Add parallel Print Page Options

Je, ni Sahihi Kuponya Siku ya Sabato?

14 Siku moja ya Sabato Yesu alikwenda nyumbani kwa miongoni mwa viongozi wa Mafarisayo kula chakula pamoja naye. Watu wote mahali pale walikuwa wanamwangalia kwa makini kuona atafanya nini. Mbele yake kulikuwa na mtu aliyekuwa na ugonjwa mbaya.[a] Yesu akawauliza wanasheria na Mafarisayo, “Je, ni halali au kosa kuponya siku ya Sabato?” Lakini walishindwa kujibu swali lake. Hivyo akamshika yule mgonjwa, na kumponya, akamruhusu aende zake. Kisha akawaambia Mafarisayo na wanasheria, “Ikiwa mwanao au mnyama wako atatumbukia kisimani siku ya Sabato, mnatambua kuwa mtamtoa haraka.” Mafarisayo na wanasheria hawakuweza kujibu kinyume na alivyosema.

Usijifanye Mtu wa Muhimu

Ndipo Yesu akagundua kuwa baadhi ya wageni walikuwa wanachagua sehemu za heshima za kukaa mezani. Ndipo akawaambia, “Ukialikwa na mtu katika sherehe ya harusi, usikae katika sehemu za heshima. Wanaweza kuwa wamemwalika mtu muhimu kuliko wewe. Na kama umekaa katika kiti muhimu zaidi, watakuja kwako na kukuambia ‘toka ulipokaa umpishe huyu!’ Ndipo itakulazimu kuhamia sehemu zisizo za heshima na utaaibika.

10 Hivyo ukialikwa, nenda ukae mahali pasipo pa heshima, ili yule aliyekualika akija, akuambie, ‘Rafiki, njoo huku mbele zaidi mahali pazuri.’ Ndipo utaheshimiwa mbele ya wageni wote walio mezani pamoja nawe. 11 Kila ajikwezaye atashushwa. Lakini ajishushaye atakwezwa.”

Utazawadiwa

12 Kisha Yesu akamwambia Farisayo aliyemwalika, “Unapoandaa chakula, usiwaalike rafiki zako tu, au ndugu zako, au jamaa zako, wala jirani zako matajiri. Kwa sababu wao pia watakualika, na kwa kufanya hivyo watakuwa wanakulipa. 13 Lakini ufanyapo sherehe waalike maskini, waliolemaa, walemavu wa miguu, na wasiyeona. 14 Utabarikiwa, kwa sababu watu hawa hawana kitu cha kukulipa. Lakini Mungu atakupa thawabu wakati wa ufufuo wa wenye haki.”

Mfano Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Chakula

(Mt 22:1-10)

15 Basi mmoja wa watu waliokuwa mezani pamoja naye aliposikia hayo akamwambia Yesu, “Wamebarikiwa watakaokula karamu katika ufalme wa Mungu.”

16 Yesu akamwambia, “Mtu mmoja aliandaa sherehe kubwa, na kuwaalika watu wengi. 17 Wakati wa kuanza sherehe ulipofika, alimtuma mtumishi wake awaambie wale walioalikwa, ‘Tafadhalini njooni sasa. Kila kitu kiko tayari.’ 18 Lakini wageni waalikwa wote walisema kuwa hawawezi kuja. Kila mmoja alitoa udhuru. Wa kwanza alisema, ‘Nimenunua shamba, hivyo ni lazima niende nikalitazame. Tafadhali unisamehe.’ 19 Mwingine alisema, ‘Nimenunua ng'ombe wa kulimia jozi tano; ni lazima niende kuwajaribu. Tafadhali unisamehe.’ 20 Na mtu wa tatu alisema, ‘Nimeoa mke, kwa sababu hiyo siwezi kuja.’

21 Hivyo mtumishi alirudi na kumjulisha bwana kilichotokea. Bwana wake akakasirika, akamwambia mtumishi wake, ‘Fanya haraka! Nenda mitaani na katika vichochoro vya mji. Niletee maskini, vilema, wasiyeona na walemavu wa miguu!’

22 Baadaye mtumishi akamwambia, ‘Mkuu nimefanya kama ulivyoniagiza, lakini bado tuna nafasi kwa ajili ya watu wengine zaidi.’ 23 Hivyo bwana wake akamwambia mtumishi, ‘Toka nje uende kwenye barabara zinazoelekea vijijini na kando kando ya mashamba. Waambie watu huko waje, ninataka nyumba yangu ijae! 24 Ninakwambia, sitaki mtu hata mmoja kati ya wale niliowaalika kwanza atakayekula chakula hiki nilichoandaa.’”

Amua Ikiwa Unaweza Kunifuata

(Mt 10:37-38)

25 Watu wengi walikuwa wanasafiri pamoja na Yesu. Akawaambia, 26 “Ikiwa unakuja kwangu na hauko tayari kuiacha familia yako, huwezi kuwa mfuasi wangu. Ukimpenda zaidi baba yako, mama yako, mke wako, watoto wako, kaka na dada zako na hata maisha yako zaidi yangu huwezi kuwa mwanafunzi wangu. 27 Yeyote ambaye hatauchukua msalaba atakaopewa na akanifuata, hawezi kuwa mfuasi wangu.

28 Ikiwa unataka kujenga nyumba, kwanza utakaa na kuamua ili kujua itakugharimu kiasi gani. Ni lazima uone ikiwa una pesa za kutosha kumaliza kazi ya ujenzi. 29 Usipofanya hivyo, unaweza ukaanza kazi, lakini ukashindwa kumaliza kujenga nyumba. Na usipoweza kuimaliza, kila mtu atakucheka, 30 Watasema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini alishindwa kumalizia.’

31 Ikiwa mfalme anakwenda kupigana vita na mfalme mwingine, atakaa chini kwanza na kupanga. Ikiwa ana askari elfu kumi, ataamua ikiwa ana uwezo wa kumshinda mfalme mwenye askari elfu ishirini. 32 Akiona hawezi kumshinda mfalme mwingine, atatuma baadhi ya watu kwa mfalme mwingine ili wapatane akiwa bado yuko mbali.

33 Ndivyo ilivyo kwa kila mmoja wenu. Lazima uache kila kitu ulichonacho. La sivyo, huwezi kuwa mfuasi wangu.

Msipoteze Umuhimu Wenu

(Mt 5:13; Mk 9:50)

34 Chumvi ni kitu kizuri; lakini chumvi ikipoteza ladha yake, huwezi kuitengenezea ladha tena. 35 Haifai. Huwezi hata kuitumia kama uchafu au mbolea. Watu huitupa tu.

Mnaonisikiliza, sikilizeni!”

Footnotes

  1. 14:2 ugonjwa mbaya Yaani, “safura”, ugonjwa unaosababisha mwili kuvimba.