Add parallel Print Page Options

Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake 72

10 Baada ya hili, Bwana alichagua wafuasi sabini na wawili[a] zaidi. Aliwatuma watangulie katika kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda wakiwa wawili wawili. Aliwaambia, “Kuna mavuno mengi ya watu wa kuwaingiza katika Ufalme wa Mungu. Lakini watenda kazi wa kuwaingiza katika ufalme wa Mungu ni wachache. Mungu anamiliki mavuno. Mwombeni ili atume watenda kazi wengi ili wasaidie kuyaingiza mavuno yake.

Mnaweza kwenda sasa. Lakini sikilizeni! Ninawatuma na mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Msibebe mfuko wowote, wala pesa au viatu. Msisimame kusalimiana na watu njiani. Kabla ya kuingia katika nyumba, mseme, ‘Amani iwemo katika nyumba hii.’ Ikiwa watu wanaoishi katika nyumba hiyo wanapenda amani, baraka yenu ya amani itakaa nao. Lakini kama siyo, baraka yenu ya amani itawarudia. Kaeni katika nyumba inayopenda amani. Kuleni na kunywa chochote watakachowapa kwa maana mfanyakazi anastahili ujira. Msihame kutoka katika nyumba hiyo na kwenda kukaa katika nyumba nyingine.

Mkiingia katika mji wowote na watu wakawakaribisha, kuleni vyakula watakavyowapa. Waponyeni wagonjwa wanaoishi katika mji huo, na waambieni Ufalme wa Mungu umewafikia![b]

10 Lakini mkiingia katika mji wowote na watu wasiwakaribishe, nendeni katika mitaa ya mji huo na mseme, 11 ‘Tunafuta mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana katika miguu yetu! Lakini kumbukeni kwamba: Ufalme wa Mungu umewafikia!’ 12 Ninawaambia, siku ya hukumu itakuwa vibaya sana kwa watu wa mji huo kuliko watu wa Sodoma.

Maonyo Kwa Wanaomkataa Yesu

(Mt 11:20-24)

13 Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida![c] Watu wenu wameniona nikifanya miujiza mingi ndani yenu, lakini hamkubadilika. Miujiza hiyo hiyo ingefanyika katika miji ya Tiro na Sidoni,[d] watu katika miji hiyo wangelikwisha badili mioyo na maisha yao siku nyingi. Wangelikwisha vaa nguo za magunia na kukaa kwenye majivu kuonesha kusikitika na kutubu dhambi zao. 14 Lakini itakuwa rahisi kwa miji ya Tiro na Sidoni siku ya hukumu kuliko ninyi. 15 Nawe Kapernaumu, Je! Utatukuzwa mpaka mbinguni? Hapana, utatupwa chini hadi mahali pa kifo.

16 Mtu yeyote akiwasikiliza ninyi wafuasi wangu, hakika ananisikiliza mimi. Lakini mtu yeyote akiwakataa ninyi, hakika ananikataa mimi. Na mtu yeyote akinikataa mimi anamkataa Yule aliyenituma.”

Shetani Aangushwa

17 Wale wafuasi sabini na wawili waliporudi kutoka katika safari yao, walikuwa na furaha sana. Walisema, “Bwana, hata pepo walitutii tulipotumia jina lako!”

18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kama mwanga wa radi kutoka mbinguni! 19 Yeye ndiye adui, lakini tambueni kuwa nimewapa mamlaka zaidi yake. Nimewapa mamlaka ya kuponda nyoka na nge zake kwa miguu yenu. Hakuna kitakachowadhuru. 20 Ndiyo, hata pepo wanawatii. Na mnaweza kufurahi, lakini si kwa sababu mna mamlaka hii. Furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Yesu Aomba Kwa Baba

(Mt 11:25-27; 13:16-17)

21 Ndipo Yesu akajisikia furaha kwa uweza wa Roho Mtakatifu, akasema, “Ninakusifu wewe, Baba, BWANA wa mbingu na nchi. Ninashukuru kwamba umewaficha mambo haya wenye hekima na akili nyingi. Lakini umeyafunua kwa watu walio kama watoto wadogo. Ndiyo, Baba, umefanya hivi kwa sababu hakika ndivyo ulitaka kufanya.

22 Baba yangu amenipa vitu vyote. Hakuna anayejua Mwana ni nani, Baba peke yake ndiye anayejua. Na Mwana peke yake ndiye anayejua Baba ni nani. Watu pekee watakaojua kuhusu Baba ni wale ambao Mwana amechagua kuwaambia.”

