Add parallel Print Page Options

Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake

(Mt 10:5-15; Mk 6:7-13)

Yesu aliwaita mitume wake kumi na wawili pamoja, akawapa nguvu kuponya magonjwa na kutoa pepo kwa watu. Akawatuma kwenda kuhubiri kuhusu Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. Akawaambia, “Mnaposafiri, msibebe kitu chochote: msichukue fimbo ya kutembelea, msibebe mkoba, chakula au fedha. Chukueni nguo mlizovaa tu kwa ajili ya safari yenu. Mkiingia katika nyumba; kaeni katika nyumba hiyo mpaka mtakapokuwa mnatoka katika mji huo. Ikiwa watu katika mji mtakaoingia hawatawakaribisha, nendeni nje ya mji na kuyakung'uta mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.”

Hivyo mitume wakaondoka. Walisafiri katika miji yote. Walihubiri Habari Njema na kuponya wagonjwa kila mahali.

Herode Achanganyikiwa Kuhusu Yesu

(Mt 14:1-12; Mk 6:14-29)

Herode, mtawala wa Galilaya alisikia mambo yote yaliyokuwa yanatokea. Alichanganyikiwa kwa sababu baadhi ya watu walisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka kwa wafu.” Wengine walisema, “Eliya amekuja kwetu,” na baadhi ya watu wengine walisema “Mmoja wa manabii wa kale amefufuka kutoka kwa wafu”. Herode alisema, “Nilimkata kichwa Yohana. Sasa, mtu huyu ninayesikia habari zake ni nani?” Herode aliendelea kutaka kumwona Yesu.

Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000

(Mt 14:13-21; Mk 6:30-44; Yh 6:1-14)

10 Mitume waliporudi, walimwambia Yesu waliyoyafanya katika safari yao. Ndipo akawachukua mpaka kwenye mji uitwao Bethsaida. Ili yeye Yesu na mitume wawe peke yao pamoja. 11 Lakini watu walipotambua mahali alikokwenda Yesu walimfuata. Aliwakaribisha na kuwaambia kuhusu ufalme wa Mungu. Na aliwaponya waliokuwa wagonjwa.

12 Baadaye nyakati za jioni. Mitume kumi na mbili walimwendea na kumwambia, “Hakuna anayeishi mahali hapa. Waage watu. Wanahitaji kutafuta chakula na mahali pa kulala katika mashamba na miji iliyo karibu na eneo hili.”

13 Lakini Yesu akawaambia mitume, “Wapeni chakula.”

Wakasema, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu. Unataka twende tukanunue vyakula kwa ajili ya watu wote hawa? Ni wengi mno!” 14 (Walikuwepo wanaume kama 5,000 pale.)

Yesu akawaambia wafuasi wake, “Waambieni watu wakae katika vikundi vya watu hamsini hamsini.”

15 Hivyo wafuasi wake wakafanya hivyo na kila mtu akakaa chini. 16 Ndipo Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili. Akatazama juu mbinguni na kumshukuru Mungu kwa ajili ya chakula hicho. Kisha akaimega vipande vipande, akawapa wanafunzi wake ili wawape watu. 17 Watu wote wakala mpaka wakashiba. Vikasalia vikapu kumi na mbili vilivyojaa vipande vya mikate na samaki ambavyo havikuliwa.

Petro Atambua Yesu ni Nani

(Mt 16:13-19; Mk 8:27-29)

18 Wakati mmoja Yesu alikuwa anaomba akiwa peke yake. Wafuasi wake walimwendea na aliwauliza, “Watu wanasema mimi ni nani?”

19 Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine wanasema wewe ni Eliya, lakini wengine wanasema wewe ni mmoja wa manabii wa zamani aliyefufuka.”

20 Kisha Yesu akawauliza wafuasi wake, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?”

Petro akajibu, “Wewe ni Masihi kutoka kwa Mungu.”

