Add parallel Print Page Options

Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato

(Mt 12:9-14; Lk 6:6-11)

Kwa mara nyingine tena Yesu alikwenda kwenye sinagogi. Huko alikuwepo mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa. Watu wengine walikuwa wakimwangalia Yesu kwa karibu sana. Walitaka kuona ikiwa angemponya mtu yule siku ya Sabato,[a] ili wapate sababu ya kumshitaki. Yesu akamwambia yule mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa, “Simama mbele ili kila mtu akuone.”

Ndipo Yesu akawaambia, “Je, ni halali kutenda mema ama kutenda mabaya siku ya Sabato? Je, ni halali kuyaokoa maisha ya mtu fulani ama kuyapoteza?” Lakini wao walikaa kimya.

Yesu akawatazama wote waliomzunguka kwa hasira lakini alihuzunika kwa sababu waliifanya mioyo yao kuwa migumu. Akamwambia mtu yule “nyosha mkono wako”, naye akaunyosha, na mkono wake ukapona. Kisha Mafarisayo wakaondoka na papo hapo wakaanza kupanga njama pamoja na Maherode kinyume cha Yesu kutafuta jinsi gani wanaweza kumuua.

Wengi Wamfuata Yesu

Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake hadi Ziwa Galilaya, na kundi kubwa la watu kutoka Galilaya likawafuata, pamoja na watu kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumea, na katika maeneo yote ng'ambo ya Mto Yordani na yale yanayozunguka Tiro na Sidoni. Lilikuwa kundi kubwa sana la watu. Wote walimjia Yesu kwa sababu walikuwa wamesikia mambo aliyokuwa anafanya.

Kwa sababu ya kundi, aliwaambia wanafunzi wake, kumtayarishia mashua mdogo, ili kwamba wasiweze kumsonga na kumbana. 10 Yesu alikuwa ameponya watu wengi. Hivyo wote wale waliokuwa na magonjwa waliendelea kujisogeza mbele kumwelekea ili wamguse. 11 Kila mara pepo wachafu walipomwona Yesu, walianguka chini mbele yake, na kulia kwa sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!” 12 Lakini yeye aliwaamuru kila mara wasimwambie mtu yeyote yeye ni nani.

Yesu Achagua Wanafunzi Wake Kumi na Wawili

(Mt 10:1-4; Lk 6:12-16)

13 Kisha Yesu akapanda juu kwenye vilima na akawaita baadhi ya wanafunzi wake, hasa wale aliowataka wajiunge naye pale. 14 Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume. Aliwachagua ili waambatane pamoja naye, na kwamba aweze kuwatuma sehemu mbalimbali kuhubiri ujumbe wa neno la Mungu. 15 Pia aliwapa mamlaka ya kufukuza mashetani toka kwa watu. 16 Yafuatayo ni majina ya mitume kumi na wawili aliowateuwa Yesu:

Simoni ambaye Yesu alimwita Petro,

17 Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu yake (ambao wote Yesu aliwaita Boanergesi), yaani “wana wa ngurumo yenye radi”,

18 Andrea,

Filipo,

Bartholomayo,

Mathayo,

Thomaso,

Yakobo mwana wa Alfayo,

Thadayo,

Simoni Mzelote

19 na Yuda Iskariote,[b] ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.

Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu

(Mt 12:22-32; Lk 11:14-23; 12:10)

20 Kisha Yesu akaenda nyumbani. Kwa mara nyingine tena umati wa watu ukakusanyika, kiasi kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakupata nafasi ya kula. 21 Familia ya Yesu ilipoyasikia haya, walikwenda kumchukua kwa sababu watu walisema amerukwa na akili.

22 Walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikuwa wanasema, “Yeye ana Beelzebuli[c] ndani yake! Kwani anafukuza mashetani kwa nguvu ya mkuu wa mashetani!”

23 Yesu akawaita na kuanza kuzungumza nao kwa kulinganisha: “Inawezekanaje Shetani ambaye ni roho mchafu kufukuza mashetani? 24 Ikiwa basi ufalme utagawanyika katika sehemu mbili zinazopingana zenyewe kwa zenyewe, ufalme huo hautaendelea. 25 Vivyo hivyo ufalme wa Shetani ukigawanyika naye akapigana dhidi ya pepo wake wabaya, basi huo utakuwa ndio mwisho wa ufalme wake. Pia ikiwa nyumba itapingana yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haitaweza kusalimika. 26 Kwa hiyo ikiwa Shetani atajipinga mwenyewe na kugawanyika basi hataweza kuendelea na huo utakuwa mwisho wake.

27 Hakika, hakuna anayeweza kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuzichukua mali zake bila kwanza kumfunga mtu huyo mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kuiba katika nyumba hiyo.

28 Ninawaambia ukweli: Watu wanaweza kusamehewa dhambi zao zote na maneno yao yenye matusi kwa Mungu. 29 Lakini yeyote atakayemtukana Roho Mtakatifu hatasamehewa kabisa. Kwa sababu mtu anayefanya hivyo atakuwa na hatia ya dhambi isiyosamehewa milele.”

30 Yesu alisema haya kwa sababu walimu wa sheria walikuwa wanasema, “Yeye ana pepo mchafu ndani yake.”

Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi

(Mt 12:46-50; Lk 8:19-21)

31 Kisha mama yake Yesu na nduguze wakaja. Wao walisimama nje na wakamtuma mtu aende kumwita ndani. 32 Humo lilikuwepo kundi lililoketi kumzunguka, lakini wao wakamwambia, “Tazama! Mama yako, kaka zako na dada zako wako[d] nje wanakusubiri.”

33 Yesu akauliza, “Mama yangu ni nani na kaka zangu ni akina nani?” 34 Yesu akawatazama wale walioketi kumzunguka na akasema “Hapa yupo mama yangu na wapo kaka zangu na dada zangu! 35 Yeyote anayeyafanya mapenzi ya Mungu ndiye kaka yangu, dada yangu, na mama yangu.”

Footnotes

  1. 3:2 Walitaka … siku ya Sabato Haikuruhusiwa kwa Wayahudi kufanya kazi siku ya Sabato na wengi waliamini kumponya mtu ambaye hakuwa katika hatari ya kufa ilikuwa ni kazi.
  2. 3:19 Iskariote Yaweza kuwa “kutoka Kirioti”, mji kusini mwa Yuda.
  3. 3:22 Beelzebuli Kwa maana ya kawaida, “Shetani”. Jina hili limetumika badala ya lile la Shetani.
  4. 3:32 na dada zako wako Nakala zingine za Kiyunani hazina maneno haya.