23 Wafuasi walikuwa na Yesu peke yao na Yesu aliwageukia akasema, “Ni baraka kubwa kwenu kuyaona mnayoyaona sasa! 24 Ninawaambia, Manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mambo haya mnayoyaona ninyi, lakini hawakuyaona, na walitamani kuyasikia mnayoyasikia ninyi lakini hawakuweza.”

Simulizi Kuhusu Msamaria Mwema

25 Kisha mwanasheria mmoja alisimama ili amjaribu Yesu. Akasema, “Mwalimu, ninatakiwa nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

26 Yesu akamwambia, “Imeandikwa nini katika torati? Unaielewaje?”

27 Yule mwana sheria akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote.’(A) Pia ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’”(B)

28 Yesu akasema, “Jibu lako ni sahihi. Fanya hivi nawe utaupata uzima wa milele.”

29 Lakini mwanasheria alitaka kuonesha kuwa alikuwa mwenye haki na aliishi kwa usahihi. Hivyo akamwuliza Yesu, “Lakini si kila mtu aliye jirani yangu, au unasemaje?”

30 Katika kujibu swali hili, Yesu akasema, “Mtu mmoja alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Akiwa njiani alivamiwa na majambazi, wakamchania nguo na kumpiga. Kisha wakamwacha amelala chini akiwa katika hali ya kufa.

31 Ikatokea kuwa kuhani mmoja alikuwa anasafiri kupitia njia hiyo hiyo. Alipomwona, hakusimama ili amsaidie, alikwenda zake. 32 Kisha Mlawi[e] alipokaribia na kumwona yule mtu, alipita upande mwingine. Hakusimama ili amsaidie, Alikwenda zake.

33 Ndipo Msamaria[f] mmoja aliyekuwa anasafiri kupitia njia ile ile, alipofika mahali ambapo mtu aliyejeruhiwa alikuwa amelala, alipomwona alimhurumia. 34 Alimkaribia ili amsaidie, akamsafisha majeraha kwa mafuta ya zeituni na divai,[g] kisha akayafunga majeraha yake. Msamaria alikuwa na punda. Akampandisha juu ya punda wake na kumpeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni. Akamhudumia huko. 35 Siku iliyofuata, Msamaria alitoa sarafu mbili za fedha na kumpa mtunza nyumba ya wageni, akamwambia, ‘Mtunze mtu huyu aliyejeruhiwa. Ukitumia pesa nyingi zaidi kwa kumhudumia, nitakulipa nitakapokuja tena.’”

36 Kisha Yesu akasema, “Ni yupi kati ya hawa watu watatu unadhani hakika alikuwa jirani wa yule mtu aliyepigwa na majambazi?”

37 Mwanasheria akajibu, “Ni yule aliyemsaidia.”

Yesu akasema, “Basi nenda ukafanye kama alivyofanya.”

Maria na Martha

38 Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanasafiri, walifika katika kijiji kimoja. Mwanamke aitwaye Martha alimkaribisha nyumbani kwake. 39 Alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Mariamu. Mariamu alikuwa amekaa karibu na Yesu akimsikiliza anavyofundisha. 40 Lakini Martha dada yake Mariamu alikuwa anashughulisha na shughuli mbalimbali zilizotakiwa kufanywa. Martha aliingia ndani na akasema, “Bwana, hujali kuona mdogo wangu ameniacha nifanye kazi zote peke yangu? Mwambie aje kunisaidia.”

41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, unasumbuka na kuhangaika kwa shughuli nyingi. 42 Lakini kitu kimoja tu ndicho cha lazima. Mariamu amefanya uchaguzi sahihi na kamwe hautachukuliwa kutoka kwake.”

Footnotes

  1. 10:1 sabini na wawili Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza wafuasi sabini. Pia katika mstari wa 17.
  2. 10:9 umewafikia Au “unakuja kwenu haraka” au “umewafikia”.
  3. 10:13 Korazini, Bethsaida Miji ya Kiyahudi iliyokuwa kando kando mwa Ziwa Galilaya ambapo Yesu alifanya miujiza mingi kudhihirisha mamlaka yake yanayotoka kwa Mungu. Pamoja na hili, watu walikataa kubadili maisha waliyoishi yasiyokuwa na Mungu.
  4. 10:13 Tiro na Sidoni Miji iliyojaa ibada ya sanamu ambayo ilijulikana sana kwa uovu uliokuwemo humo.
  5. 10:32 Mlawi Yaani mtumishi wa Hekalu.
  6. 10:33 Msamaria Wayahudi waliwachukulia Wasamaria kama maadui. Tazama Msamaria katika Orodha ya Maneno.
  7. 10:34 mafuta ya zeituni na divai Vilitumika kama dawa kwa ajili ya kulainisha na kusafisha majeraha.