Add parallel Print Page Options

Utajiri Halisi

16 Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Alikuwepo mtu mmoja tajiri, aliyekuwa na msimamizi wa kuangalia biashara zake. Baadaye akagundua kuwa msimamizi wake alikuwa anapoteza pesa zake. Hivyo, akamwita, akamwambia, ‘Nimesikia mambo mabaya juu yako. Nipe taarifa namna ulivyosimamia pesa zangu. Huwezi kuendelea kuwa msimamizi wangu.’

Hivyo msimamizi akawaza moyoni mwaka, ‘Nitafanya nini? Bwana wangu ananiachisha kazi yangu ya usimamizi. Sina nguvu za kulima, kuomba omba naona aibu. Najua nitakalofanya! Nitafanya kitu nipate marafiki. Ili nitakapopoteza kazi yangu, watanikaribisha katika nyumba zao.’

Hivyo msimamizi akawaita mmoja mmoja wale waliokuwa wanadaiwa pesa na bwana wake. Akamwuliza wa kwanza, ‘Mkuu wangu anakudai kiasi gani?’ Akamjibu, ‘Ananidai mitungi[a] 100 ya mafuta ya zeituni.’ Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, kaa chini, fanya haraka, badilisha iwe mitungi hamsini.’

Kisha akamwambia mwingine, ‘Na wewe kiasi gani unadaiwa?’ Akajibu, ‘Vipimo[b] mia moja vya ngano.’ Akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, ibadilishe iwe vipimo themanini.’

Baadaye bwana wake akamsifu msimamizi asiye mwaminifu kwa sababu ya kutenda kwa busara. Ndiyo, watu wa ulimwengu huu wana busara katika kufanya biashara kati yao kuliko wana wa Mungu.

Ninamaanisha hivi: Vitumieni vitu vya kidunia mlivyonavyo sasa ili muwe na ‘marafiki’ kwa ajili ya siku za baadaye. Ili wakati vitu hivyo vitakapotoweka, mtakaribishwa katika nyumba ya milele. 10 Mtu yeyote anayeweza kuaminiwa kwa mambo madogo anaweza kuaminiwa kwa mambo makubwa pia. Mtu asiye mwaminifu katika jambo dogo hawezi kuwa mwaminifu katika jambo kubwa. 11 Ikiwa huwezi kuaminiwa kwa mali za kidunia, huwezi kuaminiwa kwa mali za mbinguni. 12 Na kama hauwezi kuaminiwa kwa vitu vya mtu mwingine, hautapewa vitu kwa ajili yako wewe mwenyewe.

13 Mtumwa hawezi kuwatumikia mabwana wawili wakati mmoja, hata ninyi hamwezi. Utamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au utakuwa mwaminifu kwa mmoja na hautamjali mwingine. Pia, huwezi kumtumikia Mungu na pesa.”[c]

Sheria Ya Mungu Haiwezi Kubadilishwa

(Mt 11:12-13)

14 Mafarisayo walikuwa wakiyasikiliza mambo haya yote. Walimdhihaki Yesu kwa sababu wote walipenda pesa. 15 Yesu aliwaambia, “Mnajifanya kuwa wenye haki mbele za watu, lakini Mungu anajua hakika kilichomo mioyoni mwenu. Jambo ambalo watu hudhani kuwa la muhimu, kwa Mungu ni chukizo.

16 Kabla ya Yohana Mbatizaji kuja, watu walifundishwa Sheria ya Musa na maandishi ya Manabii. Lakini tangu wakati wa Yohana, Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu inahubiriwa. Na kila mtu anajitahidi sana ili kuingia katika ufalme wa Mungu. 17 Ni rahisi sana kwa mbingu na dunia kutoweka, kuliko sehemu ndogo ya herufi katika Sheria ya Musa kutoweka. 18 Mwanaume yeyote anayemtaliki mkewe na kumwoa mke mwingine anazini. Na mwanaume anayeoa mwanamke aliyetalikiwa anazini pia.”

Tajiri na Lazaro

19 Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja, tajiri ambaye daima alivaa nguo za thamani sana, alikuwa tajiri sana kiasi kwamba alifurahia vitu vizuri kila siku. 20 Alikuwepo pia maskini mmoja aliyeitwa Lazaro ambaye mwili wake ulikuwa umejaa vidonda. Mara nyingi aliwekwa kwenye lango la tajiri. 21 Lazaro alitaka tu kula masalia ya vyakula vilivyokuwa sakafuni vilivyodondoka kutoka mezani kwa tajiri. Na mbwa walikuja na kulamba vidonda vyake.

22 Baadaye Lazaro alikufa. Malaika walimchukua na kumweka kifuani pa Ibrahimu. Tajiri naye alikufa na kuzikwa. 23 Alichukuliwa mpaka mahali pa mauti[d] na akawa katika maumivu makuu. Alimwona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro akiwa kifuani pake. 24 Akaita, ‘Baba Ibrahimu, nihurumie! Mtume Lazaro kwangu ili achovye ncha ya kidole chake kwenye maji na kuupoza ulimi wangu, kwa sababu ninateseka katika moto huu!’

25 Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwanangu, unakumbuka ulipokuwa unaishi? Ulikuwa na mambo yote mazuri katika maisha. Lakini Lazaro hakuwa na chochote ila matatizo. Sasa yeye anafarijiwa hapa, na wewe unateseka. 26 Pia kuna korongo pana na lenye kina kati yetu sisi na ninyi. Hakuna anayeweza kuvuka kuja kukusaidia na hakuna anayeweza kuja huku kutoka huko.’

27 Tajiri akasema, ‘Basi, nakuomba baba, mtume Lazaro nyumbani kwa baba yangu duniani, 28 Nina ndugu watano. Mtume ili akawape tahadhari wasije wakafika mahali hapa pa mateso.’

29 Lakini Ibrahimu akasema, ‘Wanayo Sheria ya Musa na maandishi ya manabii kwa ajili ya kuyasoma; wasikilize na kutii.’

30 Tajiri akasema, ‘Hapana Baba Ibrahimu! Lakini ikiwa mtu kutoka kwa wafu akiwaendea ndipo wataamua kutubu na kubadili maisha yao.’

31 Lakini Ibrahimu akamwambia, ‘Ikiwa ndugu zako hawatawasikiliza Musa na manabii, hawataweza kumsikiliza mtu yeyote kutoka kwa wafu.’”

Footnotes

  1. 16:6 mitungi Kiyunani batous, kutoka kwa Kiebrania bath, sawa na galoni 8 au lita 34.
  2. 16:7 Vipimo Kiyunani korous, kutoka kwa Kiebrania cor, kipimo sawa kama galoni 89 au lita 390.
  3. 16:13 pesa Au “mamona”, neno la Kiaramu linalomaanisha “utajiri”.
  4. 16:23 mahali pa mauti Kwa maana ya kawaida, “Kuzimu”.