Add parallel Print Page Options

Mambo Maovu Yatatokea

Kaka na dada, tuna jambo la kuwaambia juu ya kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunataka kuzungumza nanyi juu ya wakati huo tutakapokusanyika pamoja naye. Msikubali kufadhaishwa na kutiwa kuhofu ikiwa mtasikia kwamba siku ya Bwana tayari imekwishawadia. Wengine wanaweza kusema kwamba wazo hili limetoka kwetu katika jambo alilotuambia Roho, au tulilosema, au katika barua tuliyoiandika. Msidanganywe na chochote wanachoweza kusema kuhusu kuja kwa Bwana. Siku hiyo ya Bwana haitakuja mpaka itanguliwe na kukengeuka kwa wanadamu na kumwacha Mungu. Na siku hiyo haitakuja mpaka ajitokeze kwanza Mtu wa Uovu, yule ambaye ana uhakika kuwa ataangamizwa.[a] Huyo atasimama kinyume na kujiweka mwenyewe juu ya kila kitu ambacho watu wanaabudu au kudhani kuwa kinafaa kuabudiwa. Ataenda na kuingia ndani ya Hekalu[b] na kukikalia kiti cha enzi, akidai kuwa yeye ni Mungu.

Niliwaambia zaidi ya mara moja nilipokuwa huko kwamba mambo yote haya yangetokea. Je, mnakumbuka? Na mnafahamu kinachomzuia Mtu wa Uovu. Huyo hataruhusiwa kuonekana mpaka wakati sahihi utakapofika. Tayari nguvu ya uovu inatenda kazi ulimwenguni sasa. Lakini yupo mmoja anayeizuia nguvu hiyo. Na ataendelea kuizuia mpaka atakapoondolewa. Kisha huyo Mtu wa Uovu atatokea. Lakini Bwana Yesu atamuua kwa pumzi inayotoka katika kinywa chake. Bwana atakuja katika namna ambayo kila mtu atamwona, na huo utakuwa mwisho wa Mtu wa Uovu.

Kuja kwa Mtu wa Uovu itakuwa kazi ya Shetani. Atakuja na nguvu kuu, na atafanya aina zote za miujiza ya uongo, ishara, na maajabu. 10 Mtu wa Uovu atatumia kila aina ya uovu kuwatia ujinga wote walio njiani kuelekea kuangamia. Wamepotea kwa sababu walikataa kuupenda ujumbe wenye ukweli kuhusu Yesu na kuokolewa. 11 Hivyo Mungu atawaacha wadanganyike hata kuamini uongo.[c] 12 Wote watahukumiwa kwa sababu hawakuamini ujumbe wa kweli na kwa kuwa walifurahia kufanya maovu.

Mmechaguliwa kwa ajili ya Wokovu

13 Ndugu zangu, ninyi ni watu mnaopendwa na Bwana. Na imetupasa tumshukuru Mungu daima kwa sababu yenu. Hayo ndiyo tunayotakiwa kuyatenda, kwa sababu Mungu aliwaita kuwa miongoni mwa watu[d] wa kwanza kuokolewa. Mmeokolewa na Roho aliyewafanya muwe watu wa Mungu walio watakatifu kupitia kuiamini kweli. 14 Mungu aliwaita ninyi mpate wokovu. Aliwaita kwa kutumia Habari Njema tuliwahubiri. Mliitwa ili mshiriki katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. 15 Hivyo simameni imara na kuendelea kuamini mafundisho tuliyowapa tulipokuwa huko na kupitia barua yetu.

16-17 Tunaomba kwamba Bwana Yesu Kristo na Mungu Baba yetu awafariji na kuwaimairisha katika kila jambo jema mnalotenda na kusema. Mungu alitupenda na kutupa kupitia neema matumaini ya ajabu na faraja isiyo na mwisho.

Footnotes

  1. 2:3 ataangamizwa Au “Kusababisha uharibifu”. Kwa maana ya kawaida, “ni mwana wa uharibifu”.
  2. 2:4 Hekalu Pengine Hekalu katika Yerusalemu. Tazama Hekalu katika Orodha ya Maneno.
  3. 2:11 uongo Ina maana ya kuamini uongo (mkubwa) juu ya Muasi (ya kwamba Muasi ndiye Mungu).
  4. 2:13 kuwa … watu Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza, “kuanzia mwanzo”.