Add parallel Print Page Options

Badilisheni Namna Mnavyoishi

13 Sehemu ya watu waliokuwa pamoja na Yesu pale, walimweleza kilichowapata baadhi ya waabuduo kutoka Galilaya. Pilato alikuwa ameamuru wauawe. Damu zao zilichanganywa na damu za wanyama waliowaleta kwa ajili ya kutoa dhabihu. Yesu alijibu akasema, “Mnadhani hili liliwapata watu hao kwa sababu walikuwa wenye dhambi kuliko watu wengine wote wa Galilaya? Hapana, hawakuwa hivyo. Lakini ikiwa hamtaamua kubadili maisha yenu sasa, ninyi nyote mtaangamizwa kama wao! Na vipi kuhusu wale watu kumi na wanane waliokufa pale mnara wa Siloamu ulipowaangukia? Mnadhani walikuwa na dhambi kuliko watu wengine katika mji wa Yerusalemu? Hawakuwa hivyo. Lakini ninawaambia, ikiwa hamtaamua kubadilika sasa, hata ninyi mtaangamizwa pia!”

Mti Usiozaa Matunda

Yesu akawasimulia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa amepanda mtini katika shamba lake. Alipokuja kutafuta matunda kwenye mtini huo hakupata tunda lolote. Alikuwa na mtumishi aliyekuwa akilitunza shamba. Hivyo alimwambia mtumishi wake, ‘Nimekuwa nikitafuta matunda kwenye mti huu kwa miaka mitatu, lakini sijawahi kupata tunda lolote. Ukate mti huu! Kwa maana unaiharibu ardhi.’ Lakini mtumishi alijibu, ‘Mkuu, tuuache mti huu mwaka mmoja zaidi ili tuone ikiwa utazaa matunda. Nitakusanya samadi kuuzunguka ili kuupa mbolea. Unaweza kuzaa matunda mwaka ujao. Ikiwa hautazaa, ndipo utaweza kuukata.’”

Yesu Amponya Mwanamke Siku ya Sabato

10 Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi moja siku ya Sabato. 11 Alikuwepo mwanamke mmoja ndani ya sinagogi aliyekuwa na pepo mchafu aliyemlemaza kwa muda wa miaka kumi na nane. Mgongo wake ulikuwa umepinda na hakuweza kusimama akiwa amenyooka. 12 Yesu alipomwona alimwita na kumwambia, “Mama, umefunguliwa kutoka katika ugonjwa wako!” 13 Akaweka mikono yake juu yake na saa hiyo hiyo akaweza kusimama akiwa amenyooka. Akaanza kumsifu Mungu.

14 Kiongozi wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu aliponya siku ya Sabato. Akawaambia watu, “Kuna siku sita za kufanya kazi. Hivyo njooni ili mponywe katika moja ya siku hizo, msije siku ya Sabato kutafuta uponyaji.”

15 Yesu akamjibu kwa kusema, “Ninyi watu ni wanafiki! Ninyi nyote huwafungulia punda au ng'ombe wenu wa kulimia kutoka zizini na kuwapeleka kunywa maji kila siku, hata siku ya Sabato. 16 Mwanamke huyu niliyemponya ni mzaliwa halisi wa Ibrahimu.[a] Lakini Shetani alikuwa amemfunga kwa miaka kumi na nane. Hakika si kosa yeye kuponywa ugonjwa wake siku ya Sabato!” 17 Yesu aliposema haya, watu wote waliokuwa wanampinga walidhalilika. Kundi lote likafurahi kwa sababu ya mambo makuu aliyatenda.

Simulizi Nyingine ya Ufalme

(Mt 13:31-33; Mk 4:30-32)

18 Kisha Yesu akasema, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Niufananishe na nini? 19 Ufalme wa Mungu ni kama mbegu ya haradali. Mtu mmoja aliichukua na kuipanda katika bustani yake. Mbegu ikaota, ikakua na kuwa mti na ndege wakatengeneza viota kwenye matawi yake.”

20 Yesu akasema tena, “Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? 21 Ufalme wa Mungu unafanana na kiasi kidogo cha chachu ambacho mwanamke hutumia kuchanganya na kilo 20 za unga kutengeneza mkate. Hamira huumua kinyunya[b] chote.”

Mlango Mwembamba

(Mt 7:13-14,21-23)

22 Yesu alikuwa akifundisha katika kila mji na kijiji. Aliendelea kusafiri kuelekea Yerusalemu. 23 Mtu mmoja akamwuliza, “Bwana, watu wangapi wataokolewa? Ni wachache?”

Yesu akajibu, 24 “Mlango wa kuingia katika ufalme wa Mungu ni mwembamba. Jitahidini kuingia kupitia mlango huo. Watu wengi watataka kuingia huko, lakini hawataweza. 25 Mtu anapoufunga mlango wa nyumba yake, unaweza ukasimama nje na kubisha mlangoni, lakini hataufungua. Mnaweza kusema, ‘Mkuu tufungulie mlango!’ Lakini yeye akawajibu, ‘Siwajui ninyi na mnakotoka sikujui.’ 26 Ndipo mtaanza kusema, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe. Ulifundisha katika mitaa ya mji wetu.’ 27 Kisha atawaambia, ‘Siwajui na sijui mlikotoka! Ondokeni kwangu! Ninyi nyote ni watu mnaotenda maovu!’

28 Mtamwona Ibrahimu, Isaka, Yakobo na manabii wote wakiwa katika ufalme wa Mungu. Lakini ninyi wenyewe mtatupwa nje. Hapo mtalia na kusaga meno yenu kwa uchungu. 29 Watu watakuja kutoka mashariki, magharibi, kaskazini na kusini. Watakaa kuizunguka meza ya chakula katika ufalme wa Mungu. 30 Zingatieni kwamba wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”

Yesu Atakufa Yerusalemu

(Mt 23:37-39)

31 Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakaja kwa Yesu, na wakamwambia, “Ondoka hapa, nenda ukajifiche. Kwa sababu Herode anataka kukuua!”

32 Lakini Yesu akawaambia, “Nendeni, mkamwambie yule mbweha,[c] ‘Leo na kesho ninatoa pepo wachafu na kuponya watu, na kesho kazi itakwisha.’ 33 Baada ya hilo, ni lazima niende, kwa sababu manabii wote wanapaswa kufia Yerusalemu.

34 Yerusalemu! Yerusalemu! Uwauaye manabii. Unawapiga kwa mawe watu waliotumwa na Mungu kwako. Mara ngapi nimetaka kuwasaidia watu wako! Nilitaka kuwakusanya kama kuku anavyovikusanya vifaranga vyake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu. 35 Mungu atakuacha ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’”(A)

Footnotes

  1. 13:16 mzaliwa halisi wa Ibrahimu Kwa maana ya kawaida, “Binti wa Ibrahimu.”
  2. 13:21 kinyunya Mchanganyiko wa unga wa ngano na maji Ulio tayari kwa ajili ya kutengeneza mikate.
  3. 13:32 mbweha Yesu alimaanisha kuwa Herode ni mjanja na mwenye hila kama mbweha.