Add parallel Print Page Options

Paulo Aenda Makedonia na Uyunani

20 Ghasia zilipokwisha, Paulo aliwaalika wafuasi wa Bwana kuja kumtembelea. Baada ya kuwatia moyo, aliwaaga na kuondoka kwenda Makedonia. Katika safari yake kupitia Makedonia alikuwa na maneno mengi ya kuwatia moyo wafuasi sehemu mbalimbali. Kisha alikwenda Uyunani na alikaa huko kwa miezi mitatu.

Alipokuwa tayari kutweka tanga kwenda Shamu, baadhi ya Wayahudi walikuwa wanapanga kitu kinyume naye. Hivyo aliamua kurudi nyuma kwenda Shamu kupitia Makedonia. Watu hawa walikuwa wanasafiri pamoja naye: Sopata, mwana wa Piro, kutoka mji wa Berea; Aristarko na Sekundo, kutoka mji wa Thesalonike; Gayo, kutoka mji wa Derbe; Timotheo; na watu wawili kutoka Asia, Tikiko na Trofimo. Watu hawa walimtangulia Paulo. Walitusubiri katika mji wa Troa. Baada ya Siku kuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu tulitweka tanga kutoka katika mji wa Filipi. Tuliwakuta watu hawa katika mji wa Troa siku tano baadaye na tulikaa pale kwa siku saba.

Paulo Atembelea Troa Mara ya Mwisho

Siku ya Jumapili[a] sote tulikusanyika pamoja kula Meza ya Bwana.[b] Paulo alizungumza na kundi. Kwa sababu alipanga kuondoka siku iliyofuata, aliendelea kuzungumza mpaka usiku wa manane. Tulikuwa wote kwenye chumba ghorofani na kulikuwa taa nyingi chumbani. Alikuwepo kijana mmoja aliyekuwa amekaa dirishani aliyeitwa Eutiko. Paulo aliendelea kuzungumza, na Eutiko alianza kuchoka na kusikia ungungizi. Mwishowe alisinzia na kuanguka. Alianguka chini, nje kutoka ghorofa ya tatu. Watu walipokwenda kumnyenyua alikuwa amekwisha kufa.

10 Paulo alishuka, akaenda mahali alipokuwa Eutiko, akapiga magoti, na akamkumbatia. Akawaambia waamini wengine, “Msiwe na hofu. Ni mzima yuko hai sasa.” 11 Kisha Paulo akapanda ghorofani, akamega baadhi ya mikate na kula. Alizungumza nao kwa muda mrefu. Alimaliza kuzungumza mapema asubuhi na akaondoka. 12 Wafuasi wa Bwana walimpeleka Eutiko nyumbani akiwa hai, walifarijika sana wote.

Safari Kutoka Troa kwenda Mileto

13 Tulimtangulia Paulo, tukatweka tanga kwenda Asso, tulipanga kumkuta huko. Alitwambia tufanye hivi kwa sababu alitaka kusafiri kwa nchi kavu. 14 Alipotukuta Asso, aliungana nasi na tulipanda meli pamoja naye, na sote tulitweka tanga kwenda Mitelene. 15 Siku iliyofuata, tulitweka tanga kutoka pale na kufika karibu na kisiwa cha Kio. Kisha siku iliyofuata tulitweka tanga kwenda kwenye kisiwa Samosi. Baada ya siku moja tukafika kwenye mji wa Mileto. 16 Paulo alikwisha amua kutosimama Efeso. Hakutaka kukaa Asia kwa muda mrefu. Alikuwa anaharakisha kwa sababu alitaka ikiwezekana awe Yerusalemu siku ya Pentekoste.

Paulo Azungumza na Wazee kutoka Efeso

17 Tukiwa Mileto Paulo alitume ujumbe kwenda Efeso, akiwaambia wazee wa kanisa la Efeso waje kwake.

18 Walipofika, Paulo akawaambia, “Mnafahamu kuhusu maisha yangu tangu siku ya kwanza nilipofika Asia. Mnafahamu namna nilivyoishi wakati wote nilipokuwa pamoja nanyi. 19 Wayahudi walipanga hila kinyume nami, na hila zao zilinisababishia matatizo mengi. Lakini mnafahamu kwamba daima nilimtumikia Bwana, nyakati zingine kwa machozi. Sikujipendelea mimi mwenyewe kwanza. 20 Daima niliwatendea mema. Niliwahubiri Habari Njema kuhusu Yesu sehemu za wazi mbele ya watu na pia nilifundisha katika nyumba zenu. 21 Nilimwambia kila mtu, Myahudi na Myunani, kubadilika na wakamgeukia Mungu. Niliwaambia wote wamwamini Bwana wetu Yesu.

