Add parallel Print Page Options

Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu

(Mt 3:1-12; Lk 3:1-9,15-17; Yh 1:19-28)

Mwanzo wa Habari Njema za Yesu Masihi,[a] Mwana wa Mungu,[b] zilianza kama vile Nabii Isaya alivyosema zitaanza, aliandika,

“Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
    Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.”(A)
“Kuna mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
    nyoosheni njia kwa ajili yake.’”(B)

Naye Yohana akaja, akiwabatiza watu huko nyikani huku akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. Watu kutoka Yerusalemu na maeneo yote ya Uyahudi walikwenda kwa Yohana Mbatizaji; huko waliungama matendo yao mabaya kwake naye akawabatiza katika Mto Yordani.

Huyo Yohana alivaa mavazi yaliyofumwa kutokana na manyoya ya ngamia. Naye alijifunga mkanda wa ngozi kuzunguka kiuno chake, na alikula nzige na asali mbichi.

Yeye alitangaza yafuatayo: “Yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake.[c] Mimi nawabatiza katika maji, lakini yeye huyo atawabatiza katika Roho Mtakatifu.”

Yohana Ambatiza Yesu

(Mt 3:13-17; Lk 3:21-22)

Ikatokea katika siku hizo Yesu alikuja toka Nazareti uliokuwa mji wa Galilaya akabatizwa na Yohana katika mto Yordani. 10 Mara tu aliposimama kutoka ndani ya maji, Yesu aliona mpasuko ukitokea angani, akamwona Roho akishuka chini kuja kwake kama njiwa. 11 Sauti ikasikika toka mbinguni, “Wewe ni mwanangu, ninayekupenda, napendezwa nawe sana.”

Yesu Ajaribiwa na Shetani

(Mt 4:1-11; Lk 4:1-13)

12 Kisha baada ya kutokea mambo haya Roho Mtakatifu alimchukua Yesu na kumpeleka nyikani,[d] 13 naye akawa huko kwa siku arobaini, ambapo alijaribiwa na Shetani. Yesu alikuwa nyikani pamoja na wanyama wa porini, na malaika walimhudumia.

Yesu Aanza Kazi yake Galilaya

(Mt 4:12-17; Lk 4:14-15)

14 Baada ya Yohana kuwekwa gerezani, Yesu akaja katika wilaya karibu na Ziwa Galilaya, huko aliwatangazia watu Habari Njema kutoka kwa Mungu. 15 Akasema, “Wakati umefika. Ufalme wa Mungu umewafikia.[e] Mbadili mioyo yenu na maisha yenu, na kuiamini habari njema!”

Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi

(Mt 4:18-22; Lk 5:1-11)

16 Alipokuwa akitembea kando kando ya Ziwa Galilaya, Yesu alimwona Simoni[f] na Andrea ndugu yake. Hao walikuwa wavuvi na walikuwa wakizitupa nyavu zao ziwani kukamata samaki. 17 Yesu akawaambia, “njooni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa aina nyingine, nitawafundisha jinsi ya kukusanya watu badala ya samaki.” 18 Mara moja, Simoni na Andrea wakaziacha nyavu zao na kumfuata.

19 Kisha Yesu akaendelea mbele kidogo na akawaona ndugu wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na kaka yake Yohana. Yesu aliwaona wakiwa kwenye mashua wakiandaa nyavu zao za kuvulia samaki. 20 Naye akawaita mara moja. Hivyo wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua na watu waliowaajiri na kumfuata Yesu.

Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Mchafu

(Lk 4:31-37)

21 Kisha Yesu na wafuasi wake waliingia Kapernaumu. Siku ya Sabato Yesu aliingia katika sinagogi na akaanza kuwafundisha watu. 22 Walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka.[g] 23 Ndani ya sinagogi alikuwemo mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Naye mara alipiga kelele na kusema, 24 “Unataka nini kwetu, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.”

25 Lakini Yesu akamkemea na kumwambia, “Nyamaza kimya, na kisha umtoke ndani yake.” 26 Ndipo roho yule mchafu akamfanya mtu yule atetemeke. Kisha akatoa sauti kubwa na kisha akamtoka.

27 Kila mmoja akashangazwa sana kiasi cha kuwafanya waulizane, “Hii ni nini? Ni mafundisho ya aina mpya, na mtu yule anafundisha kwa mamlaka! Yeye huwapa amri pepo wachafu nao wanamtii!” 28 Hivyo habari kuhusu Yesu zikaenea haraka katika eneo lote la Galilaya.

Yesu Awaponya Watu Wengi

(Mt 8:14-17; Lk 4:38-41)

29 Wakaondoka kutoka katika sinagogi na mara hiyo hiyo wakaenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30 Mara Yesu alipoingia ndani ya nyumba watu wakamweleza kuwa mama mkwe wake Simoni alikuwa mgonjwa sana na alikuwa amepumzika kitandani kwa sababu alikuwa na homa. 31 Yesu akasogea karibu na kitanda, akamshika mkono na kumsaidia kusimama juu. Ile homa ikamwacha, na yeye akaanza kuwahudumia.