21 Yesu akawatahadharisha wasimwambie mtu yeyote.

Yesu Asema ni Lazima Afe

(Mt 16:21-28; Mk 8:31-9:1)

22 Yesu akasema, “Ni lazima Mwana wa Adamu apate mateso mengi. Nitakataliwa na viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Na nitauawa. Lakini siku ya tatu nitafufuliwa kutoka kwa wafu.”

23 Kisha Yesu akamwambia kila mmoja aliyekuwa pale, “Mtu yeyote miongoni mwenu akitaka kuwa mfuasi wangu ni lazima ajikane yeye mwenyewe na mambo anayopenda. Ni lazima uubebe msalaba unaotolewa kwako kila siku kwa sababu ya kunifuata mimi. 24 Yeyote miongoni mwenu anayetaka kuyaponya maisha yake atayaangamiza. Lakini yeyote atakayeyatoa maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa. 25 Haina thamani kwenu kuupata ulimwengu wote ikiwa ninyi wenyewe mtateketezwa au kupoteza kila kitu. 26 Msione aibu kwa sababu ya kunifuata na kusikiliza mafundisho yangu. Mkifanya hivyo, Mimi, Mwana wa Adamu, nitawaonea aibu nitakapokuja nikiwa na utukufu wangu, utukufu wa Baba na wa malaika watakatifu. 27 Niaminini ninaposema kwamba baadhi yenu ninyi mliosimama hapa mtauona Ufalme wa Mungu kabla hamjafa.”

Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya

(Mt 17:1-8; Mk 9:2-8)

28 Baada ya siku kama nane tangu Yesu aseme maneno haya, aliwachukua Petro, Yohana na Yakobo, akapanda mlimani kuomba. 29 Yesu alipokuwa akiomba, uso wake ulianza kubadilika. Nguo zake zikawa nyeupe, zikang'aa. 30 Kisha watu wawili walikuwa pale, wakiongea naye. Walikuwa Musa na Eliya; 31 Wao pia walionekana waking'aa na wenye utukufu. Walikuwa wanazungumza na Yesu kuhusu kifo chake kitakachotokea Yerusalemu. 32 Petro na wenzake walikuwa wanasinzia. Lakini waliamka na kuuona utukufu wa Yesu. Waliwaona pia watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. 33 Musa na Eliya walipokuwa wanaondoka, Petro akasema, “Mkuu, ni vizuri tuko hapa. Tutajenga vibanda vitatu hapa, kimoja kwa ajili ya kukutukuza wewe, kingine kwa ajili kumtukuza Musa na kingine wa ajili ya kumtukuza Eliya.” Petro hakujua alichokuwa anasema.

34 Petro alipokuwa akisema mambo haya, wingu likaja, likawafunika wote. Petro, Yohana na Yakobo waliogopa walipofunikwa na wingu. 35 Sauti ikatoka katika wingu na kusema, “Huyu ni Mwanangu. Ndiye niliyemchagua. Mtiini yeye.”

36 Sauti hiyo ilipomalizika, Yesu peke yake ndiye alikuwa pale. Petro, Yohana na Yakobo hawakusema chochote. Na kwa muda mrefu baada ya hilo, hawakumwambia mtu yeyote yale waliyoyaona.

Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu

(Mt 17:14-18; Mk 9:14-27)

37 Siku iliyofuata, Yesu, Petro, Yohana na Yakobo walitelemka kutoka mlimani. Kundi kubwa la watu likaenda kukutana naye. 38 Mtu mmoja katika umati huo alimwita Yesu akisema, “Mwalimu, tafadhali njoo umwonee mwanangu. Ni mtoto pekee niliye naye. 39 Pepo mchafu humvaa na hupiga kelele, humtia kifafa na kumtoa povu mdomoni. Huendelea kumwumiza na hamwachi kirahisi. 40 Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe pepo huyu mchafu lakini wameshindwa.”

