Add parallel Print Page Options

Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 4,000

(Mt 15:32-39)

Wakati mwingine katika siku zile kundi kubwa la watu lilikusanyika na halikuwa na chakula. Yesu akawaita wanafunzi wake na kuwaambia, “Nawahurumia watu hawa, kwa sababu hata sasa wamekuwa nami kwa siku tatu, na hawana kitu cha kula.”

Nikiwaacha waende majumbani mwao wakiwa na njaa, wataanguka njiani; na baadhi yao wametoka mbali.

Wanafunzi wake wakamjibu, “Wapi mtu yeyote atapata chakula cha kutosha mahali hapa jangwani cha kuwalisha watu hawa?”

Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakajibu, “Saba.”

Kisha Yesu akaliagiza kundi la watu kuketi chini ardhini Akachukua mikate ile saba, akashukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake waigawe. Nao wakaigawa kwenye kundi. Kulikuwapo pia samaki wadogo wachache. Yesu akawabariki wale samaki na kuwaambia waigawe nayo pia.

Watu walikula na kushiba. Wakakusanya vikapu saba vilivyojaa mabaki. Ilikuwa kama watu 4,000. Kisha Yesu akawaacha waende. 10 Mara Yesu akapanda katika mashua na wanafunzi wake, na akafika katika wilaya ya Dalmanutha.

Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu

(Mt 16:1-4; Lk 11:16,29)

11 Mafarisayo wakamwendea Yesu na kuanza kubishana naye. Ili kumjaribu wakamwomba ishara kutoka mbinguni. 12 Yesu alihema kwa nguvu na kusema, “Kwa nini kizazi kinataka ishara? Ninawaambia ukweli: hakuna ishara itakayooneshwa kwa kizazi hiki.” 13 Kisha Yesu akawaacha, akapanda tena katika mashua, na akaondoka kwenda upande wa pili wa ziwa.

Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu

(Mt 16:5-12)

14 Wakati huo huo wanafunzi walikuwa wamesahau kuleta mikate yo yote, na hawakuwa na kitu kingine isipokuwa mkate mmoja. 15 Yesu akawaonya, akasema, “Mwe mwangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ile ya Herode.”

16 Nao wakaanza kujadiliana haya miongoni mwao: “Labda alisema hivi kwa sababu hatukuwa na mkate wowote.”

17 Akijua walichokuwa wakikisema, akawaambia, “Kwa nini mnajadiliana juu ya kutopata mkate? Je! Bado hamwoni na kuelewa? Je! Mmezifunga akili zenu. 18 Mnayo macho; Je! Hamwoni? Mnayo masikio; Je! Hamwezi kusikia? Mnakumbuka? 19 Nilipomega na kugawa mikate mitano kwa watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?”

Wakasema “Kumi na viwili”.

20 “Nilipomega na kugawa mikate saba kwa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?”

Wakasema “Saba”.

21 Kisha akawaambia, “Bado hamwelewi?”

Yesu Amponya Kipofu katika Kijiji cha Bethsaida

22 Walipofika katika kijiji cha Bethsaida, baadhi ya watu walimleta asiyeona kwa Yesu, na kumsihi Yesu amguse. 23 Yesu alimshika mkono yule asiyeona na kumtoa nje ya kijiji. Kisha Yesu alimtemea mate yule asiyeona kwenye macho yake, akaweka mkono wake juu ya asiyeona, na kumwuliza, “Je! Unaona kitu chochote?”

24 Kipofu akatazama juu na kusema, “Ninaona watu; wanaonekana kama miti inayotembea.”

25 Kisha Yesu akaweka mikono yake tena kwenye macho ya yule asiyeona. Naye akafumbua wazi macho yake yote. Kwani alipona kutokuona kwake na kuona kila kitu kwa uwazi. 26 Kisha Yesu akamwambia arudi nyumbani, na pia akamwambia, “Usiingie kijijini.”

Petro Atambua Yesu ni Nani

(Mt 16:13-20; Lk 9:18-21)

27 Yesu na wanafunzi wake walikwenda kwenye vijiji vinavyozunguka Kaisaria Filipi. Wakiwa njiani aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?”

28 Nao wakamjibu, “Yohana Mbatizaji. Wengine husema wewe ni Eliya. Na wengine husema wewe ni mmoja wa manabii.”

29 Kisha akawauliza wao, “Na ninyi; Je! Mnasema mimi ni nani?”

Petro akamjibu, “Wewe ni masihi.”

30 Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote kuhusu yeye.

Yesu Asema ni Lazima Afe

(Mt 16:21-28; Lk 9:22-27)

31 Ndipo alianza kuwafundisha akisema: “Mwana wa Adamu lazima apate mateso mengi, na kukatataliwa na wazee, wakuu wa makuhani na walimu wa Sheria, na ni lazima atauawa na Kufufufuka baada ya siku ya tatu.” 32 Yesu aliwaambia haya kwa uwazi bila kuwaficha.

Baada ya mafundisho haya Petro alimchukua Yesu pembeni na kuanza kumkemea. 33 Lakini Yesu aligeuka nyuma na kuwaangalia wanafunzi wake, na kumkemea Petro kwa kumwambia, “Shetani,[a] toka mbele yangu! Huyajali yale anayoyajali Mungu bali yale wanayoyaona wanadamu kuwa ni muhimu.”

34 Kisha Yesu akaliita kundi lote pamoja na wanafunzi wake kwake, akawaambia, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, lazima ajikane yeye mwenyewe, na ni lazima auchukue msalaba wake mwenyewe kisha anifuate. 35 Kwa kuwa kila anayetaka kuusalimisha uhai wake, ataupoteza, na yeyote atakayeupoteza uhai wake kwa ajili yangu na kwa ajili ya injili atausalimisha. 36 Itampa mtu manufaa gani akiupata ulimwengu wote kisha akaupoteza uhai wake? 37 Mtu anaweza kuubadilisha uhai wake na kitu gani? 38 Hiki ni kizazi chenye dhambi na kisichokuwa na uaminifu. Hivyo, mtu yeyote atakayenionea haya mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea haya mtu huyo siku ile atakaporudi katika utukufu wa Baba yake akiwa na malaika wake watakatifu.”

Footnotes

  1. 8:33 Shetani Jina la Mwovu lenye maana “Adui”. Maana ya Yesu ni kuwa Petro alikuwa akiongea kama Shetani.