Add parallel Print Page Options

Maisha Yanayompendeza Mungu

Kaka na dada zangu sasa nina mambo mengine ya kuwaambia. Tuliwafundisha namna ya kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Nanyi mnaishi hivyo. Na sasa tunawaomba na kuwatia moyo katika Bwana Yesu kuishi zaidi na zaidi katika njia hiyo. Mnafahamu yote tuliyowaamuru kufanya kwa mamlaka ya Bwana Yesu Kristo. Mungu anawataka muwe watakatifu. Anawataka mkae mbali na dhambi za zinaa. Mungu anawataka kila mmoja wenu ajifunze kuuthibiti mwili wake mwenyewe. Tumieni miili yenu kwa namna iliyo takatifu na yenye heshima.[a] Msiruhusu tamaa za mwili kuwatawala kama watu wasiomjua Mungu. Msimtendee vibaya ndugu aliye mwamini wala kuwadanganya katika hili. Bwana atawahukumu watendao hivyo. Tumekwisha kuwaambia juu ya hili na kuwaonya. Mungu alituita kuwa watakatifu na safi. Hivyo kila anayekataa kuyatii mafundisho haya anakataa kumtii Mungu, siyo wanadamu. Na Mungu ndiye anayewapa ninyi Roho Mtakatifu.

Hatuna haja ya kuwaandikia juu ya kuwa na upendo kwa katika Kristo. Mungu amekwisha kuwafundisha kupendana ninyi kwa ninyi. 10 Ukweli ni kuwa, mnawapenda wanaoamini wote walioko Makedonia. Tunawatia moyo sasa, kuuonyesha upendo wenu zaidi na zaidi.

11 Fanyeni kila mnaloweza kuishi maisha ya amani. Mjishugulishe na mambo yenu wenyewe, na mfanye kazi kwa mikono yenu wenyewe,[b] kama tulivyowaambia mwanzo. 12 Mkifanya mambo haya, ndipo wale wasioamini wataheshimu namna mnavyoishi. Na hamtawategemea wengine.

Kuja Kwa Bwana

13 Kaka na dada, tunawataka mfahamu habari za wale waliokufa. Hatupendi muwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. 14 Tunaamini kuwa Yesu alikufa, ila tunaamini pia kuwa alifufuka. Hivyo tunaamini kuwa Mungu atawaleta katika uzima kupitia Yesu kila aliyekufa na kukusanywa pamoja naye.

15 Tunalowaambia sasa ni ujumbe wake Bwana. Sisi ambao bado tu hai Bwana ajapo tena tutaungana nae, lakini hatutawatangulia wale waliokwisha kufa. 16 Bwana mwenyewe atakuja kutoka mbinguni pamoja na sauti kuu yenye agizo, na sauti kubwa kutoka kwa malaika mkuu, na ishara ya Mungu ya mlio wa tarumbeta. Na watu waliokufa walio wake Kristo watafufuliwa kwanza. 17 Baada ya hayo, sisi ambao bado tungali hai mpaka wakati huo tutakusanywa pamoja na wale waliokwisha kufa. Tutachukuliwa juu mawinguni na kukutana na Bwana angani. Na tutakuwa na Bwana milele. 18 Hivyo tianeni moyo ninyi kwa ninyi kwa maneno haya.

Footnotes

  1. 4:4 Au “Mungu anamtaka kila mmoja wenu ajue namna ya kutafuta na kupata na kuoa mke kwa namna iliyo takatifu na inayo leta heshima.”
  2. 4:11 mfanye kazi … yenu wenyewe Au mjipatie fedha zenu wenyewe. Wathesalonike wengi walikuwa watu wenye kufanya kazi za mikono ama vibarua kama vile Paulo mwenyewe alivyokuwa.