Add parallel Print Page Options

Timotheo Afuatana na Paulo na Sila

16 Paulo alikwenda Derbe kisha Listra, ambako mfuasi wa Yesu aliyeitwa Timotheo aliishi. Mamaye Timotheo alikuwa mwamini wa Kiyahudi, lakini baba yake alikuwa Myunani. Waamini katika miji ya Listra na Ikonia walimsifu Timotheo kwa mambo mema. Paulo alitaka kusafiri pamoja na Timotheo, lakini Wayahudi wote walioishi katika eneo lile walijua kuwa baba yake alikuwa Myunani. Hivyo ikamlazimu Paulo amtahiri Timotheo ili kuwaridhisha Wayahudi.

Kisha Paulo na wale waliokuwa pamoja naye wakasafiri kupitia miji mingine. Wakawapa waamini kanuni na maamuzi yaliyofikiwa na mitume na wazee wa Yerusalemu. Wakawaambia wazitii kanuni hizo. Hivyo makanisa yakawa yanaongezeka katika imani, na idadi ya waamini iliongezeka kila siku.

Paulo Aitwa Makedonia

Paulo na wale waliokuwa pamoja naye walisafiri kwa kupita katika maeneo ya Frigia na Galatia kwa sababu Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuzihubiri Habari Njema katika jimbo la Asia. Walipofika kwenye mpaka wa Misia, walijaribu kwenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu kwenda huko. Hivyo wakapita Misia na kwenda katika mji wa Troa.

Usiku ule Paulo aliona maono kwamba mtu kutoka Makedonia alimjia Paulo. Mtu huyo alisimama mbele yake na kumsihi akisema, “Vuka njoo Makedonia utusaidie.” 10 Baada ya Paulo kuona maono yale, tulijiandaa[a] haraka na tukaondoka kwenda Makedonia. Tulielewa kuwa Mungu ametuita ili tukahubiri Habari Njema huko Makedonia.

Kuongoka kwa Lydia

11 Tulisafiri kwa merikebu kutoka Troa na tukaabili kwenda katika kisiwa cha Samothrake. Siku iliyofuata tukasafiri kwenda katika mji wa Neapoli. 12 Kisha tulisafiri kwa nchi kavu mpaka Filipi, koloni la Rumi na mji maarufu katika la Makedonia. Tulikaa pale kwa siku chache.

13 Siku ya Sabato tulikwenda mtoni, nje ya lango la mji. Tulidhani tungepata mahali ambapo Wayahudi hukutana mara kwa mara kwa ajili ya kuomba. Baadhi ya wanawake walikuwa wamekusanyika huko, na hivyo tulikaa chini na kuzungumza nao. 14 Miongoni mwao alikuwepo mwanamke aliyeitwa Lydia kutoka katika mji wa Thiatira. Alikuwa mwuza rangi ya zambarau. Alikuwa mwabudu Mungu wa kweli. Lydia alimsikiliza Paulo, na Bwana akaufungua moyo wake kuyakubali yale Paulo alikuwa anasema. 15 Yeye na watu wote waliokuwa wakiishi katika nyumba yake walibatizwa. Kisha akatualika nyumbani mwake. Alisema, “Ikiwa mnaona mimi ni mwamini wa kweli wa Bwana Yesu, njooni mkae nyumbani mwangu.” Alitushawishi tukae nyumbani mwake.

Paulo na Sila Wakiwa Gerezani

16 Siku moja tulipokuwa tunakwenda pale mahali pa kufanyia kuomba, mtumishi mmoja msichana alikutana nasi. Msichana huyu alikuwa na roho ya ubashiri[b] ndani yake iliyompa uwezo wa kutabiri mambo yatakayotokea baadaye. Kwa kufanya hivi alipata fedha nyingi kwa ajili ya waliokuwa wanammiliki. 17 Akaanza kumfuata Paulo na sisi sote kila mahali akipaza sauti na kusema, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu! Wanawaambia mnavyoweza kuokolewa!” 18 Aliendelea kufanya hivi kwa siku kadhaa na ikamuudhi Paulo, akageuka na kumkemea yule roho akisema, “Kwa uwezo wa Yesu Kristo, ninakuamuru utoke ndani yake!” Mara ile roho chafu ikamtoka.

19 Wamiliki wa mtumishi yule msichana walipoona hili, wakatambua kuwa hawataweza kumtumia tena ili kupata pesa. Hivyo wakawakamata Paulo na Sila na kuwaburuta mpaka kwa watawala. 20 Wakawaleta Paulo na Sila mbele ya maofisa wa Kirumi na kusema, “Watu hawa ni Wayahudi, wanafanya vurugu katika mji wetu. 21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Rumi haturuhusiwi kuzifuata wala kutenda.”

