Add parallel Print Page Options

Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini

(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 20:45-47)

37 Baada ya Yesu kumaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika Yesu kula pamoja naye. Hivyo Yesu alikwenda na kuketi sehemu ya kulia chakula. 38 Lakini Farisayo alishangaa alipoona Yesu hakunawa[a] mikono yake kwanza kabla ya kuanza kula. 39 Bwana akamwambia, “Usafi mnaoufanya ninyi Mafarisayo ni kama kusafisha kikombe au sahani kwa nje tu. Lakini ndani yenu mna nini? Mnataka kuwadanganya na kuwaumiza watu tu. 40 Ninyi ni wajinga! Aliyeumba kilicho nje ndiye aliumba kilicho ndani. 41 Hivyo, jalini vilivyo ndani. Wapeni vitu wenye uhitaji. Ndipo mtakuwa wasafi kikamilifu.

42 Lakini, ole wenu ninyi Mafarisayo! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya vyakula mnavyopata, hata mnanaa, na hata kila mmea mdogo katika bustani[b] zenu. Lakini mnapuuzia kuwatendea haki wengine na kumpenda Mungu. Haya ni mambo mnayotakiwa kufanya. Na endeleeni kufanya mambo hayo mengine.

43 Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kupata viti vya heshima katika masinagogi. Na mnapenda kusalimiwa na watu kwa kuheshimiwa sehemu za masoko. 44 Ole wenu, kwa kuwa mnafanana na makaburi ya zamani yasiyoonekana, ambayo watu hupita juu yake na kuyakanyaga bila kuyatambua.”

45 Mmoja wa wanasheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, unaposema mambo haya kuhusu Mafarisayo unatukosoa hata sisi pia.”

46 Yesu akamjibu, “Ole wenu, enyi wanasheria! Mnatunga sheria kali ambazo ni vigumu watu kuzitii.[c] Mnawalazimisha wengine kuzitii sheria zenu. Lakini ninyi wenyewe hamthubutu hata kujaribu kufuata mojawapo ya sheria hizo. 47 Ole wenu kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii. Lakini hawa ni manabii wale wale ambao mababu zenu waliwaua. 48 Na sasa mnawaonesha watu wote kwamba mnakubaliana na mambo ambayo baba zenu walifanya. Waliwaua manabii, nanyi mnasherehekea mauaji hayo kwa kujenga makaburi ya manabii! 49 Hii ndiyo sababu ambayo kwa Hekima yake Mungu alisema, ‘Nitawatuma manabii na mitume[d] kwao. Baadhi ya manabii na mitume wangu watauawa na watu waovu. Wengine watateswa sana.’

50 Hivyo ninyi watu mnaoishi sasa mtaadhibiwa kwa sababu ya vifo vya manabii wote waliouawa tangu mwanzo wa ulimwengu. 51 Mtachukuliwa wenye hatia kutokana na vifo hivyo vyote, tangu kuuawa kwa Habili mpaka kuuawa kwa nabii Zakaria,[e] aliyeuawa kati ya madhabahu na Hekalu. Ndiyo ninawaambia, kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu yao wote.

52 Ole wenu, ninyi wanasheria, mmechukua ufunguo wa kujifunza kuhusu Mungu. Ninyi wenyewe hamtaki kujifunza na mmewazuia wengine wasijifunze pia.”

53 Yesu alipotoka humo, walimu wa sheria na Mafarisayo walianza kumpinga sana. Walianza kumjaribu ili awajibu maswali kuhusu mambo mengi, 54 ili Yesu akisema jambo isivyo sahihi waweze kupata sababu ya kumkosoa.

Read full chapter

Footnotes

  1. 11:38 hakunawa Hakunawa kwa maana ya kuwa kunawa mikono au kuoga mwili wote ilikuwa desturi ya dini ya Kiyahudi na Mafarisayo waliipa desturi hii umuhimu mkubwa.
  2. 11:42 Mnampa … bustani Kwa maana ya kawaida, “Mnatoa zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga mboga.” Sheria ya Musa iliwataka Waisraeli kushirikiana chakula kwa kutenga sehemu ya kumi ya mazao na mifugo yao kwa ajili ya Mungu (tazama Law 27:30-32; Kum 26:12). Hii haikujumuisha mazao madogo ya bustani kama yaliyotajwa hapa. Hivyo Mafarisayo hawa walikuwa wanatoa zaidi ya inavyotakiwa ili kuhakikisha kuwa hawavunji sheria.
  3. 11:46 Mnatunga sheria kali … watu kuzitii Kwa maana ya kawaida, “Mnawatwisha watu mizigo wasiyoweza kuibeba.”
  4. 11:49 manabii na mitume Watu waliochaguliwa na Mungu kuhubiri Habari Njema ulimwenguni.
  5. 11:51 Habili … Zakaria Katika Agano la Kale la Kiebrania, hawa ni watu wa kwanza na wa mwisho kuuawa. Tazama Mwa 4:8-11 na 2 Nya 24:20-25.