Add parallel Print Page Options

Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme

(Mt 21:1-11; Lk 19:28-40; Yh 12:12-19)

11 Walipokaribia Yerusalemu walifika eneo la Bethfage na Bethania lililo karibu na Mlima wa Mizeituni, Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, na kuwaagiza, “Mwende katika kijiji kilichopo ngambo yenu kule, na mara tu mtakapoingia ndani yake mtakuta mwana punda amefungwa mahali na ambaye hajawahi kupandwa na mtu yeyote. Mfungueni na kisha mumlete hapa. Na mtu yeyote akiwauliza, ‘Kwa nini mnafanya hivi?’ ninyi mseme, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha kwenu mara moja.’”

Hivyo wakaondoka, nao wakamkuta mwana punda huyo amefungwa katika mtaa wa wazi karibu na mlango. Wakamfungua. Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu na mahali pale wakawaambia, “Je, kwa nini mnamfungua mwana punda huyo?” Wanafunzi wake wakawaeleza yale walioambiwa na Yesu wayaeleze, nao wakawaacha waende zao.

Kisha wakamleta mwana punda yule kwa Yesu na wakaweka mavazi yao ya ziada juu ya mwana punda, naye akampanda na kukaa juu yake. Watu wengi wakatandika makoti yao barabarani, na wengine wakatandika matawi waliyoyakata kwenye mashamba yaliyo jirani. Wote wale waliotangulia mbele na wale waliofuata walipiga kelele kwa shangwe,

“‘Msifuni[a] Mungu!
Mungu ambariki yeye
    anayekuja katika Jina la Bwana!’(A)
10 Mungu aubariki ufalme unaokuja,
    ufalme wa Daudi baba yetu!
    Msifuni Mungu juu mbinguni!”

11 Ndipo Yesu aliingia Yerusalemu na kwenda hadi kwenye eneo la Hekalu akizunguka na kutazama kila kitu kilichokuwepo mahali hapo. Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda sana, aliondoka kwenda Bethania akiwa na wanafunzi wake kumi na wawili.

Yesu Aulaani Mtini

(Mt 21:18-19)

12 Siku iliyofuata, walipokuwa wakiondoka Bethania, Yesu akawa na njaa. 13 Na kutokea mbali akauona mti wa mtini umefunikwa kwa matawi yake mengi, hivyo akausogelea karibu ili kuona kama atakuta tunda lolote juu yake. Lakini alipoufikia hakukuta tunda lolote isipokuwa matawi tu kwani hayakuwa majira ya mitini kuwepo katika mti. 14 Akauambia mtini ule, “Mtu yeyote asile matunda kutoka kwako kamwe milele!” Na wanafunzi wake waliyasikia hayo maneno.

Yesu Asafisha Eneo la Hekalu

(Mt 21:12-17; Lk 19:45-48; Yh 2:13-22)

15 Walipofika Yerusalemu waliingia katika viwanja vya Hekalu. Yesu akaanza kuwafukuza nje wale waliokuwa wakifanya biashara ya kuuza na kununua katika eneo la Hekalu. Akapindua meza za wabadilishaji wa fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 16 Pia hakumruhusu mtu yeyote abebe kitu chochote kukatiza eneo la Hekalu. 17 Yesu akaanza kuwafundisha na kuwaeleza, “Je, haikuandikwa katika Maandiko kwamba: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ambapo watu wa mataifa yote wataleta maombi yao kwangu’?(B) Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘mahali pa wezi kujificha.’(C)

18 Na viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria waliyasikia haya, na hivyo wakaanza kutafuta njia ya kumuua. Kwani walimwogopa, kwa sababu watu wote walikuwa wamestaajabishwa na mafundisho yake. 19 Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka Yerusalemu.

Mtini na Imani, Maombi na Msamaha

(Mt 21:20-22)

20 Ilipofika asubuhi Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakitembea pamoja na wakauona ule mti wa mtini umekauka kuanzia kwenye mizizi yake. 21 Petro akakumbuka yale Yesu aliyosema kwa mti huo na kumwambia, “Mwalimu, tazama! Mti ule wa mtini ulioulaani umenyauka kabisa.”

22 Yesu akawajibu, “Mnapaswa kuweka imani yenu kwa Mungu. 23 Nawaambia kweli: Yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ukajitupe katika bahari’; kama asipokuwa na mashaka moyoni mwake, Lakini akaamini kuwa kile anachokisema kitatokea, huyo atatendewa hayo. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia chochote mtakachoomba katika sala, muamini kwamba mmekipokea na haja mliyoiomba nayo itakuwa yenu, 25 Na wakati wowote mnaposimama kuomba, mkiwa na neno lolote kinyume na mtu mwingine, mmsamehe mtu huyo. Na Baba yenu aliye mbinguni naye atawasamehe ninyi dhambi zenu.” 26 [b]

Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu

(Mt 21:23-27; Lk 20:1-8)

27 Yesu na wanafunzi wake walirudi Yerusalemu. Na walipokuwa wakitembea ndani ya viwanja vya Hekalu, viongozi wa makuhani, walimu wa Sheria na wazee walimjia Yesu 28 na kumwuliza, “Kwa mamlaka gani unafanya vitu hivi? Nani alikupa mamlaka ya kuvifanya?”

29 Yesu akawaambia, “Nitawauliza swali, na mkinijibu, ndipo nitawaeleza kwa mamlaka gani ninafanya vitu hivi. 30 Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni ama ulitoka kwa watu? Sasa mnijibu basi.”

31 Walijadiliana wao kwa wao wakisema, “Tukisema ‘ulitoka mbinguni’, atasema, ‘Kwa nini basi hamumuamini?’ 32 Lakini kama tukisema kuwa ubatizo wa Yohana ulitoka kwa wanadamu, watu watatukasirikia.” Viongozi waliwaogopa watu, kwani watu wote waliamini kuwa Yohana kweli alikuwa nabii.

33 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatufahamu.”

Hivyo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.”

Footnotes

  1. 11:9 Msifuni Yaani, “Hosanna”, ambalo ni neno la Kiebrania lililotumika kumwomba msaada Mungu. Hapa, labda ilikuwa ni kelele ya shangwe iliyotumika kumsifu Mungu au Masihi wake. Pia katika mstari wa 10.
  2. 11:26 Nakala zingine za awali za Kiyunani zimeongeza mstari wa 26: “Lakini kama hamtawasamehe wengine, basi Baba yenu wa Mbinguni hatawasamehe ninyi dhambi zenu.”