Add parallel Print Page Options

Petro na Kornelio

10 Kulikuwa mtu aliyeitwa Kornelio katika mji wa Kaisaria. Mtu huyu alikuwa ofisa wa kikosi kilichoitwa “Kikosi cha Kiitalia” katika jeshi la Rumi. Alikuwa mcha Mungu. Yeye na watu wengine wote walioishi katika nyumba yake walikuwa wanamwabudu Mungu wa kweli. Alitoa pesa zake nyingi kuwasaidia maskini miongoni mwa Wayahudi na daima alimwomba Mungu kwa kufuata utaratibu kama ilivyokuwa. Mchana mmoja yapata saa tisa, kwa uwazi na dhahiri Kornelio aliona maono. Alimwona malaika kutoka kwa Mungu akimwendea na akamwambia, “Kornelio!”

Akiwa anashangaa na kuogopa, Kornelio akasema, “Unataka nini, bwana?”

Malaika akamwambia, “Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako unazowapa maskini. Anakukumbuka kwa yote uliyotenda. Tuma baadhi ya watu sasa waende katika mji wa Yafa wakamlete mtu anayeitwa Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. Anakaa kwa mtu ambaye naye pia anaitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko kwenye ufukwe wa bahari.” Malaika aliyeongea na Kornelio akaondoka. Ndipo Kornelio aliita watumishi wake wawili na askari mmoja. Askari alikuwa mcha Mungu, mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. Kornelio akawaelekeza kila kitu watu hawa watatu kisha akawatuma kwenda Yafa.

Siku iliyofuata wakati wa adhuhuri walipokuwa wanaukaribia mji wa Yafa, Petro alipanda juu ya paa[a] kuomba. 10 Alihisi njaa na akataka chakula. Lakini walipokuwa wanamwandalia chakula ili ale, aliona maono. 11 Aliona mbingu zikifunguka na kitu kama shuka kubwa kikishushwa chini kutoka mbinguni kwa pembe nne. 12 Ndani yake mlikuwa aina zote za wanyama, watambaao na ndege. 13 Kisha sauti ikamwambia, “Petro simama uchinje chochote hapa kisha ule.”

14 Lakini Petro akasema, “Siwezi kufanya hivyo, Bwana! Sijawahi kula kitu chochote kisicho safi au kisicho stahili kutumiwa kwa chakula.”

15 Lakini sauti ikamwambia tena, “Mungu amekwisha vitakasa vitu vyote hivi. Usiseme havistahili kuliwa.” 16 Hili lilimtokea mara tatu. Kisha likachukuliwa mbinguni. 17 Petro alijiuliza maono haya yalikuwa na maana gani.

Watu ambao Kornelio aliwatuma walishaiona nyumba ya Simoni na walikuwa wamesimama mlangoni. 18 Waliuliza, “Je, Simoni Petro yuko hapa?”

19 Petro akiwa bado anafikiri kuhusu maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Sikiliza, kuna watu watatu wanakutafuta. 20 Inuka na ushuke chini. Nenda nao, usisite, kwa sababu nimewatuma.” 21 Hivyo Petro akashuka chini na kuwaambia, “Nafikiri mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja hapa?”

22 Wale watu wakasema, “Malaika mtakatifu amemwambia Kornelio akualike nyumbani mwake. Ni mtu mwema na hutenda kwa haki, na anamwabudu Mungu na Wayahudi wote wanamheshimu. Malaika alimwambia akualike nyumbani kwake ili asikilize yale utakayosema.” 23 Petro akawakaribisha ndani watu wale ili walale usiku huo.

Siku iliyofuata Petro alijiandaa na kuondoka na wale watu watatu. Baadhi ya waamini katika mji wa Yafa walikwenda pamoja naye. 24 Siku iliyofuata walifika katika mji wa Kaisaria. Kornelio alikuwa anawasubiri na alikuwa amewakusanya jamaa na rafiki zake wa karibu nyumbani mwake.

25 Petro alipoingia ndani ya nyumba, Kornelio alimlaki kisha akaanguka miguuni kwa Petro na akamwabudu. 26 Lakini Petro akamwambia asimame. Petro akasema, “Simama! Mimi ni mtu tu kama wewe.” 27 Petro aliendelea kuzungumza na Kornelio. Ndipo Petro akaingia ndani na kuona kundi kubwa la watu wamekusanyika pale.

