Add parallel Print Page Options

Barnaba na Sauli Wapewa Kazi Maalum

13 Walikuwepo baadhi ya manabii na walimu katika kanisa la Antiokia. Walikuwa Barnaba, Simeoni (ambaye pia aliitwa Nigeri[a]), Lukio (kutoka mji wa Kirene), Manaeni (aliyekua pamoja na Mfalme Herode[b]), na Sauli. Watu hawa wote kwa pamoja walikuwa wanamwabudu Bwana na wamefunga Roho Mtakatifu alipowaambia, “Nitengeeni Barnaba na Sauli ili wanifanyie kazi maalumu. Wao ndio niliowachagua kuifanya kazi hiyo.”

Hivyo kanisa lilifunga na kuomba. Wakaweka mikono yao juu ya Barnaba na Sauli, wakaagana nao na kuwaacha waende.

Barnaba na Sauli Wakiwa Kipro

Barnaba na Sauli walitumwa na Roho Mtakatifu. Walikwenda katika mji wa Seleukia. Kutoka hapo walitweka tanga na kusafiri mpaka kwenye kisiwa cha Kipro. Barnaba na Sauli walipofika kwenye mji wa Salami, walihubiri ujumbe wa Mungu katika masinagogi ya Kiyahudi. Yohana ambaye pia anaitwa Marko alikuwa pamoja nao ili kuwasaidia.

Walisafiri wakitisha kisiwa chote mpaka kwenye mji wa Pafo. Huko walimkuta mwanaume wa Kiyahudi aliyeitwa Bar-Yesu aliyekuwa akifanya uchawi. Alikuwa nabii wa uongo. Alikaa daima karibu na Sergio Paulo, aliyekuwa gavana na mtu makini sana. Sergio Paulo aliwaalika Barnaba na Sauli waende kumtembelea kwa sababu alitaka kusikia ujumbe wa Mungu. Lakini mchawi Elima (Bar-Yesu kama alivyoitwa kwa Kiyunani) alizungumza kinyume nao ili kuwapinga, akijaribu kumzuia gavana asimwamini Yesu. Kisha Sauli (ambaye pia anajulikana kama Paulo), akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkazia macho Elima 10 na kusema, “Ewe mwana wa Ibilisi, uliyejaa uongo na aina zote za hila za uovu! Wewe ni adui wa kila kilicho cha kweli. Hautaacha kuzibadili kweli za Bwana kuwa uongo? 11 Sasa Bwana atakugusa na utakuwa asiyeona. Hautaweza kuona kitu chochote kwa muda, hata mwanga wa jua.”

Ndipo kila kitu kikawa giza kwa Elima. Akazunguka kila mahali na akapotea. Alikwenda kila mahali akijaribu kumpata mtu wa kumshika mkono ili amwongoze. 12 Gavana alipoyaona haya, akaamini. Akayashangaa mafundisho kuhusu Bwana.

Paulo na Barnaba Waenda Antiokia ya Pisidia

13 Paulo na watu waliokuwa pamoja naye walitweka tanga na kusafiri kwa merikebu kutoka Pafo mpaka Perge, mji uliokuwa Pamfilia. Hapo Yohana Marko aliwaacha na akarudi Yerusalemu. 14 Waliendelea na safari yao kutoka Perge na kwenda Antiokia, mji karibu na Pisidia.

Siku ya Sabato walikwenda katika sinagogi la Kiyahudi na kuketi chini. 15 Sheria ya Musa na maandishi ya manabii vilisomwa. Kisha viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe Paulo na Barnaba, wakisema, “Ndugu zetu, ikiwa mna kitu chochote cha kusema kitakachowasaidia watu hapa, tafadhali semeni.”