32 Ilipofika jioni, baada ya jua kuzama waliwaleta kwake watu wote waliokuwa wagonjwa na waliokaliwa na mashetani. 33 Mji mzima ulikusanyika mlangoni pale. 34 Naye akawaponya watu waliokuwa na magonjwa ya kila aina, na kufukuza mashetani wengi. Lakini yeye hakuyaruhusu mashetani kusema, kwa sababu yalimjua.[h]

Yesu Aenda Katika Miji Mingine

(Lk 4:42-44)

35 Asubuhi na mapema, ilipokuwa giza na bado hakujapambazuka, Yesu aliamka na kutoka kwenye nyumba ile na kwenda mahali ili awe peke yake na kuomba. 36 Lakini Simoni na wale wote waliokuwa pamoja naye waliondoka kwenda kumtafuta Yesu 37 na walipompata, wakamwambia, “kila mmoja anakutafuta.”

38 Lakini Yesu akawaambia, “Lazima twende kwenye miji mingine iliyo karibu na hapa, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hilo ndilo nililokuja kulifanya.” 39 Hivyo Yesu alienda katika wilaya yote iliyoko mashariki mwa ziwa la Galilaya akihubiri Habari Njema katika masinagogi na kuwafungua watu kutoka katika nguvu za mashetani.

Yesu Amponya Mgonjwa

(Mt 8:1-4; Lk 5:12-16)

40 Ikatokea mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea Yesu na kupiga magoti hadi chini akimwomba msaada. Mtu huyo mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwambia Yesu, “Kama utataka, wewe una uwezo wa kuniponya nikawa safi.”

41 Aliposikia maneno hayo Yesu akakasirika.[i] Lakini akamhurumia. Akautoa mkono wake na kumgusa mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi, na kumwambia, “Ninataka kukuponya. Upone!” 42 Mara moja ugonjwa ule mbaya sana wa ngozi ulimwacha, naye akawa safi.

43 Baada ya hayo Yesu akampa maonyo yenye nguvu na kumruhusu aende zake mara moja. 44 Akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze,[j] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru[k] watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona kwa kuwa safi tena. Ukayafanye haya ili yawe uthibitisho kwa kila mmoja ya kwamba umeponywa.” 45 Lakini mtu yule aliondoka hapo na kwenda zake, na huko alianza kuzungumza kwa uhuru kamili na kusambaza habari hizo. Matokeo yake ni kwamba Yesu asingeweza tena kuingia katika mji kwa wazi wazi. Ikamlazimu kukaa mahali ambapo hakuna watu. Hata hivyo watu walikuja toka miji yote na kumwendea huko.

Footnotes

  1. 1:1 Masihi Yaani “Kristo”, tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”. Tazama Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno. Pia katika mstari wa 20 na katika kitabu chote hiki.
  2. 1:1 Mwana wa Mungu Nakala zingine za Kiyunani hazina maneno haya.
  3. 1:7 viatu vyake “Mimi sistahili kuwa hata kama mmoja wa watumishi wake anayeinama kumfungua kamba za viatu vyake.”
  4. 1:12 Roho Mtakatifu … nyikani Yaani Yesu aliondoshwa kwa nguvu na kupelekwa nyikani.
  5. 1:15 umewafikia Au “unakuja upesi”, au “umekwisha kuja”.
  6. 1:16 Simoni Jina lingine la Petro lilikuwa Simoni. Pia katika mistari wa 29,30,36.
  7. 1:22 mamlaka Hakuhitaji mamlaka yoyote zaidi ya kwake. Kinyume chake waandishi daima waliwanukuu walimu wa kale wa Kiyahudi kama mamlaka ya mafundisho yao.
  8. 1:34 mashetani … yalimjua Mashetani yalifahamu kuwa Yesu alikuwa ni Masihi, mwana wa Mungu. Tazama Mk 3:11-12.
  9. 1:41 akakasirika Nakala nyingi za Kiyunani zimetumia “Akajawa na huruma …”. Lakini ni vigumu kuelezea kwa nini tafsiri za Kiyunani na zile za Kilatini zimekuwa na “Akijawa na hasira …”, Kwa hiyo wasomi wengi zama za leo hudhani hivyo ndivyo ilivyosomeka awali.
  10. 1:44 akakuchunguze Ama akakukague. Sheria ya Musa iliagiza kwamba kuhani anapaswa kuthibitisha kama mwenye ukoma sasa amepona.
  11. 1:44 aliamuru Yaani alizoagiza Musa tazama Law 14:1-32.