikiwa atabaki kuwa mjane, atakuwa na furaha sana. Haya ni maoni yangu, na ninaamini yanatoka kwa Roho wa Mungu.

Footnotes

  1. 7:25 ambao hawajaoa au kuolewa Kwa maana ya kawaida, “Mabikra au wanawali”.
  2. 7:29 wale waliooa waishi … hawajaoa Lugha ya Paulo ni ya mfano. Huenda ana maana ya kuwa waamini wayaone mahusiano yao katika maisha ya sasa kama ya muda tu na hivyo yana kikomo na hayadumu. Hivyo wasishikamane sana na mali na mahusiano ya sasa.
  3. 7:36 Mchumba wake … wa kuolewa Au “Mchumba wa kiume anaweza akashindwa kutawala tamaa zake.”