16 Paulo akasimama, akanyoosha mkono wake ili wamsikilize, akasema, “Watu wa Israeli nanyi nyote msio Wayahudi mnaomwabudu Mungu wa kweli, tafadhali nisikilizeni! 17 Mungu wa Israeli aliwachagua baba zetu. Na watu wetu walipoishi Misri kama wageni, aliwafanya wakuu. Kisha akawatoa katika nchi ile kwa nguvu kuu. 18 Aliwavumilia kwa miaka arobaini walipokuwa jangwani. 19 Mungu aliangamiza mataifa saba katika nchi ya Kanaani na kuwapa nchi yao watu wake. 20 Yote haya yalitokea katika kipindi cha kadiri ya miaka mia nne na hamsini.[c]

Baada ya hili, Mungu akawapa watu wetu waamuzi kuwaongoza mpaka wakati wa nabii Samweli. 21 Ndipo watu wakaomba kuwa na mfalme. Mungu akawapa Sauli, mwana wa Kishi. Sauli alitoka katika kabila la Benjamini. Alikuwa mfalme kwa miaka arobaini. 22 Baada ya Mungu kumwondoa Sauli katika ufalme, Mungu alimfanya Daudi kuwa Mfalme wao. Hiki ndicho Mungu alisema kuhusu Daudi: ‘Daudi, mwana wa Yese, ni mtu ambaye Mimi mwenyewe nimemchagua. Atafanya kila kitu nitakachotaka afanye.’

23 Kama alivyoahidi, Mungu amemleta mmoja wa wazao wa Daudi katika Israeli ili awe Mwokozi wao, mzao huyo wa Daudi ni Yesu. 24 Kabla Yesu hajaja, Yohana aliwaambia watu wote wa Israeli wanachopaswa kufanya. Waliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa walitaka kubadili maisha yao. 25 Yohana alipokuwa anamaliza kazi yake, alisema, ‘Mnadhani mimi ni nani? Mimi siyo Masihi.[d] Masihi atakuja baadaye, nami sistahili kuwa mtumwa wake wa kufungua kamba za viatu vyake.’

26 Ndugu zangu, wana katika familia ya Ibrahimu na ninyi watu wengine ambao pia mnamwabudu Mungu wa kweli, sikilizeni! Habari kuhusu wokovu huu imeletwa kwetu. 27 Wayahudi waishio Yerusalemu na viongozi wao hawakutambua kuwa Yesu ni Mwokozi. Maneno ambayo manabii waliandika kuhusu yeye yalikuwa yakisomwa kila siku ya Sabato, lakini hawakuyaelewa. Walimhukumu Yesu. Walipofanya hivi, waliyatimiliza maneno ya manabii. 28 Hawakupata sababu ya msingi kwa nini Yesu afe, lakini walimwomba Pilato amwue.

29 Wayahudi hawa walimtendea Yesu mambo yote mabaya ambayo Maandiko yalisema yangempata Yesu. Kisha walimteremsha Yesu kutoka msalabani na kumweka kaburini. 30 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu! 31 Baada ya hili, kwa siku nyingi, wale waliofuatana na Yesu kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu walimwona. Wao sasa ni mashahidi wake kwa watu wetu.

32 Tunawahubiri Habari Njema kuhusu ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu. 33 Sisi ni wazao wao, na Mungu ameitimiza ahadi hii kwa ajili yetu. Mungu aliitimiza ahadi hii kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Tunasoma pia kuhusu hili katika Zaburi 2:

‘Wewe ni Mwanangu.
    Leo nimekuwa baba yako.’(A)

34 Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Yesu hatarudi kaburini na kuwa mavumbi. Hivyo Mungu alisema,

‘Nitawapa ahadi ya kuaminiwa na
    takatifu niliyoiahidi kwa Daudi.’(B)

35 Lakini Zaburi nyingine inasema,

‘Hautaruhusu Mtakatifu wako aoze kaburini.’(C)

