Yesu Afundisha Kuhusu Talaka

10 Yesu akaondoka mahali pale akavuka mto wa Yordani, akaenda sehemu ya Yudea. Umati wa watu ukamfuata tena na kama kawaida yake akawafundisha.

Baadhi ya Mafarisayo wakamjia wakitaka kumtega, wakamwul iza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake?”

Yesu akawajibu, “Musa aliwaamuruje?” Wakamjibu, “Musa aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”

Yesu akawaambia, “Musa aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mume na mke. Na kwa sababu hii mume atamwacha baba yake na mama yake na hao wawili, watakuwa mwili mmoja.’ Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena bali mwili mmoja. Basi, alichokiun ganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

10 Baadaye waliporudi nyumbani , wanafunzi wa Yesu walimwul iza kuhusu jambo hili.

11 Akawajibu, “Mtu ye yote anayempa mkewe talaka na kuoa mke mwingine, anazini kwa yule mke aliyempa talaka. 12 Na mwa namke anayempa mumewe talaka na kuolewa na mume mwingine, anazini pia.”

Yesu Anawabariki Watoto Wadogo

13 Watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse lakini wanafunzi wake wakawakemea. 14 Yesu alipoona yaliyokuwa yakitokea alichukizwa, akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa watu kama hawa! 15 Ninawahakikishieni kwamba, mtu ye yote ambaye hataukubali Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.” 16 Akawakumbatia wale watoto wadogo, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.

Mtu Tajiri

17 Yesu alipoanza tena safari yake, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini niurithi Ufalme wa milele?”

18 Yesu akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna ali yemwema isipokuwa Mungu peke yake. 19 Unazifahamu amri ‘Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye. Waheshimu baba yako na mama yako .”’

20 Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”

21 Yesu akamtazama kwa moyo wa upendo akamwambia, “Umepun gukiwa na kitu kimoja tu. Nenda ukauze vitu vyote ulivyo navyo uwape maskini fedha utakazopata, nawe utakuwa na utajiri mbin guni; kisha njoo, unifuate.”

22 Yule mtu aliposikia hayo, alisikitika sana, akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa tajiri sana.

23 Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Itakuwa vigumu sana kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa

Mungu!”

24 Wanafunzi wake wakashtushwa sana na maneno hayo. Lakini Yesu akasema tena, “Wanangu, ni vigumu sana kuingia katika Ufalme wa Mungu. 25 Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

26 Wanafunzi wake wakashangaa mno. Wakaulizana wao kwa wao, “Ni nani basi anaweza kuokolewa?”

27 Yesu akawatazama akawaambia, “Kwa wanadamu haiwezekani, lakini kwa Mungu si hivyo. Mambo yote yanawezekana kwa Mungu.” 28 Petro akaanza kumwambia, “Sisi tumeacha kila kitu tukakufu ata!”

29 Yesu akajibu, “Ninawaambieni hakika, hakuna mtu ye yote aliyeacha nyumba, kaka, dada, mama, baba, watoto au shamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya kuitangaza Habari Njema, 30 ambaye hatalipwa katika ulimwengu huu mara mia zaidi: nyumba, kaka, dada, mama, watoto, mashamba na mateso pia; na kupewa uzima wa milele katika ulimwengu ujao. 31 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho na wa mwisho watakuwa wa kwanza.”

Yesu Azungumzia Tena Kifo Chake

32 Walikuwa njiani kuelekea Yerusalemu na Yesu alikuwa ame tangulia. Wanafunzi wake walikuwa wamejawa na hofu, na watu wal iowafuata walikuwa wanaogopa. Yesu akawachukua tena wale wana funzi wake kumi na wawili kando akawaambia yatakayompata. 33 Akasema, “Tunakwenda Yerusalemu, na Mimi Mwana wa Adamu nitapelekwa kwa makuhani wakuu na walimu wa sheria; nao watanihu kumu adhabu ya kifo na kunikabidhi kwa mataifa. 34 Wao watanid hihaki na kunitemea mate na kunipiga na kuniua. Baada ya siku tatu, nitafufuka.”

Ombi La Yakobo Na Yohana

35 Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo wakamwendea Yesu wakamwambia, “Bwana, kuna jambo moja tungependa kukuomba.”

