Add parallel Print Page Options

Paulo Aenda Rumi

27 Iliamriwa kwamba tutakwenda Italia. Ofisa wa Jeshi aliyeitwa Yulio, aliyetumika katika jeshi maalumu la mfalme mkuu, aliwekwa kuwa kiongozi wa kumlinda Paulo na baadhi ya wafungwa wengine safarini. Tuliingia kwenye meli katika mji wa Adramatio. Meli hiyo ilikuwa inasafiri kupitia sehemu mbalimbali za Asia. Aristarko, mtu Thesalonike katika makedonia alisafiri pamoja nasi.

Siku iliyofuata tulifika kwenye mji wa Sidoni. Yulio alikuwa mwema sana kwa Paulo na akampa uhuru wa kwenda kuwatembelea rafiki zake pale, walimpa chochote alichohitaji. Tuliondoka katika mji ule na tukatweka tanga tukasafiri karibu na kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa unavuma kinyume nasi. Tulikwenda kwa kukatisha bahari upande wa Kilikia na Pamfilia. Kisha tukafika katika mji wa Mira katika jimbo la Likia. Tulipofika hapo ofisa wa jeshi akapata meli iliyotoka katika mji wa Iskanderia iliyokuwa inakwenda Italia. Akatupandisha humo.

Tulitweka tanga na kusafiri taratibu kwa siku nyingi. Ilikuwa vigumu kwetu kufika katika mji wa Nido kwa sababu upepo ulikuwa unavuma kinyume chetu. Hatukuweza kuendelea zaidi kwa kupitia njia hiyo, hivyo tulitweka tanga tukasafiri kupitia upande wa kusini mwa kisiwa cha Krete karibu na Salmone. Tulisafiri sambamba na pwani, lakini kwa shida. Ndipo tukafika mahali palipoitwa Bandari Salama, karibu na mji wa Lasea.

Tulikuwa tumepoteza muda mwingi, na ilikuwa hatari kutweka tanga, kwa sababu tayari ilikuwa baada ya siku ya Kiyahudi ya kufunga.[a] Hivyo Paulo aliwaonya akasema, 10 “Ndugu zangu, ninaona kuwa kutakuwa shida nyingi katika safari hii. Meli, kila kitu ndani yake na pia hata maisha yetu yanaweza kupotea!” 11 Lakini nahodha na mmiliki wa meli hawakukubaliana na Paulo. Hivyo ofisa wa jeshi alikubali walichokisema badala ya kumwamini Paulo. 12 Pia, bandari ile haikuwa mahali pazuri kwa meli kukaa majira ya baridi, hivyo watu karibu wote wakaamua kwamba ni lazima tuondoke pale. Walitegemea kuwa tungeweza kufika Foeniki, ambako meli ingekaa majira ya baridi. Foeniki ulikuwa mji katika kisiwa cha Krete. Ulikuwa na bandari iliyotazama Kusini-Magharibi na Kaskazini-Magharibi.

Dhoruba

13 Ndipo upepo mzuri ukaanza kuvuma kutoka kusini. Watu ndani ya meli wakafikiri, “Huu ndio upepo tulioutaka, na sasa tumeupata!” Hivyo wakavuta nanga. Tulitweka tanga tukasafiri karibu na kisiwa cha Krete. 14 Lakini upepo wenye nguvu unaoitwa “Kaskazini-Mashariki” ulikuja kwa kukikatisha kisiwa. 15 Upepo huu uliichukua meli na kuisukumia mbali. Meli haikuweza kwenda kinyume na upepo, hivyo tulisimama tukijaribu kuuacha upepo utusukume.

16 Tulikwenda upande wa chini wa kisiwa kidogo kilichoitwa Kauda. Kisiwa kikatukinga dhidi ya upepo, tulichukua mtumbwi wa kuokolea watu, lakini ilikuwa vigumu sana kufanya hivyo. 17 Baada ya watu kuleta mtumbwi wa kuokolea, wakaifunga meli kamba kuizungushia ili iendelee kushikamana isipasuke. Waliogopa kwamba meli ingekwama kwenye mchanga wa pwani ya Sirti.[b] Hivyo walishusha tanga na kuiacha meli ichukuliwe na upepo.