36 Daudi aliyatenda mapenzi ya Mungu alipokuwa hai. Kisha alikufa na kuzikwa kama baba zake wote. Na mwili wake ulioza kaburini! 37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuoza kaburini. 38-39 Ndugu zangu, eleweni yale tunayowaambia. Mnaweza kupata msamaha wa dhambi kupitia huyu Yesu. Sheria ya Musa haikuwatoa kutoka katika dhambi zenu. Lakini mnaweza kuwa huru mbali na hukumu. 40 Hivyo iweni waangalifu! Msiruhusu walichosema manabii kikawatokea ninyi:

41 ‘Sikilizeni enyi watu wenye mashaka!
    Mnaweza kushangaa,
    lakini sasa nendeni na mfe.
Kwa sababu kipindi cha wakati wenu,
    nitafanya kitu ambacho hamtaamini.
Hata kama kitafafanuliwa kwenu!’”(D)

42 Paulo na Barnaba walipokuwa wanaondoka kwenye sinagogi, watu waliwaomba warudi tena Sabato inayofuata ili wawaeleze zaidi kuhusu mambo haya. 43 Baada ya mkutano, watu wengi, Wayahudi na wale waliobadili dini zao na kufuata dini ya Kiyahudi, waliwafuata Paulo na Barnaba; nao waliwatia moyo watu hawa waendelee kuitumaini neema ya Mungu.

44 Siku ya Sabato iliyofuata, karibu watu wote katika mji walikusanyika ili wasikie neno la Bwana. 45 Wayahudi waliokuwepo pale walipowaona watu wote hawa, wakaingiwa na wivu sana. Wakakashifu na kubishia kila kitu alichosema Paulo. 46 Lakini Paulo na Barnaba walihubiri kwa ujasiri. Walisema, “Tulikuwa tuuhubiri ujumbe wa Mungu kwenu ninyi Wayahudi kwanza, lakini mmekataa kusikiliza. Mmeweka wazi kuwa hamstahili kuupata uzima wa milele. Hivyo tutakwenda sasa kwa wale wasio Wayahudi. 47 Hivi ndivyo Bwana alivyotuambia kufanya:

‘Nimewafanya ninyi mwanga kwa ajili ya mataifa mengine,
    kuwaonesha watu ulimwenguni kote njia ya wokovu.’”(E)

48 Wasio Wayahudi waliposikia Paulo akisema hivi, walifurahi sana. Waliuheshimu ujumbe wa Bwana, na wengi wao wakauamini. Hawa ni wale waliochaguliwa kuupata uzima wa milele.

49 Na hivyo ujumbe wa Bwana ulihubiriwa katika nchi yote. 50 Lakini Wayahudi pale walisababisha baadhi ya wanawake muhimu waifuatayo dini na viongozi wa mji kuwakasirikia na kuwachukia Paulo na Barnaba na wakawafukuza mjini. 51 Hivyo Paulo na Barnaba wakakung'uta mavumbi ya miguu yao.[e] Kisha wakaenda katika mji wa Ikonia. 52 Lakini wafuasi wa Bwana katika Antiokia walijaa furaha na walijazwa Roho Mtakatifu.

Footnotes

  1. 13:1 Nigeri Ni neno la Kilatini linalomaanisha weusi au nyeusi.
  2. 13:1 Herode Huyu ni Herode Antipa, mwana wa Herode Mkuu. Huyu ni Herode wa nne. Baada ya Herode Mkuu kufa, ufalme wake uligawanywa kwa wanaye wanne. Tazama Herode katika Orodha ya Maneno.
  3. 13:20 miaka mia nne na hamsini Yaani miaka 400 ya kuishi Misri, miaka 40 ya kusafiri jangwani na miaka 10 ya kuteka nchi.
  4. 13:25 Masihi Kwa maana ya kawaida, “Mimi” (yaani, “yeye” au “Yule anayestahili”), Hii inamaanisha yule aliyechaguliwa na kutumwa na Mungu. Linganisha na Yh 1:20. Tazama Masihi katika Orodha ya Maneno.
  5. 13:51 wakakung'uta … yao Ilionesha kuwa walimaliza kuzungumza na watu hawa.