Add parallel Print Page Options

Yesu ni Msaidizi Wetu

Wapendwa wanangu, ninawaandikieni waraka huu ili kwamba msitende dhambi. Ila kama yeyote akitenda dhambi, tunaye Yesu Kristo wa kutusaidia. Yeye daima alitenda haki, kwa hiyo anaweza kututetea mbele za Mungu Baba. Yesu ndiye njia ambapo dhambi zetu zinaondolewa. Naye haziondoi dhambi zetu tu bali anaziondoa dhambi za watu wote.

Kama tukitii mambo ambayo Mungu ametuamuru kuyafanya, tunapata uhakika ya kuwa tunamjua. Kama tukisema kuwa tunamjua Mungu lakini hatuzitii amri zake, tunasema uongo. Kweli haimo ndani mwetu. Lakini tunapotii mafundisho ya Mungu, kwa hakika upendo wake unakamilika ndani yetu. Hivyo ndivyo tunavyojua kuwa tunaishi ndani yake. Kama tukisema kuwa tunaishi ndani ya Mungu, ni lazima tuishi kwa namna ambvyo Yesu aliishi.

Yesu Alituagiza Kuwapenda Wengine

Wapendwa rafiki zangu, siwaandiki ninyi amri mpya. Ni amri ile ile ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ni fundisho lile lile ambalo mmekwishalisikia. Lakini kile ninachokiandika pia ni amri mpya. Ni kweli; Mnaweza kuiona kweli ndani ya Yesu na ndani yenu ninyi wenyewe. Giza linatoweka, na nuru ya kweli tayari inang'aa.

Mtu anaweza kusema, “Niko nuruni,” lakini ikiwa anamchukia ndugu yeyote katika familia ya Mungu, basi angali bado katika giza. 10 Wao wanaowapenda ndugu wanaishi katika nuru, na hakuna kitu ndani yao cha kuwafanya watende mabaya. 11 Lakini yeyote anayemchukia nduguye wa kike au wa kiume yuko gizani. Anaishi katika giza. Hajui anakoenda, kwa sababu giza limemfanya asiweze kuona.

12 Ninawaandikia, ninyi watoto wapendwa,
    kwa sababu dhambi zenu zimesamehewa kwa njia ya Kristo.
13 Ninawaandikia, ninyi akina baba,
    kwa sababu mnamjua yeye aliyekuwepo tangu mwanzo.
Ninawaandikia, ninyi vijana,
    kwa sababu mmemshinda yule mwovu.
14 Ninawaandikia ninyi watoto,
    kwa sababu mnamjua Baba.
Ninawaandikia ninyi, akina baba,
    kwa sababu mnamfahamu yeye aliyekuwepo tangu mwanzo.
Ninawaandikia ninyi, vijana,
    kwa sababu mna nguvu.
Mafundisho ya Neno la Mungu yimo ndani yenu,
    na mmemshinda yule mwovu.

15 Msiipende dunia hii ya uovu wala mambo yaliyomo ndani yake. Kama mkiipenda dunia, upendo wa baba haumo ndani yenu. 16 Yote yaliyomo katika dunia: yaani, tamaa halisi za kibinadamu, tamaa kwa yale mabaya tunayoyaona, na kiburi cha vitu tulivyonavyo. Lakini hakuna hata mojawapo ya haya litokalo kwa Baba. Yote yanatoka katika dunia. 17 Dunia inapita, na mambo yote ambayo watu wanayataka kutoka katika dunia nayo yanapita. Lakini yeyote atendaye mambo ambayo Mungu anayataka ataishi milele.

Msiwafuate Maadui wa Kristo

18 Wapendwa wanangu, mwisho umekaribia! Mmesikia kuwa adui wa Kristo anakuja. Na sasa maadui wengi wa Kristo tayari wapo hapa. Hivyo tunajua kwamba mwisho umekaribia. 19 Maadui hawa walikuwa miongoni mwetu, lakini walituacha. Hawakuwa wenzetu hasa. Kama wangelikuwa kweli wenzetu, wangebaki pamoja nasi. Lakini walituacha. Hii inaonesha kuwa hakuna hata mmoja wao aliyekuwa kwa hakika mwenzetu.

20 Mnayo karama[a] aliyowapa Yeye Aliye Mtakatifu.[b] Hivyo nyote mnaijua kweli. 21 Mnadhani ninawaandikia waraka huu kwa sababu hamuijui kweli? Hapana! Ninawaandikia kwa sababu mnaijua kweli. Na mnajua kuwa hakuna uongo utokao katika kweli.

22 Ni nani basi aliye mwongo? Ni yeye anayesema kuwa Yesu siyo Kristo. Yeyote anayesema hivyo ni adui wa Kristo. Yeye huyo asiyemwamini Baba wala Mwana. 23 Yeyote asiyemwamini Mwana hana Baba, ila yeye anayemkubali Mwana anaye Baba pia.

24 Mnapaswa kuendelea kuyafuata mafundisho mliyoyasikia tangu mwanzo. Kama mkifanya hivyo, mtakuwa siku zote katika Mwana na katika Baba. 25 Na hili ndilo ambalo Mwana ameliahidi kwetu sisi, uzima wa milele.

26 Ninawaandikia barua hii juu ya wale ambao wanataka kuwapotosha katika njia isiyo sahihi. 27 Kristo aliwapa karama maalumu.[c] Nanyi bado mngali na karama hiyo ndani yenu. Hivyo hamumhitaji yeyote kuwafundisha. Karama aliyowapa inawafundisha juu ya kila jambo. Ni karama ya kweli, si ya uongo. Hivyo endeleeni kuishi katika Kristo, kama karama yake ilivyowafundisha.

28 Ndiyo, wanangu wapendwa, ishini ndani yake. Kama tukifanya hivyo, hatutakuwa na hofu siku kristo atakapo kuja tena. Hatutahitaji kujificha na kuwa na aibu ajapo. 29 Mnajua ya kwamba daima Kristo alifanya yaliyo ya haki. Vivyo hivyo mnajua pia ya kwamba wote watendao haki ni watoto wa Mungu.

Footnotes

  1. 2:20 karama Kwa maana ya kawaida, “upako”. Hili linaweza kumaanisha Roho Mtakatifu. Au Mafundisho au Kweli kama ilivyo katika mstari wa 24. Pia katika mstari wa 27.
  2. 2:20 Mtakatifu Mungu au Kristo.
  3. 2:27 karama maalumu Kwa ufasaha “upako”.