22 Umati wote wa watu ukawa kinyume na Paulo na Sila. Maofisa wakawachania nguo Paulo na Sila na wakaamuru wapigwe bakora. 23 Walichapwa sana kisha wakawekwa gerezani. Maofisa wakamwambia mkuu wa gereza, “Walinde watu hawa kwa umakini!” 24 Mkuu wa gereza aliposikia amri hii maalumu, aliwaweka Paulo na Sila ndani zaidi gerezani na kuwafunga miguu yao kwenye nguzo kubwa za miti.

25 Usiku wa manane Paulo na Sila walipokuwa wakiomba na kumwimbia Mungu nyimbo za sifa, wafungwa wengine wakiwa wanawasikiliza. 26 Ghafla kulitokea tetemeko kubwa lililotikisa msingi wa gereza. Milango yote ya gereza ilifunguka, na minyororo waliyofungwa wafungwa wote ikadondoka. 27 Mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza imefunguliwa. Alidhani wafungwa wametoroka, hivyo alichukua upanga wake ili ajiue.[c] 28 Lakini Paulo alipaza sauti akamwambia, “Usijidhuru! Sote tuko hapa!”

29 Mkuu wa gereza akaagiza aletewe taa. Kisha akakimbia kuingia ndani, akitetemeka kwa woga, akaanguka mbele ya Paulo na Sila. 30 Kisha akawatoa nje na kusema, “Nifanye nini ili niokoke?”

31 Wakamwambia, “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokolewa pamoja na watu wote waishio katika nyumba yako.” 32 Hivyo Paulo na Sila wakamhubiri ujumbe wa Bwana mkuu wa gereza na watu wote walioishi katika nyumba yake. 33 Ilikuwa usiku sana, lakini mkuu wa gereza aliwachukua Paulo na Sila na akawaosha majeraha yao. Kisha mkuu wa gereza na watu wote katika nyumba yake wakabatizwa. 34 Baada ya hili mkuu wa gereza akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake akawapa chakula. Watu wote walifurahi kwa sababu sasa walikuwa wanamwamini Mungu.

35 Asubuhi iliyofuata maofisa wa Kirumi waliwatuma baadhi ya askari kwenda gerezani na wakamwambia mkuu wa gereza, “Waachie watu hawa huru.”

36 Mkuu wa gereza akamwambia Paulo, “Maofisa wamewatuma askari hawa ili kuwaachia huru. Mnaweza kuondoka sasa. Nendeni kwa amani.”

37 Lakini Paulo akawaambia askari, “Wale maofisa hawakuthibitisha kuwa tulifanya chochote kibaya, lakini walitupiga kwa bakora hadharani na kutuweka gerezani. Nasi ni raia wa Rumi.[d] Na sasa wanataka tuondoke kimya kimya. Haiwezekani, ni lazima waje hapa wao wenyewe kisha watutoe nje!”

38 Askari wakawaambia maofisa alichosema Paulo. Waliposikia kwamba Paulo na Sila ni raia wa Rumi, waliogopa. 39 Hivyo walikwenda gerezani kuwaomba msamaha. Waliwatoa nje ya gereza na kuwaomba waondoke mjini. 40 Lakini Paulo na Sila walipotoka gerezani, walikwenda nyumbani kwa Lydia. Wakawaona baadhi ya waamini pale, wakawatia moyo. Kisha wakaondoka.

Footnotes

  1. 16:10 tulijiandaa Luka, mwandishi wa kitabu hiki alisafiri pamoja na Paulo kwenda Makedonia lakini alibaki Filipi, Paulo alipoondoka. (Tazama mstari wa 40.) Kiwakilishi cha kwanza cha nafsi kinatokea tena katika Mdo 20:5-21:18 na 27:1-28.
  2. 16:16 roho ya ubashiri Roho chafu kutoka kwa mwovu inayomwezesha mtu kuwa na ujuzi au utambuzi. Iliamika kuwa watu waliokuwa na roho hii waliipata kutoka kwa Appollo mungu wa Wayunani (Wagiriki).
  3. 16:27 ajiue Alijua viongozi wake wangemwua kwa kudhani kuwa alizembea na wafungwa wametoroka.
  4. 16:37 raia wa Rumi Sheria ya Kirumi ilisema kuwa raia yeyote wa Rumi hapaswi kupigwa kabla ya kuendesha kesi na kutolewa hukumu.