Add parallel Print Page Options

Naye Yesu aliwaambia, “Ninawaambia Ukweli: baadhi yenu mnaosimama hapa mtauona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu kabla ya kufa kwenu.”

Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya

(Mt 17:1-13; Lk 9:28-36)

Baada ya siku sita, Yesu akamchukua Petro, Yakobo na Yohana na kuwaongoza hadi mlima mrefu wakiwa peke yao tu. Na mwonekano wa Yesu ulibadilika mbele yao. Huko Yesu akabadilika sura nyingine akiwa mbele yao. Mavazi yake yakiwa na mng'ao, na meupe kabisa kuliko mtu anavyoweza kufua nguo kwa sabuni na kuitakatisha. Huko Eliya na Musa pia wakawatokea, na Yesu alizungumza na manabii hao wawili.

Petro akafungua kinywa chake na kumwambia Yesu, “Mwalimu, ni vyema tupo hapa. Tufanye basi vibanda vitatu; moja kwa ajili yako, moja kwa ajili ya Musa na moja kwa ajili ya Eliya.” Petro aliyasema haya kwa sababu hakujua aseme nini, kwa sababu yeye na wenzake walikuwa wamepata hofu.

Ndipo wingu likaja na kuwafunika wote kwa kivuli chake. Na sauti ikatoka mawinguni, ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa. Msikilizeni yeye.”

Ndipo ghafula walipokuwa wakiangalia huku na huko, hawakuona mtu yeyote akiwa pamoja nao isipokuwa Yesu peke yake.

Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote kile walichokiona mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka katika wafu.

10 Hivyo hawakuwaeleza wengine juu ya jambo lile bali walijadiliana miongoni mwao wenyewe juu ya maana ya “kufufuka kutoka kwa wafu.” 11 Wakamwuliza Yesu, “kwa nini walimu wa sheria wanasema Eliya lazima aje kwanza?”

12 Yesu akawaambia, “Ndiyo, Eliya atakuja kwanza[a] kuja kuyaweka mambo yote sawa kama jinsi yalivyokuwa hapo mwanzo. Lakini kwa nini imeandikwa juu ya Mwana wa Adamu[b] ya kwamba itampasa kuteswa na kudhalilishwa? 13 Lakini ninawaambia, Eliya amekuja,[c] na walimtendea kila kitu walichotaka, kama vile ilivyoandikwa[d] kuhusu yeye.”

Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu

(Mt 17:14-20; Lk 9:37-43a)

14 Wakati Yesu, Petro, Yakobo, na Yohana walipowafikia wanafunzi wengine, waliliona kundi kubwa la watu lililowazunguka na wakawaona walimu wa Sheria wakibishana nao. 15 Mara tu watu wote walipomwona Yesu, walishangazwa, na wakakimbia kwenda kumsalimia.

16 Akawauliza, “Mnabishana nao kitu gani?”

17 Na mtu mmoja kundini alimjibu, “Mwalimu, nilimleta mwanangu kwako ili umponye. Yeye amefungwa na pepo mbaya anayemfanya asiweze kuzungumza. 18 Na kila mara anapomshambulia humtupa chini ardhini. Naye hutokwa mapovu mdomoni na kusaga meno yake, huku akiwa mkakamavu. Nami niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze kutoka ndani yake, lakini hawakuweza.”

19 Kisha Yesu akajibu na kuwaambia, “ninyi kizazi kisichoamini, kwa muda gani niwe pamoja nanyi? Kwa muda gani nitapaswa kuchukuliana nanyi? Mleteni huyo mvulana kwangu.”

20 Wakamleta yule mvulana kwake. Na yule pepo alipomwona Yesu, kwa ghafula akamtingisha yule mvulana ambaye alianguka chini kwenye udongo, akivingirika na kutokwa povu mdomoni.

21 Yesu akamwuliza babaye, “Kwa muda gani amekuwa katika hali hii?”

Yule babaye akajibu akisema, “amekuwa katika hali hii tangu utoto. 22 Mara nyingi anamtupa katika moto ama katika maji ili kumwua. Lakini ikiwa unaweza kufanya kitu chochote, uwe na huruma na utusaidie.”

23 Yesu akamwambia, “Una maana gani kusema ‘ikiwa unaweza’? Kila kitu kinawezekana kwake yeye anayeamini.”

24 Mara, babaye yule mvulana alilia kwa sauti kubwa na kusema, “Naamini! Nisaidie kutokuamini kwangu.”

25 Yesu alipoona lile kundi likizidi kuwa kubwa, alimkemea yule pepo mchafu na kumwambia, “Wewe pepo uliyemfanya mvulana huyu asiweze kusikia na asiweze kusema, nakuamuru, utoke ndani yake, na usimwingie tena!”

26 Na pepo yule alilia kwa sauti, akamtupa yule mvulana chini katika mishituko ya kutisha, kisha akatoka, naye akawa kama mtu aliyekufa, kiasi kwamba watu wengi wakadhani ya kuwa amekufa. 27 Lakini Yesu akamshika yule mvulana mikononi, na kumwinua naye akasimama.