28 Petro akawaambia watu wale kuwa, “Mnaelewa kuwa ni kinyume na sheria yetu kwa Myahudi kushirikiana au kumtembelea mtu ambaye si Myahudi. Lakini Mungu amenionyesha kuwa nisimchukulie mtu yeyote kuwa yu kinyume na desturi za Kiyahudi. 29 Ndiyo sababu sikubisha watu wenu waliponiambia kuja hapa. Sasa, tafadhali niambieni kwa nini mmeniita hapa.”

30 Kornelio akasema, “Siku nne zilizopita, kama saa tisa mchana nilikuwa ninaomba ndani ya nyumba yangu. Ghafla akawepo mtu mmoja amesimama mbele yangu amevaa mavazi meupe yanayong'aa. 31 Akasema, ‘Kornelio, Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako kwa maskini. Anakukumbuka wewe na yote uliyofanya. 32 Hivyo tuma baadhi ya watu kwenye mji wa Yafa na wamwambie Simoni Petro kuja. Anakaa na mtu mwingine anayeitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko pembeni mwa bahari.’ 33 Hivyo nikawatuma kwako haraka. Imekuwa vizuri sana umekuja hapa. Sasa sote tupo hapa mbele za Mungu na tuko tayari kusikia kila kitu ambacho Bwana amekwamuru utuambie.”

Petro Ahubiri Katika nyumba ya Kornelio

34 Petro akaanza kwa kusema: “Hakika sasa ninaelewa ni kwa nini Mungu hawachukulii kundi fulani la watu kuwa bora kuliko wengine. 35 Anamkubali yeyote anayemwabudu na anayetenda haki. Haijalishi wanatoka katika taifa lipi. 36 Mungu amezungumza na watu wa Israeli. Aliwaletea Habari Njema kwamba amani imekuja kupitia Yesu Kristo ambaye ndiye Bwana wa watu wote.

37 Mnafahanu kilichotokea katika Uyahudi yote. Kilianzia Galilaya baada ya Yohana kuwaambia watu kuwa inawapasa kubatizwa. 38 Mnajua kuhusu Yesu kutoka Nazareti. Mungu alimfanya Masihi kwa kumpa Roho Mtakatifu na nguvu. Yesu alikwenda kila mahali akiwatendea mema watu. Akawaponya wale waliokuwa wakitawaliwa na yule Mwovu, akionyesha kuwa Mungu alikuwa pamoja naye.

39 Tuliona yote ambayo Yesu alitenda katika Uyahudi na katika mji wa Yerusalemu. Lakini aliuawa. Walimpigilia kwenye msalaba uliotengenezwa kwa mti. 40 Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, Mungu alimfufua na kumfanya aonekane wazi wazi. 41 Hakuonekana kwa Wayahudi wote, lakini alionekana kwetu sisi tu, ambao Mungu tayari alikwisha kutuchagua tuwe mashahidi. Tulikula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu.

42 Yesu alitwambia twende na kuwaeleza watu. Alituagiza tuwaeleza kwamba yeye ndiye ambaye Mungu amemchagua kuwa mwamuzi wa wote walio hai na wote walio kufa. 43 Na ya kwamba kila atakayemwamini Yesu, atasamehewa dhambi zake kupitia nguvu jina Lake. Manabii wote wanakubali kuwa jambo hili ni la kweli.”

Roho Mtakatifu Awashukia Watu Wasio Wayahudi

44 Petro alipokuwa bado anazungumza, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanamsikiliza. 45 Waamini wa Kiyahudi waliofuatana na Petro walishangaa kwamba Roho Mtakatifu amemiminwa kama zawadi hata kwa watu wasio Wayahudi. 46 Waliwasikia wakiongea lugha mbalimbali na kumsifu Mungu. Ndipo Petro akasema, 47 “Je, mtu yeyote anawezaje kuzuia watu hawa wasibatizwe katika maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea!” 48 Hivyo Petro akawaambia wambatize Kornelio pamoja na jamaa zake na rafiki zake katika jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba Petro akae nao kwa siku chache.

Footnotes

  1. 10:9 paa Nyakati za Biblia, nyumba zilikuwa na paa zilizosawa kama sakafu, zilizotumika kama vyumba vya ziada au sehemu za kufanyia mazungumzo.