36 Akawauliza, “Mngependa niwafanyie jambo gani?”

37 Wakamjibu, “ Tunakuomba utakapoketi katika ufalme wako wa utukufu, uturuhusu tuketi pamoja nawe, mmoja wetu mkono wako wa kulia na mwingine mkono wako wa kushoto.”

38 Yesu akawaambia, “Hamjui mnaloliomba. Mko tayari kunywea kikombe cha mateso nitakachokunywa? Mnaweza kubatizwa ubatizo nitakaobatizwa?”

39 Wakamjibu, “ Tunaweza.” Yesu akawaambia, “Mtakunywa katika kikombe nitakachokunywa na kubatizwa ubatizo nitakaobati zwa. 40 Lakini kuhusu kuketi mkono wangu wa kulia au wa kushoto si juu yangu mimi kuwaruhusu. Mungu atatoa nafasi hizo kwa watu aliowaandalia.”

41 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, waliwaka sirikia Yakobo na Yohana. 42 Yesu akawaita wanafunzi wake wote pamoja akawaambia, “Mnafahamu kwamba watu wanaotawala watu wa mataifa hutumia mabavu, na viongozi wa vyeo vya juu hupenda kuon yesha wana madaraka! 43 Lakini haipasi kuwa hivyo kati yenu. Badala yake, anayetaka kuwa mkuu kati yenu hana budi kuwa mtum ishi wenu, 44 na ye yote anayetaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa mtumishi wa wote. 45 Kwa maana hata mimi Mwana wa Adamu sikuja ili nitumikiwe, bali nilikuja ili niwe mtumishi na kutoa maisha yangu yawe fidia kwa ajili ya watu wengi.”

Yesu Amponya Kipofu Bartimayo

46 Wakafika Yeriko. Na Yesu alipokuwa akiondoka pamoja na Wanafunzi wake na umati wa watu, kipofu mmoja, jina lake Barti mayo, mwana wa Timayo, alikuwa ameketi kando kando ya njia, akiomba.

47 Aliposikia kuwa Yesu wa Nazareti alikuwa akipita, akaanza kupiga kelele, “Yesu, Mwana wa Daudi, nionee huruma!”

48 Watu wengi wakamkemea, wakamwambia akae kimya. Lakini yeye alipiga kelele zaidi, “Mwana wa Daudi, nionee huruma!”

49 Yesu akasimama akawaambia, “Mwiteni.” Wakamwita wakamwambia, “Changamka! Usimame, anakuita.”

50 Akatupa vazi lake kando, akaruka juu, akamwendea Yesu. 51 Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Yule kipofu akajibu, “Mwalimu, nataka kuona tena.” 52 Yesu akamwambia, “Nenda, imani yako imekuponya.” Wakati huo huo akaweza kuona, akamfuata Yesu njiani.

Yesu Afundisha Kuhusu Talaka

(Mt 19:1-12)

10 Naye aliondoka mahali pale, na kufika katika nchi ya Uyahudi ng'ambo ya Mto Yordani. Na makundi ya watu wakamjia tena na kama alivyofanya daima aliwafundisha.

Kisha baadhi ya Mafarisayo walimwendea na kumwuliza “Je, ni sahihi mtu kumtaliki mkewe?” Nao walimwuliza hivyo ili kumjaribu.

Yesu akawajibu, “Musa aliwapa amri mfanye nini?”

Wakasema, “Musa alimpa ruhusa mume kuandika hati ya kutangua ndoa[a] na kisha kumtaliki mke wake.”

Yesu akawaambia, “Musa aliwaandikia amri hii kwa sababu ninyi ni wakaidi na hamkutaka kuyapokea mafundisho ya Mungu. Lakini tangu mwanzo wa uumbaji wake Mungu ‘aliwaumba mwanaume na mwanamke’.(A) ‘Basi kwa sababu ya hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, na kujiunga na mkewe. Na hao wawili wataungana pamoja na kuwa mwili mmoja.’(B) Nao si wawili tena bali ni mwili mmoja. Kwa hiyo, mtu yeyote asitenganishe kile ambacho Mungu amekiunganisha pamoja.”

