Add parallel Print Page Options

Nguvu ya Paulo Inatoka Katika Udhaifu

12 Inanipasa kuendelea kujivuna juu yangu mwenyewe. Hiyo haitasaidia, lakini nitazungumza juu ya maono na mafunuo kutoka kwa Bwana. Ninamjua mtu mmoja[a] katika Kristo aliyechukuliwa juu katika mbingu ya tatu. Hili lilitokea miaka 14 iliyopita. Sifahamu ikiwa mtu huyu alikuwa ndani ya mwili wake au nje ya mwili wake, lakini Mungu anajua. 3-4 Na ninajua kuwa mtu huyu alichukuliwa juu paradiso. Sijui kama alikuwa katika mwili wake au nje ya mwili wake. Mungu pekee ndiye anajua. Lakini mtu huyu aliyasikia mambo ambayo hana uwezo wa kuyasimulia. Alisikia mambo ambayo mtu yeyote anaruhusiwa kuyasema. Nitajivunia mtu wa namna hiyo, lakini sitajivuna juu yangu mwenyewe. Nitajivuna tu katika madhaifu yangu.

Lakini ikiwa nilitaka kujivuna, sitakuwa nikizungumza kama mjinga, kwa sababu ningekuwa nasema iliyo kweli. Lakini sitajivuna tena zaidi, kwa sababu sitaki watu wanifikirie kwa ubora zaidi kuliko wanavyoniona nikitenda ama kusikia ninayosema.

Lakini imenipasa kutojivuna zaidi juu ya mambo ya ajabu yaliyoonyeshwa kwangu. Kwa sababu hiyo nilipewa tatizo lenye maumivu;[b] malaika toka kwa Shetani; aliyetumwa kwangu kunitesa, ili nisiweze kufikiri kwamba mimi ni bora zaidi kuliko watu wengine. Nilimwomba Bwana mara tatu kuliondoa tatizo hili kwangu. Lakini Bwana alisema, “Neema yangu ndiyo unayoihitaji. Ni pale tu unapokuwa dhaifu ndipo kila kitu kinapoweza kufanyika katika uwezo wangu.” Hivyo nitajivunia udhaifu wangu kwa furaha. Hapo ndipo uweza wa Kristo unaweza kukaa ndani yangu. 10 Ndiyo, nina furaha kuwa na madhaifu ikiwa ni kwa ajili ya Kristo. Nina furaha kuaibishwa na kupitia magumu. Nina furaha ninapoteswa na kupata matatizo, kwa sababu ni pale nilipodhaifu ndipo ninapokuwa na nguvu.

Upendo wa Paulo kwa Waamini wa Korintho

11 Nimekuwa nikizungumza kama mjinga, lakini ninyi ndiyo mliosababisha nikafanya hivyo. Ninyi ndiyo mnaopaswa kuzungumza mema juu yangu. Mimi si kitu, lakini mimi si myonge kwa njia yeyote ile kwa hao “mitume wakuu”. 12 Nilipokuwa pamoja nanyi, nilifanya kwa uvumilivu wote vitu vilivyo nilidhihirisha kuwa mimi ni mtume kwa ishara, maajabu na miujiza. 13 Kwa hiyo mlipokea kila kitu ambacho makanisa yote yalipata. Kitu kimoja tu ndicho kilikuwa cha tofauti na cha kipekee: Sikuwa mzigo au msumbufu kwenu. Mnisamehe kwa hilo.

14 Niko tayari sasa kuwatembelea kwa mara ya tatu, na sitakuwa mzigo kwenu. Mimi sitafuti kitu chochote kilicho chenu. Ninawataka ninyi tu. Watoto wasiweke akiba vitu vya kuwapa wazazi wao. Wazazi wanapaswa kuweka akiba vitu vya kuwapa watoto wao. 15 Kwa hiyo ninayo furaha kutumia kile nilichonacho kwa ajili yenu. Na mimi mwenyewe nitajitoa kikamilifu kwa ajili yenu. Je, kama upendo wangu kwenu utakuwa mkubwa, upendo wenu kwangu utapungua?

16 Ni wazi kuwa sikuwa mzigo kwenu, lakini baadhi yenu wanadhani kuwa nilikuwa mjanja, na kutumia hila kuwaweka mtegoni. 17 Je, niliwadanganya kwa kuwatumia mtu yeyote kati ya wale niliyowatuma kwenu? Mnafahamu kuwa sikufanya hivyo. 18 Nilimwomba Tito aje kwenu, na nilimtuma kaka yetu afuatane naye. Tito hakuwadanganya, je alifanya hivyo? Hapana! Na kwa hiyo mjue kuwa matendo yangu na tabia yangu ilikuwa ya dhati kama ilivyokuwa kwake.

19 Je! Mnadhani tumekuwa tukijitetea? Hapana, tunasema haya katika Kristo na mbele za Mungu. Ninyi ni rafiki zetu wapendwa, na kila tunachofanya tunakifanya ili muwe imara. 20 Ninafanya hivi kwa sababu ninaogopa kuwa nitakapokuja, hamtakuwa kama vile ninavyotaka muwe. Na pia nina wasiwasi kuwa sitakuwa kwa namna ile mnayotaka mimi niwe. Nina hofu kuwa nitawakuta mkibishana, wenye wivu, wenye hasira, mkipigana kwa ubinafsi wenu, wenye misemo mibaya, watetaji, wenye kiburi, na machafuko huko. 21 Nina wasiwasi kuwa nitakapokuja kwenu, Mungu wangu ataninyenyekeza tena mbele yenu. Nitalazimika kuomboleza kwa ajili ya wale ambao wametenda dhambi. Wengi wao hawajarejea na kutubia maisha yao ya uovu, dhambi za zinaa, na mambo ya aibu waliyotenda.

Footnotes

  1. 12:2 mtu mmoja Katika sura 12:2-5 Paulo huenda anasema habari zake mwenyewe.
  2. 12:7 tatizo lenye maumivu Kwa maana ya kawaida, “mwiba mwilini”.