Add parallel Print Page Options

Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao

(Mt 24:1-25; Lk 21:5-24)

13 Yesu alikuwa akiondoka katika eneo la Hekalu na moja ya wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu, tazama mawe haya yanavyopendeza na jinsi majengo haya yanavyopendeza!”

Yesu akamjibu, “Je, mnayaona majengo haya makubwa? Yote yatabomolewa. Kila jiwe litaporomoshwa hata chini. Hakuna jiwe lolote kati ya haya litakaloachwa mahali pake.”

Naye alipokuwa ameketi juu ya Mlima wa Mizeituni upande wa pili kuvuka Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea walimwuliza wakiwa faragha, “Haya tuambie, ni lini mambo haya yatakapotokea? Ni ishara gani itakayoonesha ya kwamba yote yanakaribia kutimizwa?”

Yesu akaanza kuwaeleza, “Muwe waangalifu mtu asije akawadanganya. Wengi watakuja huku wakilitumia Jina langu na kusema, ‘Mimi ndiye Masihi,’[a] nao watawadanganya wengi. Mtasikia juu ya vita vinavyopiganiwa na mtasikia habari juu ya vita vingine vinavyoanza. Hata hivyo msishtushwe. Mambo hayo lazima yatokee, kabla ule mwisho wenyewe kufika. Kwani taifa moja litapigana dhidi ya taifa lingine na ufalme mmoja utapigana dhidi ya ufalme mwingine. Yatatokea matetemeko mengi mahali pengi na kutakuwepo na njaa kali sehemu nyingi. Mambo haya yatakuwa ni mwanzo tu wa uchungu wa mama mzazi kabla ya mtoto kuzaliwa.

Hivyo mjihadhari! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka mkahukumiwe kwa kuwa ninyi ni wanafunzi wangu. Watawapiga katika masinagogi yao. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na watawala. Nanyi mtawaeleza habari zangu. 10 Kabla ya mwisho kufika, ni lazima kwanza habari Njema itangazwe kwa mataifa yote. 11 Wakati wowote watakapowakamata na kuwashitaki, msiwe na wasiwasi kujiandaa kwa yale mtakayoyasema, lakini myaseme yale mtakayopewa saa ile ile, kwa kuwa si ninyi mnaozungumza; bali, ni Roho Mtakatifu anayezungumza.

12 Na ndugu atamsaliti nduguye hata kuuawa, na baba atamsaliti mwanawe. Watoto nao watawaasi wazazi wao na hata kuwatoa wauawe. 13 Nanyi mtachukiwa na wote kwa sababu yangu. Lakini yeyote atakayevumilia hadi mwisho ataokoka.

14 Wakati mtakapoliona chukizo la uharibifu[b] likisimama mahali pasipotakiwa lisimame.” (Msomaji aelewe hii ina maana gani?[c]) “Kisha wale waliopo katika Uyahudi wakimbilie milimani. 15 Ikiwa mtu yupo katika paa la nyumba yake, asishuke chini na kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu chochote. 16 Ikiwa mtu yupo shambani asirudi kuchukua vazi lake.

17 Wakati huo itakuwa hatari kwa wanawake walio waja wazito na wale wenye watoto wachanga. 18 Ombeni kwamba haya yasitokee wakati wa majira ya baridi. 19 Kwa kuwa taabu itakayotokea katika siku hizo itakuwa ile ambayo haijawahi kutokea tangu mwanzo pale Mungu alipoumba dunia hadi sasa. Na hakitatokea tena kitu kama hicho. 20 Kama Bwana asingelifupisha muda huo, hakuna ambaye angenusurika. Lakini yeye amefupisha siku hizo kwa ajili ya watu wale aliowateuwa.

21 Ikiwa mtu atawaambia, ‘Tazama, Kristo ni huyu hapa!’ ama ‘Ni yule pale!’ Usiliamini hilo. 22 Kwani Makristo wa uongo na manabii wa uongo watatokea, nao watafanya ishara na miujiza kuwadanganya watu ikiwezekana hata wale ambao Mungu amewachagua. 23 Kwa hiyo mjihadhari nimewaonya juu ya mambo haya kabla hayajatokea.

Yesu Atakaporudi Tena

(Mt 24:29-51; Lk 21:25-36; 19:12-13,40)

24 Lakini katika siku hizo, baada ya kipindi cha dhiki,

‘Jua litatiwa giza,
    mwezi hautatoa mwanga,
25 nyota zitaanguka kutoka angani,
    na mbingu yote itatikisika.’[d]

26 Ndipo watu watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na nguvu kubwa na utukufu. 27 Baada ya hapo Mwana wa Adamu atawatuma malaika, na atawakusanya wateule wake kutoka kila upande wa dunia.

28 Jifunzeni somo hili kutoka katika mti wa mtini: Matawi yake yanaponyauka na kubeba majani, unajua kwamba kiangazi kimekaribia. 29 Vivyo hivyo, unapoona mambo haya yanaanza kutokea unajua kwamba muda umekaribia na umeshafika mlangoni. 30 Ninawaambieni ukweli: Kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo haya yote hayajatokea. 31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

32 Hakuna anayejua wakiwemo malaika wa mbinguni ama Mwana bali baba peke yake lini siku au saa ile itakapowadia. 33 Mjihadhari; Kesheni! Kwani hamjui lini muda huo utafika.

34 Ni kama mtu anayeenda safarini na kabla ya kuondoka huiacha nyumba yake mikononi mwa watumishi wake. Kabla ya kuiacha nyumba yake anawaweka watumishi wake kusimamia kila mmoja akiwa na kazi yake maalumu. Kisha atamwamuru mlinzi mlangoni awe macho. 35 Vivyo hivyo ni lazima mjihadhari, kwa sababu hamjui ni muda gani mkuu wa nyumba atakuja; hamjui kama atakuja jioni, usiku wa manane, wakati jogoo anawika, au alfajiri. 36 Ikiwa atakuja ghafula, basi asiwakute mmelala. 37 Ninachowaambia, namwambia kila mmoja: ‘muwe tayari.’”

Footnotes

  1. 13:6 Masihi Kwa maana ya kawaida, “Yule ambaye”, kwa maana ya Mfalme Mteule wa Mungu aliyetumwa na Mungu. Tazama Mt 24:5 na Masihi katika Orodha ya Maneno.
  2. 13:14 chukizo la uharibifu Ni maneno yanayoashiria kitu ambacho Mungu hapendezwi nacho. Tazama Dan 9:27; 11:31 na 12:11.
  3. 13:14 Msomaji aelewe hii ina maana gani Mwandishi anamtaka msomaji azingatie kwamba anazungumzia Jeshi la Rumi ambalo litaharibu Yerusalemu, ingawa hataki kulielezea hili kwa wazi. Tazama Lk 21:20-24.
  4. 13:24-25 Tazama Isa 13:10; 34:4.