28 Baada ya Yesu kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuuliza wakiwa peke yao, “Kwa nini sisi hatukuweza kumfukuza pepo yule?”

29 Naye akawaambia, “Aina hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa maombi.”[e]

Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake

(Mt 17:22-23; Lk 9:43-45)

30 Wakaondoka mahali pale na kusafiri kupitia Galilaya. Yesu hakutaka mtu yeyote kujua walikuwa huko, 31 alitaka kuwafundisha wanafunzi wake peke yake. Na Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kuwekwa mikononi mwa watu wengine, nao watamwua. Kisha siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.” 32 Lakini hawakuuelewa usemi huu, na walikuwa wanaogopa kumuuliza zaidi.

Nani ni Mkuu Zaidi?

(Mt 18:1-5; Lk 9:46-48)

33 Kisha wakaja Kapernaumu. Na Yesu alipokuwa ndani ya nyumba aliwauliza, “Je, mlikuwa mnajidiliana nini njiani?” 34 Lakini wao walinyamaza kimya, kwa sababu njiani walikuwa wamebishana juu ya nani kati yao alikuwa ni mkuu zaidi.

35 Hivyo Yesu aliketi chini, akawaita wale kumi na mbili, na akawaambia, “Ikiwa yupo mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, inapasa basi awe wa mwisho kuliko wote na mtumishi wa wote.”

36 Akamchukua mtoto mdogo mikononi mwake na kumsimamisha mbele yao. Akimkumbatia mtoto huyo, Yesu alisema, 37 “Yeyote atakayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu hapa kwa sababu ya jina langu basi ananikaribisha na mimi pia. Yeyote anayenikubali mimi hanikubali mimi tu bali anamkubali pia yeye aliyenituma.”

Yeyote Ambaye Hayuko Kinyume Chetu Yuko Pamoja Nasi

(Lk 9:49-50)

38 Yohana akamwambia Yesu, “Mwalimu tulimwona mtu akifukuza pepo kwa jina lako. Nasi tulijaribu kumzuia, kwa sababu hakuwa mmoja wetu.”

39 Lakini Yesu akawaambia, “Msimzuie, kwa sababu hakuna atendaye miujiza kwa jina langu kisha mara baada ya hilo aseme maneno mabaya juu yangu. 40 Yeye ambaye hapingani na sisi basi yuko pamoja na sisi. 41 Yeyote anayewapa ninyi kikombe cha maji kwa sababu ninyi ni wake Kristo.[f] Hakika ninawaambia ukweli kwamba, hatapoteza thawabu yake.

Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi

(Mt 18:6-9; Lk 17:1-2)

42 Yeyote anayemsababisha mmoja wa hawa walio wadogo ambao wananiamini mimi kujikwaa na kuanguka, itakuwa bora kwake ikiwa atatupwa baharini huku amefungwa jiwe la kusagia shingoni mwake. 43 Ikiwa mkono wako unakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa na mkono mmoja kuliko kuwa na mikono miwili na kuenda Jehanamu, ambako kuna moto usiozimika. 44 [g] 45 Na ikiwa mguu wako utakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa mlemavu kuliko kuwa na miguu miwili na kutupwa Jehanamu. 46 [h] 47 Na kama jicho lako litakusababisha ufanye dhambi, liondoe. Ni bora uingie katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja kuliko kuwa nayo macho mawili na kutupwa Jehanamu, 48 ambapo waliomo watatafunwa na funza wasiokufa na kuchomwa na moto usiozimika kamwe.(A)

49 Kwa kuwa kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.[i]

50 Chumvi ni njema. Lakini ikiwa chumvi itaharibika, utawezaje kuifanya chumvi tena? Muwe na chumvi miongoni mwenu na muishi kwa amani ninyi kwa ninyi.”

Footnotes

  1. 9:12 atakuja kwanza Ama atatangulia.
  2. 9:12 Mwana wa Adamu Jina lingine alilojitambulisha Yesu.
  3. 9:13 Eliya amekuja Habari hii inamhusu Yohana Mbatizaji.
  4. 9:13 kama vile ilivyoandikwa Hii inahusu maandiko ya Agano la Kale.
  5. 9:29 maombi Nakala zingine za Kiyunani zina “maombi na kufunga”.
  6. 9:41 Kristo Mpakwa mafuta au masihi, aliyechaguliwa na Mungu.
  7. 9:44 Nakala zingine za Kiyunani zinaongeza mstari wa 44, ambao ni sawa na mstari 48.
  8. 9:46 Nakala zingine za Kiyunani zinaongeza mstari wa 46, ambao ni sawa na mstari 48.
  9. 9:49 Nakala zingine za Kiyunani zinaongeza, “Kila dhabihu itatiwa chumvi.” Katika Agano la Kale chumvi ilinyunyiziwa kwenye dhabihu. Mstari huu unaweza kuwa na maana kuwa wanafunzi wa Yesu watajaribiwa kwa mateso na kwamba wanapaswa kujitoa wenyewe kwa Mungu kama dhabihu.