Add parallel Print Page Options

Uwe tayari kwa ujio wa Bwana

Na sasa ndugu zangu, hatuna haja ya kuwaandikia juu ya nyakati na tarehe. Ninyi mnafahamu vizuri kuwa siku ambayo Bwana atakuja itakuwa ya kushitukiza, kama mwizi anavyokuja usiku. Watu watasema, “tuna amani na tuko salama.” Wakati huo ndipo uharibifu utakapowajia haraka, kama maumivu anayoyapata mwanamke anapojifungua. Na watu hao hawataweza kukwepa.

Lakini ninyi ndugu zangu, hamuishi katika giza. Na hivyo ile siku haitawashangaza kama mwivi. Nyote ni watu wa nuru. Ni watu wa mchana. Hatuko katika usiku wala giza. Hivyo tusiwe kama watu wengine. Tusiwe wasinziao. Tuwe macho na wenye kiasi. Watu walalao, hulala usiku. Watu wanywao kupita kiasi, hunywa usiku. Bali sisi ni watu wa mchana, hivyo tujitawale wenyewe. Tuvae imani na upendo vitulinde. Na tumaini la wokovu liwe kwetu kama kofia ya vita.

Mungu hakutuchagua tuangamie katika hasira yake. Mungu alituchagua tuwe na wokovu katika Bwana wetu Yesu Kristo. 10 Yesu alikufa kwa ajili yetu ili tuishi pamoja nae. Haijalishi kama tu hai au wafu atakapokuja. 11 Hivyo farijianeni ninyi kwa ninyi na msaidiane kukua imara katika imani, kama mnavyofanya sasa.

Maagizo ya Mwisho na Salamu

12 Tunawaomba mwatambue wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao, kama wafuasi wa Bwana, wanatumika kama viongozi wenu na kuwafundisha namna ya kuishi. 13 Wapeni heshima ya hali ya juu na upendo kwa sababu ya kazi wanayofanya.

Ishini kwa amani kila mmoja na mwenzake. 14 Tunawasihi, kuwaonya wale wanaokataa kuishi kwa kuwajibika.[a] Watieni moyo wanaoogopa. Wasaidieni walio dhaifu. Mvumilieni kila mmoja. 15 Asiwepo anae jaribu kulipiza baya kwa baya. Lakini kila mara mfanye lililo jema kwa kila mmoja wenu na kwa watu wote.

16 Mwe na furaha daima. 17 Msiache kuomba. 18 Shukuruni kwa kila jambo. Hivi ndivyo Mungu anavyotutaka tuishi katika Kristo Yesu.

19 Msiizimishe kazi ya Roho Mtakatifu. 20 Msiuchukulie unabii kama kitu kisicho cha muhimu. 21 Lakini pimeni kila kitu. Lishikeni lililo jema, 22 na mkae mbali na kila aina ya ovu.

23 Tunaomba kwamba Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, atawafanya muwe watakatifu mkiwa wake. Tunaomba kwamba katika roho yote, nafsi yote, na mwili mzima mtahifadhiwa salama pasipo lawama Bwana wetu Yesu Kristo atakapokuja. 24 Yeye awaitae atawatendea haya. Mnaweza kumtumainia.

25 Kaka na dada zangu, tafadhali mtuombee. 26 Wasalimuni ndugu wote kwa salamu maalum ya watu wa Mungu.[b] 27 Ninawaagiza kwa mamlaka ya Bwana kuusoma walaka huu kwa waamini wote huko. 28 Neema ya Bwana wetu Yesu kristo iwe nanyi nyote.

Footnotes

  1. 5:14 kuwajibika Ikiwa na maana ya “kuishi kwa kufuata utaratibu unaofaa” Kuishi pasipo kuwajibika ni kutofanya kazi.
  2. 5:26 salamu maalum ya watu wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “busu takatifu”.