Add parallel Print Page Options

Kazi ya Paulo Thesalonike

Ndugu zangu, mnafahamu kuwa safari yetu kuja kwenu ilikuwa yenye nguvu. Lakini kabla ya kuja kwenu, watu wa Filipi walitutenda vibaya kwa kututukana matusi mengi na kutusababishia mateso. Mnafahamu yote kuhusu hilo. Na kisha tulipokuja kwenu, watu wengi huko walitupinga. Tuliwaeleza ninyi Habari Njema za Mungu lakini ni kwa sababu Mungu alitupa ujasiri tulio hitaji. Hatukuwa na kitu cha kupata faida kwa kuwaomba ninyi muiamini Habari Njema. Hatukuwa tunataka kuwafanya wajinga wala kuwadanganya. Hapana, tulifanya hivyo kwa sababu Mungu ndiye aliyetuagiza kazi hii. Na hii ilikuwa baada ya yeye kutupima na kuona ya kuwa tunaweza kuaminiwa kuifanya. Hivyo tunapoongea, tunajaribu tu kumpendeza Mungu, na sio wanadamu. Yeye tu ndiye awezaye kuona kilichomo ndani yetu.

Mnafahamu kuwa hatukujaribu kuwarubuni kwa kusema mambo mazuri juu yenu. Hatukuwa tunatafuta jinsi ya kuzichukua pesa zenu. Hatukutumia maneno ama matendo kuficha tamaa yetu. Mungu anajua ya kuwa huu ni ukweli. Hatukuwa tukitafuta sifa toka kwa watu ama kutoka kwenu au kwa mtu yeyote.

Tulipokuwa pamoja nanyi, kama mitume wa Kristo tulikuwa na uwezo wa kutumia mamlaka yetu kuleta madai ya nguvu kwenu. Lakini tulikuwa wapole kwenu.[a] Tulikuwa kama vile mkunga anavyowahudumia watoto wake wadogo. Ilikuwa ni upendo wetu mkuu sana kwenu uliotufanya tuwashirikishe Habari Njema za Mungu. Zaidi ya hayo yote tulifurahi kuwashirikisha ninyi nafsi zetu wenyewe. Hiyo inadhihirisha ni kwa kiwango gani tuliwapenda. Ndugu zangu, ninajua kuwa mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi kwa bidii. Tulifanya kazi usiku na mchana ili tujitegemee, pasipo kumwelemea mtu yeyote wakati tukifanya kazi ya kuhubiri Habari Njema za Mungu.

10 Tulipokuwa pamoja nanyi enyi mnaoamimi, tulikuwa safi, wa kweli, na wasio na kosa lolote kwa namna tulivyoishi maisha matakatifu. Mnafahamu, kama vile Mungu anavyotenda, kuwa jambo hili ni la kweli. 11 Mnafahamu jinsi tulivyo mtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea wanaye. 12 Tuliwatia moyo, tuliwafariji, na tuliwaambia kuishi maisha mema kwa Mungu. Yeye anawaita muwe sehemu ya maisha mema mbele za Mungu.

13 Pia, tunamshukuru Mungu pasipo kuacha kwa sababu ya namna mlivyoupokea ujumbe wake. Ingawa tuliuleta kwenu, mliupokea si kama ujumbe unaotoka kwa wanadamu, bali kama ujumbe wa Mungu. Kweli hakika ni ujumbe kutoka kwa Mungu, unaofanya kazi kwenu ninyi mnao uamini. 14 Kaka na dada zangu katika Bwana, mmeufuata mfano wa makanisa ya Mungu yaliyoko Uyahudi[b] yaliyo mali ya Kristo Yesu. Nina maana ya kuwa ninyi mlitendewa vibaya na watu wa kwenu, namna ile ile walioamini wa Kiyahudi walivyotendewa vibaya na Wayahudi wenzao. 15 Wayahudi wengine pia walimuua Bwana Yesu na manabii. Na walitulazimisha sisi kuondoka katika mji lenu. Hawampendezi Mungu, na wako kinyume na watu wengine wote. 16 Na wanajaribu kutuzuia tusizungumze na wasio Wayahudi. Wanapofanya hivi wanawazuia watu wasio Wayahudi kuokoka. Na hivyo wanaendelea kuziongeza dhambi zao hata kujaza kipimo. Sasa wakati umefika kwa wao kuadhibiwa na hasira ya Mungu.

Shauku ya Paulo kuwa tembelea tena

17 Kaka na dada zangu, tulikuwa kama yatima, tulitengwa nanyi kwa muda. Lakini hata kama hatukuwa pamoja nanyi, mawazo yetu yalikuwa bado yangali nanyi. Tulitamani sana kuwaona, na tulijitahidi sana kulitimiza hilo. 18 Ndiyo, tulitamani kuja kwenu. Mimi, Paulo, nilijaribu zaidi ya mara moja kuja kwenu, lakini Shetani alituzuia. 19 Ninyi ni tumaini letu, furaha yetu, na taji yetu tutakayojivunia wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu. 20 Mnatuletea heshima na furaha.

Footnotes

  1. 2:7 Lakini tulikuwa wapole kwenu Nakala nyingi za Kiyunani zina “Lakini tulikuwa watoto”.
  2. 2:14 Uyahudi Ni nchi ya kiyahudi ambako Yesu aliishi na kufundisha, pia ndipo mahali ambapo kanisa lilianzia.