Add parallel Print Page Options

Yesu Atarudi

Rafiki zangu, hii ni barua yangu ya pili kuwaandikia. Barua zote mbili nimewaandikia ili kusaidia fikra zenu njema zikumbuke kitu. Ninataka mkumbuke maneno ambayo manabii watakatifu walisema huko nyuma. Na mkumbuke amri ambayo Bwana na Mwokozi wetu aliwapa. Aliwapa amri hiyo kupitia mitume wake waliowafundisha.

Ni muhimu kwenu kuelewa kitakachotokea siku za mwisho. Watu watawacheka kwa yale mliyofundishwa. Wataishi kwa kufuata maovu wanayotaka kufanya. Watasema, “Yesu aliahidi kuwa atarudi. Yuko wapi? Baba zetu wamekufa, lakini ulimwengu unaendelea kama ambavyo umekuwa tangu ulipoumbwa.”

Lakini watu hawa hawataki kukumbuka kilichotokea zamani. Anga ilikuwepo, na Mungu aliiumba dunia kwa kutumia maji. Hili lilitokea kwa neno la Mungu. Kisha ulimwengu uliangamizwa kwa maji wakati wa gharika. Na neno hilo hilo la Mungu linaiweka anga na dunia tuliyonayo sasa. Vimewekwa ili vichomwe moto. Vimewekwa kwa ajili ya siku ya hukumu na kuangamia kwa watu wote walio kinyume na Mungu.

Lakini rafiki zangu wapendwa msisahau jambo hili moja ya kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu moja, na miaka elfu moja ni kama siku moja. Bwana hakawii kufanya alichoahidi kama ambavyo watu wengine wanaelewa maana ya kukawia. Lakini Bwana amewavumilia. Hataki mtu yeyote aangamie. Anataka kila mtu abadili njia zake na aache kutenda dhambi.

10 Lakini siku atakayorudi Bwana itakuwa siku isiyotarajiwa na kila mtu kama ambavyo mwizi huja. Anga itatoweka kwa muungurumo wa sauti kuu. Kila kitu kilicho angani kitateketezwa kwa moto. Na dunia na kila kitu kilichofanyika ndani yake kitafunuliwa na kuhukumiwa[a] na Mungu. 11 Kila kitu kitateketezwa kwa namna hii. Sasa mnapaswa kuishi kwa namna gani? Maisha yenu yanapaswa kuwa matakatifu na yanayompa heshima Mungu. 12 Mnapaswa kuangalia mbele, kuiangalia siku ile ya Bwana, mkifanya kile mnachoweza ili ije mapema. Itakapofika, anga itateketezwa kwa moto na kila kitu kilicho angani kitayeyuka kwa joto. 13 Lakini Mungu alituahidi. Na tunasubiri alichoahidi, yaani anga mpya na dunia mpya. Mahali ambapo hakia unaishi.

14 Rafiki wapendwa, tunasubiri hili litokee. Hivyo jitahidini kadri mnavyoweza msiwe na dhambi wala kosa. Jitahidini kuwa na amani na Mungu. 15 Kumbukeni kuwa tumeokolewa kwa sababu Bwana wetu ni mvumilivu. Ndugu yetu mpendwa Paulo aliwaambia jambo hili hili alipowaandikia kwa hekima aliyopewa na Mungu. 16 Ndivyo anavyosema katika barua zake zote anapoandika kuhusu mambo haya. Sehemu zingine katika barua zake ni ngumu kuzielewa, na kuna baadhi ya watu huzifafanua vibaya. Watu hawa ni wajinga na wasioaminika. Watu hawa hutoa pia maana potofu kwa Maandiko mengine. Lakini kwa kufanya hivi wanajiangamiza wao wenyewe.

17 Rafiki wapendwa, tayari mnajua kuhusu hili. Hivyo iweni waangalifu. Msiwaruhusu watu hawa waovu wakawaongoza kwenye upotevu kwa mabaya wanayofanya. Jichungeni msipoteze imani yenu iliyo imara. 18 Lakini mkue katika neema na kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu ni wake, sasa na hata milele! Amina.

Footnotes

  1. 3:10 kitafunuliwa na kuhukumiwa Nakala zingine za kale za Kiyunani zina “zitaungua”, na moja ina “zitatoweka”.