22 Lakini sasa ni lazima nimtii Roho na kwenda Yerusalemu. Sifahamu nini kitanipata huko. 23 Ninafahamu kitu kimoja kwamba katika kila mji Roho Mtakatifu huniambia kwamba matatizo na hata kufungwa gerezani kunanisubiri. 24 Siujali uhai wangu mwenyewe. Jambo la muhimu zaidi ni mimi kuimaliza kazi yangu. Ninataka niimalize huduma ambayo Bwana Yesu alinipa niifanye, nayo ni kuwahubiri watu Habari Njema kuhusu neema ya Mungu.

25 Na sasa nisikilizeni. Ninafahamu kwamba hakuna mmoja wenu atakayeniona tena. Wakati wote nilipokuwa pamoja nanyi, niliwahubiri Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. 26 Hivyo leo ninaweza kuwaambia kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho: Mungu hatanilaumu ikiwa baadhi yenu hamtaokoka. 27 Ninaweza kusema hivi kwa sababu ninajua niliwaambia yote ambayo Mungu anataka mfahamu. 28 Jilindeni ninyi wenyewe pamoja na watu wote mliopewa na Mungu. Naye Roho Mtakatifu amewapa ninyi kazi ya kuwachunga[c] kondoo hawa.[d] Ni lazima muwe wachungaji wa kanisa la Mungu,[e] watu ambao Mungu aliwanunua kwa damu ya Mwanaye wa pekee.[f] 29 Ninafahamu ya kwamba nikishaondoka, baadhi ya watu watakuja kwenye kundi letu. Watakuwa kama mbwa mwitu na watajaribu kuwaangamiza kondoo. 30 Pia, watu kutoka kwenye kundi lenu wenyewe wataanza kufundisha mambo yasiyo sahihi. Watawaongoza baadhi ya wafuasi wa Bwana mbali na kweli ili wawafuate katika upotovu wao. 31 Hivyo iweni waangalifu! Na daima kumbukeni mambo niliyofanya kwa miaka mitatu nilipokuwa pamoja nanyi. Sikuacha kumkumbusha kila mmoja wenu jinsi anavyopaswa kuishi, nikiwashauri usiku na mchana na kulia kwa ajili yenu.

32 Sasa ninawaweka katika uangalizi wa Mungu. Ninategemea ujumbe wa neema yake kuwaimarisha ninyi. Ujumbe huo unaweza kuwapa ninyi baraka ambazo Mungu huwapa watakatifu wake wote. 33 Nilipokuwa pamoja nanyi, sikutamani pesa ya mtu yeyote au nguo nzuri. 34 Mnafahamu kwamba daima nilifanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe ili nimudu mahitaji yangu mwenyewe na mahitaji ya watu waliokuwa pamoja nami. 35 Daima niliwaonesha kwamba mnapaswa kufanya kazi nilivyofanya na kuwasaidia wadhaifu. Niliwafundisha kukumbuka maneno ya Bwana Yesu aliyosema, ‘Ni baraka kuu kutoa kuliko kupokea.’”

36 Paulo alipomaliza kuzungumza, alipiga magoti chini, na wote waliomba pamoja. 37-38 Walilia sana. Kilichowahuzunisha sana ilikuwa kauli ya Paulo alipowaambia kuwa hawatamwona tena. Walimkumbatia na kumbusu. Kisha walikwenda pamoja naye mpaka kwenye meli na wakaagana naye.

Footnotes

  1. 20:7 Jumapili Kwa maana ya kawaida, “siku ya kwanza ya juma”, ambayo kwa Wayahudi ilianza machweo ya jua siku ya Jumamosi. Lakini ikiwa mwandishi (Luka) anatumia kalenda ya Kiyunani hapa, basi mkutano huu ulifanyika Jumapili usiku.
  2. 20:7 kula Meza ya Bwana Kwa maana ya kawaida, “kuumega mkate”. Hii inaweza kumaanisha mlo au Meza ya Bwana, mlo maalumu ambao Yesu aliwaambia wafuasi wake kula kwa ajili ya kumkumbuka Yeye. Tazama Lk 22:14-20.
  3. 20:28 amewapa … kuwachunga Kwa maana ya kawaida “Amewafanya kuwa waangalizi wa.”
  4. 20:28 kondoo hawa Hapa limetumika kumaanisha, kundi la watu wa Mungu wanaowafuata viongozi wao kama kondoo anavyomfuata mchungaji.
  5. 20:28 la Mungu Nakala zingine za Kiyunani zina, “la Bwana”.
  6. 20:28 damu ya Mwanaye wa pekee Au “damu yake mwenyewe”.