Add parallel Print Page Options

Furaha Mbinguni

(Mt 18:12-14)

15 Watoza ushuru na wenye dhambi wengi waliendelea kuja kumsikiliza Yesu. Hivyo Mafarisayo na walimu wa sheria wakaanza kulalamika wakisema, “Mtazameni mtu huyu[a] huwakaribisha wenye dhambi na hata kula pamoja nao!”

Hivyo Yesu akawaambia mfano huu, “Chukulia mmoja wenu ana kondoo mia, lakini mmoja akapotea. Utafanya nini? Utawaacha wale tisini na tisa na kwenda kumtafuta yule mmoja aliyepotea mpaka umpate. Na ukishampata, utafurahi sana. Utambeba mabegani mwako mpaka nyumbani. Kisha utakwenda kwa majirani na rafiki zako na utawaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimempata kondoo wangu aliyepotea!’ Katika namna hiyo hiyo ninawaambia, kunakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mtu anayeacha dhambi zake. Kuna furaha zaidi kwa ajili ya mtu mmoja anayeacha dhambi kuliko watu wema tisini na tisa ambao hudhani hawahitaji kubadilika.

Fikiria kuhusu mwanamke mwenye sarafu kumi za fedha,[b] lakini akapoteza sarafu moja kati ya hizo. Atawasha taa na kuifagia nyumba. Ataitafuta sarafu kwa bidii mpaka aione. Na akiiona, atawaita rafiki na jirani zake na kuwaaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata sarafu niliyoipoteza!’ 10 Katika namna hiyo hiyo, ni furaha kwa malaika wa Mungu, mwenye dhambi mmoja anapotubu.”

Simulizi Kuhusu Mwana Mpotevu

11 Kisha Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. 12 Mwana mdogo alimwambia baba yake, ‘Baba, nipe sehemu ya mali ninayotarajia kurithi baadaye.’ Hivyo baba yake akagawa utajiri wake kwa wanawe wawili.

13 Baada ya siku chache yule mdogo akauza mali zake, akachukua pesa zake na akaondoka. Akasafiri mbali katika nchi nyingine. Huko alipoteza pesa zake zote katika starehe na anasa. 14 Baada ya kutumia vyote alivyokuwa navyo, kukatokea njaa kali katika nchi ile yote. Akawa na njaa na mhitaji wa pesa. 15 Hivyo alikwenda kutafuta kazi kwa mwenyeji mmoja wa nchi ile, naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. 16 Alikuwa anasikia njaa kiasi kwamba alikuwa anatamani kula chakula walichokula nguruwe. Lakini hakuna mtu aliyempa chakula.

17 Alipotambua namna alivyokuwa mjinga, akafikiri moyoni mwake na kusema, ‘Wafanyakazi wote wa baba yangu wana chakula kingi. Lakini niko hapa kama niliyekufa kwa sababu sina chakula. 18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu. Nitamwambia hivi: Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe. 19 Sistahili kuitwa mwanao tena. Lakini niruhusu niwe kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ 20 Hivyo akaondoka na kurudi kwa baba yake.

Alipokuwa mbali na nyumbani kwao, baba yake alimwona, akamwonea huruma. Akamkimbilia, akamkumbatia na kumbusu sana. 21 Mwanaye akasema, ‘Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe; sistahili kuitwa mwanao tena.’

22 Lakini baba akawaambia watumishi wake, ‘Fanyeni haraka, leteni vazi maalumu, mvikeni. Pia, mvisheni viatu vizuri na pete kwenye kidole chake. 23 Na leteni ndama aliyenona, mchinjeni ili tule na kusherehekea. 24 Kwa sababu mwanangu alikuwa amekufa, lakini sasa yuko hai tena! Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kusherehekea.

25 Mwanaye mkubwa alikuwa shambani. Alipoikaribia nyumba, alisikia sauti za muziki na kucheza. 26 Akaita mmoja wa watumishi na akamwuliza, ‘Kuna nini?’ 27 Mtumishi akasema, ‘Mdogo wako amerudi, na baba yako amechinja ndama aliyenona. Anafurahi kwa sababu amempata mwanaye akiwa salama na mzima.’

28 Mwana mkubwa alikasirika na hakutaka kwenda kwenye sherehe. Hivyo baba yake akatoka nje kumsihi. 29 Lakini alimwambia baba yake, ‘Tazama, miaka yote hii nimekutumikia kama mtumishi, kamwe sijaacha kukutii! Lakini hujawahi kunipa hata mbuzi mdogo ili nisherehekee pamoja na rafiki zangu. 30 Lakini alipokuja huyu mwanao aliyepoteza mali zako kwa makahaba, umemchinjia ndama aliyenona!’

31 Baba yake akamwambia, ‘Mwanangu, daima umekuwa pamoja nami, na vyote nilivyo navyo ni vyako. 32 Lakini tulipaswa kusherehekea. Mdogo wako alikuwa amekufa, lakini sasa ni hai tena. Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’”

Footnotes

  1. 15:2 mtu huyu Yaani, Yesu. Adui zake walikuwa wanakwepa kutamka jina lake.
  2. 15:8 sarafu kumi za fedha Kila sarafu, Sarafu ya Kiyunani iliyoitwa drachma ilikuwa na thamani ya ujira au mshahara wa siku moja.