Add parallel Print Page Options

Salamu kutoka kwa Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo.

Kwenu ninyi nyote mliopokea imani inayowapa baraka sawa nasi. Mlipewa imani kwa sababu Mungu wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo hufanya yaliyo mema na haki.

Mpewe neema na amani zaidi na zaidi, kwa sababu sasa mnamjua Mungu na Yesu Bwana wetu.

Mungu Ametupa Kila Kitu Tunachohitaji

Yesu ana nguvu ya Mungu. Na nguvu yake imetupa heshima ili tuishi maisha yanayomtukuza na kumpendeza Mungu. Tuna vitu hivi kwa sababu tunamjua. Yesu alitualika kwa utukufu na nguvu ya uungu wake. Na kupitia haya, alitupa ahadi kuu mno. Ili kwamba kwa hizo mnaweza kushiriki katika kuwa kama Mungu na ukaepuka maangamizo ya kiroho yanayokuja kwa watu ulimwenguni kwa sababu ya mambo maovu wanayotaka.

Kwa sababu mna baraka hizi, jitahidini kadri mnavyoweza kuongeza mambo haya: katika imani yenu ongezeni wema, katika wema wenu ongezeni maarifa; katika maarifa yenu ongezeni kiasi; katika kiasi chenu ongezeni uvumilivu; katika uvumilivu wenu ongezeni kumwabudu Mungu; katika kumwabudu Mungu kwenu ongezeni huruma kwa ndugu katika Kristo na kwa wema huu ongezeni upendo. Ikiwa mambo haya yote yatakaa ndani yenu na kukua, mtazaa matunda mazuri yakiwa ni matokeo ya ninyi kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini wale wasiokua na sifa hizi ndani yao ni wasiyeona. Hawataweza kuona kwa uwazi yale waliyonayo. Wamesahau kuwa dhambi zao ziliondolewa kutoka kwao na wakawa safi.

10 Ndugu zangu, Mungu aliwaita na akawachagua ili muwe wake. Jitahidini mhakikishe kuwa mnapata yale aliyonayo Mungu kwa ajili yenu. Mkifanya hivi hamtajikwa na kuanguka. 11 Na mtakaribishwa kwa baraka kuu katika ufalme usio na mwisho, ufalme wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

12 Mnayajua mambo haya tayari. Mko imara katika kweli mliyo nayo. Lakini daima nitajitahidi kuwakumbusha. 13 Nikiwa bado naishi hapa duniani, nadhani ni sahihi kwangu kuwakumbusha. 14 Ninajua kuwa ni lazima nitauacha mwili huu kitambo kijacho kwani Bwana wetu Yesu Kristo amenionyesha. 15 Nitafanya kwa kadri ninavyoweza kuhakikisha kuwa daima mtayakumbuka mambo haya hata baada ya kifo changu.

Tuliuona Utukufu wa Kristo

16 Tuliwaambia kuhusu nguvu ya Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake katika nguvu kuu. Mambo tuliyowaambia hayakuwa simulizi za kuvutia zilizotungwa watu. Hapana, tuliuona ukuu wa Yesu kwa macho yetu wenyewe. 17 Yesu aliisikia sauti ya Mungu Mkuu na Mwenye Mtukufu alipopokea heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba. Sauti ilisema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda. Ninafurahishwa naye.” 18 Nasi tuliisikia sauti hiyo. Sauti hiyo ilitoka mbinguni tulipokuwa na Yesu juu ya mlima mtakatifu.[a]

19 Hili linatufanya tuwe na ujasiri kwa yale waliyosema manabii. Na ni vizuri ninyi mkifuata yale waliyosema, ambayo ni kama mwanga unaoangaza mahali penye giza. Mna mwanga unaoangaza mpaka siku inapoanza na nyota ya asubuhi huleta mwanga mpya katika fahamu zenu. 20 Jambo la muhimu kuliko yote ambalo ni lazima mlielewe ni hili ya kwamba hakuna unabii katika Maandiko unaotokana na mawazo ya nabii. 21 Nabii hakusema kile alichotaka kusema. Lakini wanadamu waliongozwa na Roho Mtakatifu kusema ujumbe uliotoka kwa Mungu.

Footnotes

  1. 1:17-18 Tukio hili limeelezwa katika Injili. Tazama Mt 17:1-8; Mk 9:2-8; Lk 9:28-36.