41 Yesu akajibu, “Enyi watu msio na imani. Maisha yenu ni mabaya. Nitakaa na kuchukuliana nanyi mpaka lini?” Ndipo Yesu akamwambia yule mtu, “Mlete kijana wako hapa.”

42 Kijana alipokuwa anakwenda kwa Yesu, pepo mchafu akamwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamwamuru atoke. Kijana akaponywa, na Yesu akampeleka kwa baba yake. 43 Watu wote wakaushangaa ukuu wa nguvu ya Mungu.

Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake

(Mt 17:22-23; Mk 9:30-32)

Watu walipokuwa bado wanayashangaa mambo yote aliyofanya Yesu. Akawaambia wanafunzi wake, 44 “Msiyasahau nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu yu karibu kukamatwa na kuwekwa katika mikono ya watu wengine.” 45 Lakini wanafunzi hawakuelewa alichomaanisha. Maana ilifichwa kwao ili wasitambue. Lakini waliogopa kumwuliza Yesu kuhusiana na alilosema.

Nani ni Mkuu Zaidi?

(Mt 18:1-5; Mk 9:33-37)

46 Wafuasi wa Yesu walianza kubishana wakiulizana nani ni mkuu kuliko wote miongoni mwao. 47 Yesu alijua walichokuwa wanafikiri, hivyo akamchukua mtoto mdogo na kumsimamisha karibu yake. 48 Kisha akawaambia, “Yeyote anayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu kwa jina langu ananikaribisha mimi. Na yeyote anayenikaribisha mimi anamkaribisha yule aliyenituma. Aliye mnyenyekevu zaidi miongoni mwenu, ndiye mkuu.”

Asiye Kinyume Nanyi ni Mmoja Wenu

(Mk 9:38-40)

49 Yohana akajibu; “Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kutoka kwa watu akitumia jina lako. Tulimwambia aache kwa sababu hayuko katika kundi letu.”

50 Yesu akamwambia, “Msimkataze. Asiye kinyume nanyi yu pamoja nanyi.”

Katika Mji wa Samaria

51 Wakati ulikuwa unakaribia ambapo Yesu alikuwa aondoke na kurudi mbinguni. Hivyo aliamua kwenda Yerusalemu. 52 Alituma baadhi ya watu kumtangulia. Waliondoka na kwenda katika mji mmoja wa Samaria, ili kumwandalia mahali pa kufikia. 53 Lakini watu katika mji huo hawakumkaribisha Yesu kwa sababu alikuwa anakwenda Yerusalemu. 54 Wafuasi wake; Yakobo na Yohana walipoona hayo, wakasema, “Bwana, unataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni na kuwateketeza watu hawa?”[a]

55 Lakini Yesu aligeuka na akawakemea baada ya wao kusema hivi.[b] 56 Kisha Yesu na wanafunzi wake wakaondoka wakaenda katika mji mwingine.

Kumfuata Yesu

(Mt 8:19-22)

57 Walipokuwa wakisafiri pamoja njiani, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata kokote utakakokwenda.”

58 Yesu akamwambia, “Mbweha wana mapango na ndege wa angani wana viota. Lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”

59 Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate!”

Lakini mtu yule akamwambia, “Bwana, niache nikamzike baba yangu kwanza.”

60 Lakini Yesu akamwambia, “Waache waliokufa wawazike wafu wao. Ni lazima uende kuhubiri kuhusu Ufalme wa Mungu.”

61 Mtu mwingine pia akamwambia, “Nitakufuata Bwana, lakini niruhusu kwanza nikaiage familia yangu.”

62 Yesu akamwambia, “Mtu yeyote anayeanza kulima, kisha akaangalia nyuma hajajiandaa kwa ajili ya Ufalme wa Mungu.”

Footnotes

  1. 9:54 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza “Kama Eliya alivyofanya?”
  2. 9:55 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza “Na akasema, ‘Hamjui mna roho ya namna gani. 56 Mwana wa Adamu hakuja kuyateketeza maisha ya watu bali kuyaokoa.’”