10 Walipokuwa ndani ya nyumba ile kwa mara nyingine, wanafunzi wake wakamwuliza Yesu juu ya jambo hili. 11 Naye akawaambia, “yeyote atakayemtaliki mke wake na kuoa mwanamke mwingine, anazini kinyume cha mkewe. 12 Na ikiwa mke atamtaliki[b] mumewe na kuolewa na mume mwingine, basi naye anafanya zinaa.”[c]

Yesu Awakaribisha Watoto

(Mt 19:13-15; Lk 18:15-17)

13 Nao watu wakawaleta watoto wadogo kwa Yesu, ili aweze kuwawekea mikono na kuwabariki. Hata hivyo wanafunzi wake waliwakemea. 14 Yesu alipoona hayo, alikasirika, na akawaambia, “Waruhusuni watoto hao waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu kama hao. 15 Ninawaambia kweli, Yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyoupokea hataweza kuingia ndani yake.” 16 Naye Yesu akawakumbatia watoto kifuani mwake na akaweka mikono yake juu yao na kuwabariki.

Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu

(Mt 19:16-30; Lk 18:18-30)

17 Na alipokuwa ameanza safari, mtu mmoja alimkimbilia, akafika na kupiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?

18 Yesu akamwuliza, kwa nini unaniita mimi mwema? Hakuna aliye mwema isipokuwa Mungu peke yake. 19 Je, unazijua amri: Usiue, usizini, usiibe, usitoe ushahidi wa uongo, usidanganye wengine, uwaheshimu baba na mama yako.”(C)

20 Naye akamwambia Yesu, “Mwalimu, nimeyatii hayo tangu ujana wangu.”

21 Yesu akamwangalia. Naye akashikwa na upendo kwa mtu yule, na hivyo akamwambia, “umekosa kitu kimoja: Nenda ukaviuze vyote ulivyo navyo kisha ukawape walio maskini, nawe utakuwa umejitunzia hazina mbinguni. Kisha uje ukanifuate.”

22 Yule mtu alisikitishwa sana na usemi huo, na akaondoka kwa huzuni kwa kuwa alikuwa na mali nyingi.

23 Yesu aligeuka kuwatazama wanafunzi wake na kuwaambia wake, “Angalieni jinsi ilivyo vigumu sana kwa walio na mali nyingi kuingia katika ufalme wa Mungu.”

24 Wanafunzi wake walistaajabishwa na maneno yale. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, ni vigumu[d] sana kuuingia ufalme wa Mungu. 25 Kwani ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuuingia ufalme wa Mungu.”

26 Nao walistajaabu zaidi, na wakaambiana wao kwa wao, “Ni nani basi atakayeweza kuokolewa?”

27 Huku akiwatazama, Yesu alisema, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, lakini kwa Mungu linawezekana, kwa sababu yote yanawezekana kwake Mungu.”

28 Petro akaanza kumwambia, “Tazama! Tumeacha kila kitu tukakufuata.”

29 Yesu akasema, “Nawaambieni kweli: Hakuna aliyeacha nyumba, kaka, dada, mama, baba, watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili 30 ambaye hatapata malipo mara mia zaidi katika nyakati hizi; nyumba, kaka, dada, mama, watoto, na mashamba, pamoja na mateso; na uzima wa milele katika kizazi kinachokuja. 31 Lakini wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho baadaye na wale walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza baadaye.”

Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake

(Mt 20:17-19; Lk 18:31-34)

32 Walikuwa wote njiani wakipanda kuelekea Yerusalemu, na Yesu alikuwa akitembea mbele yao. Nao walisumbuka sana. Na wale waliowafuata walikuwa na hofu pia. Kwa mara nyingine Yesu akawachukua wale wanafunzi kumi na mbili pembeni, na akaanza kuwaeleza yale yatakayomtokea Yerusalemu. 33 “Sikilizeni! Tunaelekea hadi Yerusalemu na Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria, nao watamtia hatiani na kumpa hukumu kifo, kisha watamtoa kwa wale wasio Wayahudi, 34 Nao watamdhihaki, na watamtemea mate, na watamchapa kwa viboko vya ngozi, nao watamwua. Ndipo atafufuka baada ya siku ya tatu.”

Yakobo na Yohana Waomba Kutawala Pamoja na Yesu

(Mt 20:20-28)

35 Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu, wakamwambia, “Mwalimu tunataka utufanyie kile tunachokuomba.”

