Add parallel Print Page Options

Tunataka tuwaambie juu ya Neno[a] linalo toa uzima. Yeye aliyekuwepo tangu mwanzo. Huyu ndiye yule tuliyemsikia na kumwona kwa macho yetu. Tuliyaona mambo aliyeyafanya, na mikono yetu ilimgusa. Ndiyo, yeye aliye uzima alidhihirishwa kwetu. Tulimwona, na hivyo tunaweza kuwaeleza wengine juu yake. Sasa tunawaeleza habari kwamba yeye ndiye uzima wa milele aliyekuwa pamoja na Mungu Baba na alidhihirishwa kwetu. Tuna wasimulia mambo tuliyoyaona na kuyasikia kwa sababu tunawataka muwe na ushirika pamoja nasi. Ushirika tulionao ni pamoja na Mungu Baba na mwanaye Yesu Kristo. Tunawaandikia mambo haya ili furaha yetu iwe kamili.

Mungu Anatusamehe Dhambi Zetu

Tulisikia mafundisho ya kweli toka kwa Mungu. Na sasa tunayasimulia kwenu. Mungu ni nuru, na ndani yake hamna giza. Kwa hiyo kama tukisema kuwa tunashirikiana na Mungu, lakini tukaendelea kuishi katika giza, tunakuwa ni waongo, tusioifuata kweli. Tunapaswa kuishi katika nuru, ambamo Mungu yupo. Kama tunaishi katika nuru, tunashirikiana sisi kwa sisi, na sadaka ya damu yake Yesu, Mwana wa Mungu, inatutakasa kila dhambi.

Kama tukisema kuwa hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na tumeikataa kweli. Lakini kama tukiungama dhambi zetu, Mungu atatusamehe. Tunaweza kumwamini Mungu kufanya hili. Kwa sababu Mungu daima hufanya lililo haki. Atatufanya tuwe safi toka kila dhambi tuliyofanya. 10 Kama tukisema kuwa hatujafanya dhambi, tunasema kuwa Mungu ni mwongo na tumeyakana mafundisho yake.

Footnotes

  1. 1:1 Neno Kwa Kiyunani neno hili ni logos, lenye maana mawasiliano ya aina yoyote. Hapa, ina maana kuwa Kristo ni Njia ambayo Mungu aliwajulisha watu kuhusu yeye mwenyewe.