Add parallel Print Page Options

23 Paulo aliwatazama wajumbe wa baraza na kusema, “Ndugu zangu, Nimeishi maisha yangu katika njia nzuri mbele za Mungu. Daima nimefanya yale niliyodhani ni haki.” Anania,[a] kuhani mkuu alikuwa pale. Aliposikia hili, aliwaambia watu waliokuwa wamesisima karibu na Paulo wampige kwenye mdomo. Paulo akamwambia Anania, “Mungu atakupiga wewe pia! Wewe ni kama ukuta mchafu uliopakwa rangi nyeupe. Umeketi hapa na kunihukumu, ukitumia Sheria ya Musa. Lakini unawaambia wanipige wakati ni kinyume cha sheria.”

Watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Una uhakika unataka kumtukana kuhani mkuu wa Mungu namna hiyo?”

Paulo akasema, “Ndugu zangu, sikufahamu kuwa mtu huyu ni kuhani mkuu. Maandiko yanasema, ‘Usiseme mambo mabaya kuhusu kiongozi wa watu wako.’”(A)

Paulo alijua kuwa baadhi ya watu kwenye baraza lile ni Masadukayo na baadhi yao ni Mafarisayo. Hivyo akapaza sauti akasema, “Ndugu zangu, Mimi ni Farisayo na baba yangu ni Farisayo! Nimeshitakiwa hapa kwa sababu ninaamini kuwa watu watafufuka kutoka kwa wafu.”

Paulo alipolisema hili, mabishano makubwa yakaanza kati ya Mafarisayo na Masadukayo. Baraza likagawanyika. (Masadukayo hawaamini katika ufufuo, malaika au roho. Lakini Mafarisayo wanaamini vyote.) Wayahudi hawa wote wakaanza kubishana kwa kupaza sauti. Baadhi ya walimu wa sheria, waliokuwa Mafarisayo wakasimama na kusema, “Hatuoni kosa lolote kwa mtu huyu. Inawezekana kwa hakika malaika au roho alizungumza naye.”

10 Mabishano yaligeuka kuwa mapigano na kamanda aliogopa kwamba Wayahudi wangempasua Paulo vipande vipande. Hivyo akawaambia askari wateremke, wamwondoe Paulo na kumweka mbali na Wayahudi hao katika jengo la jeshi.

11 Usiku uliofuata Bwana Yesu akaja na kusimama pembeni mwa Paulo. Akamwambia, “Uwe jasiri! Umewaambia watu kuhusu mimi humu Yerusalemu. Ni lazima ufanye vivyo hivyo Rumi.”

Baadhi ya Wayahudi Wapanga Kumwua Paulo

12 Asubuhi iliyofuata baadhi ya Wayahudi walifanya mpango wa kumwua Paulo. Walijiapiza kuwa hawatakula wala kunywa kitu chochote mpaka watakapomwua Paulo. 13 Walikuwa watu zaidi ya 40 waliofanya mpango huu. 14 Walikwenda wakaongea na viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wa Wayahudi. Walisema, “Tumejiwekea nadhiri kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tumemwua Paulo. 15 Tunataka mfanye hivi: Mtumieni kamanda ujumbe kutoka kwenu na baraza kuu. Mwambieni mnamtaka amlete Paulo kwenu. Semeni kwamba mnataka kumwuliza maswali zaidi, tutamwua akiwa njiani kuja hapa.”

16 Lakini mpwaye Paulo aliusikia mpango huu. Alikwenda kwenye jengo la jeshi na kumwambia Paulo. 17 Kisha Paulo akamwita mmoja wa maofisa wa jeshi na kumwambia, “Mchukue huyu kijana kwa kamanda. Ana ujumbe kwa ajili yake.” 18 Hivyo ofisa wa jeshi akampeleka mpwaye Paulo kwa kamanda. Ofisa wa jeshi akasema, “Mfungwa Paulo ameniomba nimlete kijana huyu kwako. Ana kitu cha kukueleza.”

19 Kamanda akamchukua kijana na kwenda naye mahali ambapo wangekuwa peke yao. Kamanda akamwuliza, “Unataka kuniambia nini?”

20 Kijana akasema, “Baadhi ya Wayahudi wameamua kukuomba umpeleke Paulo kwenye mkutano wa baraza lao kesho. Wanataka wewe udhani kuwa wamepanga kumwuliza Paulo maswali zaidi. 21 Lakini usiwaamini! Zaidi ya watu 40 miongoni mwao wamejificha na wanasubiri kumwua. Wote wameweka nadhiri kuwa hawatakula wala kunywa mpaka wamemwua Paulo. Sasa hivi wanasubiri wewe ukubali.”

22 Kamanda akamtoa kijana, akamwambia, “Usimwambie yeyote kuwa umeniambia kuhusu mpango wao.”

Paulo Apelekwa Kaisaria

23 Ndipo Kamanda akawaita maofisa wawili wa jeshi. Akawaambia, “Ninataka baadhi ya watu kwenda Kaisaria. Andaeni askari mia mbili. Pia andaeni askari sabini waendao kwa farasi na mia mbili wa kubeba mikuki. Iweni tayari kuondoka saa tatu usiku. 24 Andaeni baadhi ya farasi kwa ajili ya Paulo kuendesha ili aweze kupelekwa kwa Gavana Feliki salama.” 25 Kamanda aliandika barua kuhusu Paulo. Hivi ndivyo alivyosema:

26 Kutoka kwa Klaudio Lisiasi.

Kwenda kwa Mheshimiwa Gavana Feliki.

Salamu:

27 Baadhi ya Wayahudi walimkamata mtu huyu na walikuwa karibu ya kumwua. Lakini nilipogundua kuwa ni raia wa Rumi, nilikwenda pamoja na askari wangu tukamwokoa. 28 Nilitaka kufahamu kwa nini walikuwa wanamshitaki. Hivyo nikampeleka kwenye mkutano wa baraza lao. 29 Hivi ndivyo nilivyoona: Wayahudi walisema mtu huyu alifanya mambo mabaya. Lakini mashitaka haya yalihusu sheria zao za Kiyahudi, na hakukuwa kosa lolote linaloweza kusababisha kufungwa au kifo. 30 Nimeambiwa kuwa baadhi ya Wayahudi walikuwa wanafanya mpango wa kumwua. Hivyo nimeamua kumleta kwako. Pia nimewaambia Wayahudi hao wakwambie walichonacho dhidi yake.

31 Askari walifanya kile walichoambiwa. Walimchukua Paulo na kumpeleka kwenye mji wa Antipatri usiku ule. 32 Siku iliyofuata askari wa farasi walikwenda na Paulo mpaka Kaisaria, lakini askari wengine na wale wa mikuki walirudi kwenye jengo la jeshi mjini Yerusalemu. 33 Askari wa farasi waliingia Kaisaria, wakampa barua Gavana Feliki, kisha wakamkabidhi Paulo kwake.

34 Gavana akaisoma barua na kumwuliza Paulo, “Unatoka jimbo gani?” Gavana alitambua kuwa Paulo alikuwa anatoka Kilikia. 35 Gavana akasema, “Nitakusikiliza Wayahudi wanaokushitaki watakapokuja hapa pia.” Kisha gavana akaamuru Paulo awekwe kwenye jumba la kifalme. (Jengo hili lilijengwa na Herode.)

Footnotes

  1. 23:2 Anania Si Anania anayetajwa katika Mdo 22:12.