Add parallel Print Page Options

Yesu Amponya Mtumishi wa Afisa wa Jeshi

(Mt 8:5-13; Yh 4:43-54)

Yesu alipomaliza kuwaambia watu mambo yote aliyotaka kuwaambia, alikwenda mjini Kapernaumu. Afisa wa jeshi katika mji wa Kapernaumu alikuwa na mtumishi aliyekuwa wa muhimu sana kwake. Mtumishi huyu alikuwa mgonjwa sana karibu ya kufa. Afisa huyu aliposikia kuhusu Yesu, aliwatuma baadhi ya viongozi wa wazee wa Kiyahudi kwa Yesu. Aliwataka wamwombe Yesu aende kumponya mtumishi wake. Wazee walikwenda kwa Yesu, wakamsihi amsaidie afisa. Walisema, “Mtu huyu anastahili msaada wako, Kwa sababu anawapenda watu wetu na ametujengea sinagogi.”

Hivyo Yesu alikwenda nao. Alipoikaribia nyumba ya yule afisa, afisa aliwatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, huhitaji kufanya kitu chochote maalumu kwa ajili yangu. Sistahili wewe uingie nyumbani mwangu. Ndiyo maana sikuja mimi mwenyewe kwako. Unahitaji kutoa amri tu na mtumishi wangu atapona. Ninajua hii, kwa kuwa ninaelewa mamlaka. Kuna watu wenye mamlaka juu yangu, na nina askari walio chini ya mamlaka yangu. Nikimwambia askari mmoja ‘nenda’, huenda. Na nikimwambia mwingine ‘njoo’, huja. Pia nikimwambia mtumwa wangu ‘fanya hiki’, hunitii.”

Yesu aliposikia hayo alishangaa, akawageukia watu waliokuwa wanamfuata, akawaambia, “Ninawaambia, Sijawahi kuona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.”

10 Kundi lililotumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani, walimkuta yule mtumishi amepona.

Yesu Amfufua Kijana wa Mama Mjane

11 Siku iliyofuata Yesu na wafuasi wake walikwenda katika mji wa Naini. Kundi kubwa la watu walisafiri pamoja nao. 12 Yesu alipolikaribia lango la mji, aliona watu wamebeba maiti. Alikuwa ni mwana pekee wa mama mjane. Watu wengi kutoka mjini walifuatana na yule mama mjane. 13 Bwana alipomwona yule mama, alimwonea huruma na kumwambia, “Usilie.” 14 Akakaribia, akaligusa jeneza. Wanaume waliokuwa wamebeba jeneza wakasimama. Ndipo Yesu akamwambia kijana aliyekufa, “Kijana, nakuambia, inuka!” 15 Yule kijana, akaketi, akaanza kuongea. Yesu akamrudisha kwa mama yake.

16 Kila mtu aliingiwa hofu. Wakaanza kumsifu Mungu na kusema, “Nabii mkuu yuko hapa pamoja nasi!” na “Mungu amekuja kuwasaidia watu wake!”

17 Habari hii kuhusu Yesu ikaenea katika Uyahudi yote, na kila sehemu kuzunguka pale.

Yohana Atuma Watu Kumwuliza Yesu Swali

(Mt 11:2-19)

18 Wafuasi wa Yohana Mbatizaji walimweleza Yohana Mbatizaji kuhusu mambo haya yote. Naye aliwaita wanafunzi wake wawili. 19 Akawatuma waende na kumwuliza Yesu, “Wewe ndiye tuliyesikia anakuja, au tumsubiri mwingine?”

20 Wafuasi wa Yohana walipofika kwa Yesu, wakasema, “Yohana Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: ‘Wewe ndiye yule ajaye, au tumsubiri mwingine?’”

21 Wakati ule ule Yesu alikuwa amewaponya watu wengi madhaifu na magonjwa yao. Aliwaponya waliokuwa na pepo wabaya na kuwafanya wasiyeona wengi kuona. 22 Kisha aliwaambia wanafunzi wa Yohana, “Nendeni mkamweleze Yohana yale mliyoyaona na kuyasikia: wasiyeona wanaona, walemavu wa miguu wanatembea, wenye magonjwa mabaya ya ngozi wanatakasika, wasiyesikia wanasikia. Waliokufa wanafufuliwa na Habari Njema inahubiriwa kwa maskini. 23 Heri wale wasio na mashaka kunikubali mimi.”[a]

24 Baada ya wanafunzi wa Yohana kuondoka, Yesu akaanza kuwaambia watu kuhusu Yohana, “Mlitoka kwenda jangwani kuona nini? Mtu aliyekuwa dhaifu, kama unyasi unaotikiswa na upepo? 25 Mlitegemea kuona nini? Mtu aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hilo. Watu wanaovaa mavazi mazuri na kuishi kwa anasa wako katika majumba ya wafalme. 26 Sasa, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yohana ni zaidi ya nabii. 27 Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana:

‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
    Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’(A)

28 Ninawaambia, hakuna aliyewahi kuzaliwa aliye mkuu kuliko Yohana. Lakini mwenye umuhimu mdogo, katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana.”

