Add parallel Print Page Options

Askari Mwaminifu wa Kristo Yesu

Kwako wewe mwanangu, uwe hodari kwa njia ya neema inayopatikana kwa Kristo Yesu. Yachukue mambo uliyoyasikia kwangu mbele za mashahidi wengi, na yakabidhi kwa watu waaminifu ambao watakuwa na uwezo wa kuwafundisha wengine pia. Kama askari mwaminifu wa Kristo Yesu, jiunge nami katika mateso. Hakuna hata mmoja anayefanya kazi kama askari kisha akajishughulisha pia na mambo ya kiraia. Hii ni wa sababu anataka kumfurahisha kamanda wake. Na kama kuna mtu anayeshiriki katika mashindano ya riadha, hawezi kushinda taji endapo hatashindana kwa kufuata sheria. Mkulima mwenye juhudi anastahili kuwa wa kwanza kufurahia sehemu ya mavuno yake. Nakutaka wewe kuyafikiri ninayokuambia na Bwana atakupa uwezo wa kuyaelewa mambo haya yote.

Endelea kumkumbuka Yesu Kristo, aliyefufuka kutoka kwa wafu, na ni kutoka ukoo wa Daudi. Na huu ndiyo Habari Njema ninayoihubiri. Kwa sababu ya Habari Njema ninateseka, hadi hatua ya kufungwa kwa minyororo kama mhalifu. Lakini ujumbe wa Mungu haujafungwa. 10 Kwa hiyo nayavumilia yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili na wao waweze kuufikia wokovu unaopatikana katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.

11 Na hapa kuna usemi wa kuaminiwa:

Kama tumekufa pamoja naye,
    tutaweza kuishi naye pia.
12 Kama tutastahimili, tutaweza pia kumiliki pamoja naye.
    Kama tutamkana yeye, naye atatukana sisi.
13 Kama hatutakuwa waaminifu,
    yeye anabaki kuwa mwaminifu,
    kwa sababu hawezi kujikana mwenyewe.

Mtendakazi Ampendezaye Mungu

14 Endelea kuwakumbusha watu juu ya mambo haya. Waonye kwa mamlaka mbele za Mungu wasipigane juu ya maneno. Mapigano hayo hayana mambo mazuri, bali huwaharibu wanaoyasikiliza. 15 Jitahidi kujionesha mwenyewe kuwa umekubaliwa na Mungu, kama mtumishi asiye na kitu cho chote cha kumfadhaisha na anayeufanyia kazi ujumbe wa kweli ya Mungu katika njia sahihi.

16 Bali uyaepuke majadiliano ya kijinga ya kidunia, ambayo huwapeleka watu mbali na Mungu, 17 na mafundisho ya wale wanaoyachukua mafundisho hayo wanaenea kama saratani mwilini. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto, 18 aliyeiasi na kuikosa kweli. Wanasema kuwa ufufuo kutoka kwa wafu kwa watu wote umekwisha kutokea, na wanageuza imani za watu wengine.

19 Hata hivyo, msingi ulio imara ambao Mungu aliuweka unasimama imara, na maneno haya yameandikwa juu yake: “Bwana anawajua wale walio wake,”(A) na “Kila anayesema kuwa ni wa Bwana aweze kuuacha ubaya.”

20 Ndani ya nyumba kubwa hakuna vyombo vya dhahabu na fedha pekee, bali hata vya udongo na mbao. Na vingine ni vya kutumika kwa matukio maalumu, na vingine ni kwa matumizi ya kawaida. 21 Hivyo mtu akitakaswa kutoka maovu yote, atakuwa mtakatifu na chombo maalumu cha kutumiwa na Bwana kilicho tayari kwa kila kazi njema.

22 Bali uzikimbie tamaa za ujana na kuyatafuta maisha ya haki, imani, upendo na amani, pamoja na wote wanaomwita Bwana kwa mioyo safi. 23 Nyakati zote ujiepushe na mabishano ya kijinga, kwa sababu unajua kuwa huleta mabishano makubwa. 24 Kwani mtumwa wa Bwana hapaswi kubishana, bali kuwa mkarimu kwa watu wote, mwenye ujuzi katika kufundisha na asiye mtukanaji. 25 Anapaswa kuwaelekeza wapinzani wake kwa upole katika tumaini kwamba Mungu anaweza kuwasaidia hao kutubu na kuujua ukweli, 26 na ili waweze kurudi katika fahamu zao na kuuepuka mtego wa adui, ambako wameshikiliwa kama mateka na Ibilisi na wamelazimishwa kuyafanya mapenzi yake.