Add parallel Print Page Options

Paulo Asimama Mbele ya Mfalme Agripa

26 Agripa[a] akamwambia Paulo, “Unaweza sasa kujitetea wewe mwenyewe.” Paulo akanyoosha mkono wake ili wamsikilize kwa makini na akaanza kusema. “Mfalme Agripa, najisikia heshima kusimama hapa mbele yako leo ili nijibu mashitaka yote yaliyotengenezwa na Wayahudi dhidi yangu. Ninafurahi kuzungumza nawe, kwa sababu unafahamu sana kuhusu desturi za Kiyahudi na mambo ambayo Wayahudi hubishana. Tafadhali uwe mvumilifu kunisikiliza.

Wayahudi wote wanafahamu maisha yangu yote. Wanafahamu namna nilivyoishi tangu mwanzo miongoni mwa watu mwangu na baadaye Yerusalemu. Wayahudi hawa wamenifahamu kwa muda mrefu. Wakitaka wanaweza kukwambia kwamba nilikuwa Farisayo mzuri. Na Mafarisayo wanazitii sheria za dini ya Kiyahudi kwa uangalifu kuliko kundi lolote. Na sasa nimeshitakiwa kwa sababu ninatumaini ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu. Hii ni ahadi ambayo makabila yote kumi na mbili ya watu wetu yanatumaini kuipokea. Kwa sababu ya tumaini hili Wayahudi wanamtumikia Mungu usiku na mchana. Ee Mfalme wangu, Wayahudi wamenishitaki kwa sababu ninatumaini ahadi hii hii. Kwa nini ninyi watu mnadhani Mungu hawezi kuwafufua watu kutoka kwa wafu?

Huko nyuma nilidhani kuwa ninapaswa kufanya kinyume na Yesu kutoka Nazareti kwa kadri ninavyoweza. 10 Na ndivyo nilivyofanya, kuanzia Yerusalemu. Viongozi wa makuhani walinipa mamlaka ya kuwaweka gerezani watu wa Mungu wengi. Na walipokuwa wanauawa nilikubali kuwa lilikuwa jambo zuri. 11 Nilikwenda katika masinagogi yote na kuwaadhibu, nikijaribu kuwafanya wamlaani[b] Yesu. Hasira yangu dhidi ya watu hawa ilikuwa kali sana kiasi kwamba nilikwenda katika miji mingine kuwatafuta na kuwaadhibu.

Paulo Aeleza Alivyomwona Yesu

12 Wakati fulani viongozi wa makuhani walinipa ruhusa na mamlaka kwenda katika mji wa Dameski. 13 Nikiwa njiani, mchana, niliona mwanga kutoka mbinguni, unaong'aa kuliko jua. Uling'aa kunizunguka mimi pamoja na wale waliokuwa wanasafiri pamoja nami. 14 Sote tulianguka chini. Kisha nilisikia sauti iliyozungumza nami kwa Kiaramu. Sauti ilisema, ‘Sauli, Sauli, kwa nini unanitesa? Unajiumiza wewe mwenyewe kwa kunipinga mimi.’

15 Nilisema, ‘Wewe ni nani, Bwana?’

Bwana alisema, ‘Mimi ni Yesu. Unayemtesa. 16 Simama! Nimekuchagua wewe kuwa mtumishi wangu. Utawaambia watu habari zangu, ulichoona leo na yale nitakayokuonesha. Hii ndiyo sababu nimekuja kwako. 17 Nitakulinda dhidi ya watu wako na dhidi ya watu wasio Wayahudi, ninaokutuma kwao. 18 Utawafanya waielewe kweli. Watatoka gizani na kuja kwenye mwanga. Watageuka kutoka kwenye mamlaka ya Shetani na kumgeukia Mungu. Ndipo dhambi zao zitasamehewa, na wataweza kupewa nafasi miongoni mwa watu wa Mungu, walifanywa watakatifu kwa kuniamini.’”

Paulo Aeleza Kuhusu Kazi Yake

19 Paulo aliendelea kusema: “Mfalme Agripa, baada ya kuona maono haya kutoka mbinguni, nilitii. 20 Nilianza kuwaambia watu kubadili mioyo na maisha yao na kumgeukia Mungu. Niliwaambia kufanya yale yatakayoonyesha kwamba hakika wamebadilika. Kwanza nilikwenda kwa watu waliokuwa Dameski. Kisha nikaenda Yerusalemu na kila sehemu ya Uyahudi na nikawaambia watu huko. Nilikwenda pia kwa watu wasio Wayahudi.

21 Hii ndiyo sababu Wayahudi walinikamata na kujaribu kuniua Hekaluni. 22 Lakini Mungu alinisaidia, na bado ananisaidia leo. Kwa msaada wa Mungu nimesimama hapa leo na kuwaambia watu kile nilichokiona. Lakini sisemi chochote kipya. Ninasema kile ambacho Musa na manabii walisema kingetokea. 23 Walisema kwamba Masihi atakufa na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu. Walisema kwamba ataleta mwanga wa kweli[c] ya Mungu inayowaokoa wote, Wayahudi na wasio Wayahudi.”

Paulo Ajaribu Kumshawishi Agripa

24 Paulo alipokuwa bado anajitetea, Festo alipaza sauti akasema, “Paulo, umerukwa na akili! Kusoma kwingi kumekufanya kichaa.” 25 Paulo akasema, “Mheshimiwa Festo, mimi si kichaa. Ninachokisema ni kweli na kinaingia akilini. 26 Mfalme Agripa analifahamu hili, na ninaweza kuzungumza naye kwa uhuru. Ninafahamu kwamba amekwisha kusikia kuhusu mambo haya, yalitokea mahali ambako kila mtu aliyaona. 27 Mfalme Agripa, unaamini yale ambayo manabii waliandika? Ninajua unaamini!”

28 Mfalme Agripa akamwambia Paulo, “Unadhani unaweza kunishawishi kirahisi kiasi hicho ili niwe Mkristo?”

29 Paulo akasema, “Haijalishi kwangu, ikiwa ni vigumu au rahisi. Ninaomba tu kwa Mungu kwamba si wewe peke yako lakini kila mtu anayenisikiliza leo angeokolewa ili awe kama mimi, isipokuwa kwa minyororo hii!”

30 Mfalme Agripa, Gavana Festo, Bernike, na watu wote waliokaa pamoja nao wakasimama 31 na kuondoka chumbani. Walikuwa wanaongea wenyewe. Walisema, “Mtu huyu hajafanya chochote kinachostahili kuuawa au kuwekwa gerezani.” 32 Kisha Agripa akamwambia Festo, “Tungemwachia huru, lakini ameomba kumwona Kaisari.”

Footnotes

  1. 26:1 Agripa Herode Agripa wa Pili, mjukuu wa herode Mkuu.
  2. 26:11 wamlaani Kwa maana ya kawaida, “wamkufuru”, sawa na kusema hawataki kumwamini Yesu.
  3. 26:23 ataleta mwanga wa kweli Kwa maana ya kawaida, “kutangaza mwanga”.