29 (Watu waliposikia hili, wote walikubali kuwa mafundisho ya Mungu yalikuwa mazuri. Hata watoza ushuru waliobatizwa na Yohana walikiri. 30 Lakini Mafarisayo na wanasheria walikataa kuukubali mpango wa Mungu kwa ajili yao; hawakumruhusu Yohana awabatize.)

31 “Niseme nini kuhusu watu wa wakati huu? Niwafananishe na nini? Wanafanana na nini? 32 Ni kama watoto waliokaa sokoni. Kundi moja la watoto likawaita watoto wengine na kusema,

‘Tuliwapigia filimbi
    lakini hamkucheza.
Tuliwaimba wimbo wa huzuni,
    lakini hamkulia.’

33 Yohana Mbatizaji alikuja na hakula chakula cha kawaida au kunywa divai. Nanyi mkasema, ‘Ana pepo ndani yake.’ 34 Mwana wa Adamu amekuja anakula na kunywa. Mnasema, ‘Mwangalieni anakula sana na kunywa sana divai. Ni rafiki wa watoza ushuru na watenda dhambi wengine.’ 35 Lakini hekima huoneshwa kuwa sahihi kwa wale wanaoikubali.”

Yesu na Mwanamke Mwenye Dhambi

36 Mmoja wa Mafarisayo alimwalika Yesu kula chakula nyumbani mwake. Yesu akaenda nyumbani kwa yule Farisayo, akaketi[b] katika nafasi yake sehemu ya kulia chakula.

37 Alikuwepo mwanamke mmoja katika mjini ule aliyekuwa na dhambi nyingi. Alipojua kuwa Yesu alikuwa anakula chakula nyumbani kwa Farisayo, alichukua chupa kubwa yenye manukato ya thamani sana. 38 Alisimama karibu na miguu ya Yesu akilia. Kisha alianza kuisafisha miguu ya Yesu kwa machozi yake na akaifuta kwa nywele zake, akaibusu mara nyingi na kuipaka manukato.

39 Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona hili, alijisemea moyoni mwake, “Mtu huyu angekuwa nabii, angetambua kuwa mwanamke huyu anayemgusa ni mwenye dhambi.”

40 Katika kujibu kile Farisayo alichokuwa akifikiri, Yesu akasema, “Simoni nina kitu cha kukwambia.”

Simoni akajibu, “Nieleze, Mwalimu.”

41 Yesu akasema, “Kulikuwa watu wawili. Wote wawili walikuwa wanadaiwa na mkopeshaji mmoja. Mmoja alidaiwa sarafu mia tano za fedha, na wa pili sarafu hamsini za fedha. 42 Watu wale hawakuwa na fedha, hivyo hawakuweza kulipa madeni yao. Lakini mkopeshaji aliwasamehe wote wawili. Kati ya wote wawili ni yupi atakayempenda mkopeshaji zaidi?”

43 Simoni akajibu, “Nafikiri ni yule aliyekuwa anadaiwa fedha nyingi.”

Yesu akamwambia, “Umejibu sawa.” 44 Kisha akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, “Unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako hukunipa maji ili ninawe miguu yangu. Lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kuikausha kwa nywele zake. 45 Wewe hukunisalimu kwa busu, lakini amekuwa akinibusu miguu yangu tangu nilipoingia. 46 Hukuniheshimu kwa mafuta kwa ajili ya kichwa changu, lakini yeye amenipaka miguu yangu manukato yanayonukia vizuri. 47 Ninakwambia kuwa dhambi zake zilizo nyingi zimesamehewa. Hii ni wazi, kwa sababu ameonesha upendo mkubwa. Watu wanaosamehewa kidogo hupenda kidogo.”

48 Kisha akamwambia mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”

49 Watu waliokaa naye sehemu ya chakula wakaanza kusema mioyoni mwao, “Mtu huyu anadhani yeye ni nani? Anawezaje kusamehe dhambi?”

50 Yesu akamwambia mwanamke, “Kwa sababu uliamini, umeokolewa kutoka katika dhambi zako. Nenda kwa amani.”

Footnotes

  1. 7:23 Heri … kunikubali mimi Au “Baraka kuu ni kwa wale wasio na mashaka kunikubali.”
  2. 7:36 akaketi Waliketi kwa kujilaza kidogo kuelekea katika meza ya chakula katika mzunguko, miguu yao ikiwa imenyooka kwa nyuma.