36 Yesu akawaambia, “Ni kitu gani mnachotaka niwafanyie?”

37 Nao wakamwambia, “Uturuhusu tuketi pamoja nawe katika utukufu wako, mmoja wetu aketi kulia kwako na mwingine kushoto kwako.”

38 Yesu akawaambia, “Hamjui mnachokiomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninachokinywea[e] mimi? Au mnaweza kubatizwa ubatizo ninaobatizwa?”

39 Wakamwambia, “Tunaweza.”

Kisha Yesu akawaambia, “Mtakinywa kikombe cha mateso ninachokunywa mimi, na mtabatizwa ubatizo[f] ninaobatizwa mimi. 40 Lakini kuhusu kuketi kulia kwangu ama kushoto kwangu siyo mamlaka yangu kusema. Mungu ameandaa nafasi hizo kwa ajili ya wale aliowateuwa.”

41 Wale wanafunzi kumi wengine walipoyasikia maombi haya, waliwakasirikia Yakobo na Yohana. 42 Na Yesu akawaita wale wanafunzi kumi na kusema, “Mnajua kuwa miongoni mwa mataifa watawala huwa na mamlaka makubwa juu ya watu, na viongozi wenye nguvu huwakandamiza watu wao. 43 Haipaswi kuwa hivyo miongoni mwenu. Kwani yeyote atakaye kuwa mkuu miongoni mwenu basi na awe mtumishi wenu. 44 Yeyote anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima akubali kuwa mtumwa wenu wote. 45 Kwani hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa bali alikuja kuwatumikia wengine na kuyatoa maisha yake ili kuwaweka huru wengi.”

Yesu Amponya Asiyeona

(Mt 20:29-34; Lk 18:35-43)

46 Kisha wakafika Yeriko. Yesu alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati wa watu, Bartimayo mwana wa Timayo, ombaomba asiyeona, alikuwa amekaa kando ya barabara. 47 Aliposikia kwamba huyo alikuwa ni Yesu wa Nazareti, alianza kupiga kelele na kusema, “Yesu Mwana wa Daudi, unihurumie!”

48 Na watu wengi walimkemea na kumwambia anyamaze kimya. Lakini yeye alipiga kelele kwa sauti kubwa zaidi na kusema, “Mwana wa Daudi, unihurumie!”

49 Kwa hiyo Yesu akasimama na kusema, “Hebu mwiteni.”

Nao wakamwita yule mtu asiyeona na kumweleza, “Jipe moyo mkuu! Inuka! Yesu anakuita.” 50 Naye akalitupa joho lake, akaruka juu, na akamwendea Yesu.

51 Naye Yesu akamwambia, “Unataka nikufanyie nini?”

Yule mtu asiyeona akamwambia, “Mwalimu, nataka kuona tena.”

52 Hivyo Yesu akamwambia, “Nenda! Imani yako imekuponya.”[g] Na mara akaweza kuona tena, na akamfuata Yesu barabarani.

Footnotes

  1. 10:4 hati ya kutangua ndoa Ama talaka 24:1.
  2. 10:12 atamtaliki Ama kumwacha yaani kutoa talaka. Pia kutaliki ni kutoa talaka, ambayo ni kuandika hati ya kutangua ndoa (tazama mstari 4 hapo juu).
  3. 10:12 zinaa Zinaa ni Kuvunja ahadi ya ndoa kwa kufanya dhambi ya mtu kulala na mtu mwingine asiye mume ama mkewe wa ndoa.
  4. 10:24 vigumu Baadhi ya nakala za zamani za Kiyunani zina “vigumu kwa wale walioweka matumaini yao kwenye utajiri”.
  5. 10:38 kikombe Kikombe ni ishara ya mateso. Yesu alitumia dhana ya kukinywea kikombe akimaanisha kuyakubali mateso ambayo angeyapata katika matukio ya kutisha ambayo yangetokea muda mfupi ujao.
  6. 10:39 ubatizo Neno hili ubatizo lina maana ya kutumbukiza majini, lakini pia lina maana maalumu hapa, ambayo ni kufunikwa, kuwekwa ndani ya ama kufunikwa au kuzikwa mwili wote.
  7. 10:52 imekuponya Kiyunani kinatumia neno hilo hilo kuwa na maana ya neno kuponya na kumaanisha kuokoa.