Add parallel Print Page Options

Paulo Aomba Kumwona Kaisari

25 Festo akawa gavana na siku tatu baadaye akasafiri kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria. Viongozi wa makuhani na viongozi maarufu wa Kiyahudi wakatoa mashitaka dhidi ya Paulo mbele ya Festo. Walimwomba Festo awasaidie. Walitaka amrudishe Paulo Yerusalemu kwa sababu walipanga kumwua akiwa njiani. Lakini Festo alijibu, “Hapana, Paulo ataendelea kuwekwa Kaisaria. Nitaenda huko mimi mwenyewe hivi karibuni, na viongozi wenu wanaweza kufuatana nami. Kama mtu huyu hakika amefanya chochote kibaya, wanaweza kumshitaki huko.”

Festo alikaa Yerusalemu kwa siku nane au kumi zaidi kisha alirudi Kaisaria. Siku iliyofuata Festo akawaambia askari wamlete Paulo mbele yake. Festo alikuwa amekaa kwenye kiti cha hukumu. Paulo aliingia kwenye chumba na Wayahudi waliokuja kutoka Yerusalemu walisimama kumzunguka. Walileta mashitaka mengi mazito dhidi yake, lakini hawakuweza kuthibitisha chochote. Paulo alijitetea mwenyewe, akasema, “Sijatenda kitu chochote kibaya kinyume na sheria ya Kiyahudi, kinyume na Hekalu au kinyume na Kaisari.”

Lakini Festo alitaka kuwaridhisha Wayahudi. Hivyo alimwuliza Paulo, “Unataka kwenda Yerusalemu ili nikakuhukumu huko kutokana na mashitaka haya?”

10 Paulo akasema, “Kwa sasa nimesimama kwenye kiti cha hukumu cha Kaisari. Hapa ndipo ninatakiwa kuhukumiwa. Sijatenda lolote baya kwa Wayahudi na unafahamu hilo. 11 Ikiwa nilitenda chochote kibaya na sheria inasema ni lazima nife, basi ninakubali kuwa ninapaswa kufa. Siombi kuokolewa kutokana na kifo. Lakini kama mashitaka haya siyo ya kweli, basi hakuna anayeweza kunikabidhi kwa watu hawa. Hapana, Nataka Kaisari aisikilize kesi yangu!”

12 Festo alijadiliana na washauri wake kuhusu hili. Kisha akasema, “Umeomba kumwona Kaisari, basi utakwenda kwa Kaisari!”

Festo Amwuliza Mfalme Agripa Kuhusu Paulo

13 Siku chache baadaye Mfalme Agripa pamoja na dada yake aliyeitwa Bernike[a] walikuja Kaisaria kumtembelea Festo. 14 Walikaa huko kwa siku nyingi, na Festo akamwambia mfalme kuhusu kesi ya Paulo. Festo alisema, “Kuna mtu ambaye Feliki alimwacha gerezani. 15 Nilipokwenda Yerusalemu, viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wa Kiyahudi walitengeneza mashitaka dhidi yake. Walinitaka nimhukumu kifo. 16 Lakini niliwaambia, ‘Mtu anaposhitakiwa kuwa ametenda jambo baya, Warumi hawampeleki kwa watu wengine ili ahukumiwe. Kwanza, ni lazima aonane na watu wanaomshtaki. Na kisha ni lazima aruhusiwe kujitetea yeye mwenyewe dhidi ya mashitaka yao.’

17 Hivyo Wayahudi walipokuja hapa kwa ajili ya kesi, sikupoteza muda. Siku iliyofuata nilikaa kwenye kiti cha hukumu na kuamuru Paulo aletwe ndani. 18 Wayahudi walisimama na kumshitaki. Lakini hawakumshitaki kwa makosa niliyodhani wangemshitaki. 19 Mashitaka yao yote yalihusu dini yao wenyewe na kuhusu mtu anayeitwa Yesu. Yesu alikufa lakini Paulo anasema bado yuko hai. 20 Baada ya kuona kuwa sijui jinsi ya kuyachunguza mambo haya. Hivyo nilimwuliza Paulo, ‘Unataka kwenda Yerusalemu ili ukahukumiwe huko?’ 21 Lakini Paulo aliomba abaki mahabusu hapa Kaisaria. Anataka uamuzi kutoka kwa mfalme mkuu. Hivyo niliamua aendelee kushikiliwa hapa mpaka nitakapompeleka kwa Kaisari huko Rumi.”

22 Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyu pia.”

Festo akasema, “Utaweza kumsikiliza kesho.”

23 Siku iliyofuata Agripa na Bernike walikuja kwenye mkutano kwa fahari kubwa, wakijifanya watu wa muhimu sana. Waliingia kwenye chumba pamoja na viongozi wa kijeshi na watu maarufu wa mji. Festo akawaamuru askari wamwingize Paulo ndani.

24 Festo akasema, “Mfalme Agripa nanyi nyote mliokusanyika hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu. Wayahudi wote, hapa na Yerusalemu wamelalamika kwangu juu yake. Wanapolalamika, wanapaza sauti zao wakisema kwamba anapaswa kuuawa. 25 Nilipochunguza, sikuona ikiwa alitenda kosa lolote linalostahili hukumu ya kifo. Lakini ameomba kuhukumiwa na Kaisari, hivyo niliamua apelekwe Rumi. 26 Hata hivyo, sifahamu kwa hakika ni nini cha kumwandikia bwana wangu Kaisari kama sababu ya kumpeleka mtu huyu kwake. Hivo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa wewe, Mfalme Agripa. Ninatumaini kwamba utamwuliza maswali na kunipa kitu cha kumwandikia Kaisari. 27 Nafikiri ni upumbavu kupeleka mfungwa kwa Kaisari bila kuainisha mashitaka dhidi yake.”

Footnotes

  1. 25:13 Bernike Dada yake Mfalme Agripa, binti mkubwa wa Herode Agripa wa Kwanza.