18 Siku iliyofuata upepo ulivuma kinyume nasi kwa nguvu kiasi kwamba watu walitupa baadhi ya vitu kutoka katika shehena ya meli.[c] 19 Siku moja baadaye wakatupa vifaa vya meli. 20 Kwa siku nyingi hatukuweza kuliona jua au nyota. Dhoruba ilikuwa mbaya sana. Tulipoteza matumaini yote ya kuendelea kuwa hai, tulidhani tutakufa.

21 Watu hawakula kwa muda mrefu. Ndipo siku moja Paulo akasimama mbele yao na kusema, “Ndugu zangu, niliwaambia tusiondoke Krete. Mngenisikiliza msingepata tatizo hili na hasara hii. 22 Lakini sasa ninawaambia iweni na furaha. Hakuna hata mmoja wenu atakayekufa, lakini meli itapotea. 23 Usiku uliopita malaika kutoka kwa Mungu ninayemwabudu na ambaye mimi ni wake. 24 Aliniambia, ‘Paulo, usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari. Mungu amekupa ahadi hii: Ataokoa maisha ya wote wanaosafiri pamoja nawe.’ 25 Hivyo ndugu, msihofu kitu chochote. Ninamwamini Mungu, na nina uhakika kila kitu kitatokea kama malaika wake alivyoniambia. 26 Lakini tutajigonga kwenye kisiwa.”

27 Usiku wa kumi na nne tulikuwa bado tunasukumwa na upepo katika bahari ya Adriatiki. Mabaharia wakadhani tulikuwa karibu na nchi kavu. 28 Wakatupa kamba iliyofungwa kitu kizito kwenye ncha yake. Wakakuta kwamba kina cha maji ni futi mia moja na ishirini.[d] Wakaendelea mbele kidogo na kutupa kamba tena. Kina kilikuwa futi tisini.[e] 29 Mabaharia waliogopa kwa kudhani kwamba tungegonga miamba, hivyo wakatupa nanga nne kwenye maji. Kisha wakaomba mchana ufike. 30 Baadhi ya mabaharia walitaka kuiacha meli, waliishusha majini mtumbwi wa kuokolea. Walitaka watu wengine wadhani kuwa walikuwa wanatupa nanga upande wa mbele wa meli. 31 Lakini Paulo alimwambia ofisa wa jeshi na askari wengine, “Iwapo watu hawa hawatakaa ndani ya meli, mtapoteza matumaini yote ya kupona.” 32 Hivyo askari wakakata kamba na kuuacha mtumbwi uanguke majini.

33 Kabla ya kupambazuka Paulo alianza kuwashawishi watu wote kula. Alisema, “Kwa wiki mbili mmekuwa mnasubiri na kuangalia, hamjala kwa siku kumi na nne. 34 Sasa ninawasihi mle chakula, mnakihitaji ili kuishi. Hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza hata unywele mmoja kutoka kwenye kichwa chake.” 35 Baada ya kusema hili, Paulo alichukua baadhi ya mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya mikate hiyo mbele yao wote. Akakata kipande na kuanza kula. 36 Watu wote wakafarijika na kuanza kula pia. 37 (Walikuwemo watu mia mbili sabini na sita ndani ya meli.) 38 Tulikula kila tulichohitaji. Kisha tukaanza kumwaga nafaka baharini ili meli iwe nyepesi.

Meli Yaharibiwa

39 Mchana ulipofika, mabaharia waliiona nchi kavu, lakini hawakupafahamu mahali pale. Waliona ghuba yenye ufukwe na walitaka kuipeleka meli ufukweni ikiwa wangeweza. 40 Hivyo walikata kamba kwenye nanga na kuziacha nanga ndani ya bahari. Wakati huo huo walifungua kamba zilizokuwa zinaushikilia usukani. Kisha wakanyanyua tanga la mbele na kutweka tanga kuelekea ufukweni. 41 Lakini meli uligonga mwamba wa michanga. Sehemu ya mbele ya meli ilikwama pale na haikuweza kutoka. Kisha mawimbi makubwa yakaanza kuvunja sehemu ya nyuma ya meli vipande vipande.

42 Askari waliamua kuwaua wafungwa ili asiwepo mfungwa hata mmoja atakayeogelea na kutoroka. 43 Lakini Yulio, ofisa wa jeshi alitaka Paulo asiuawe. Hivyo hakuwaruhusu askari kuwaua wafunga. Aliwaambia watu wanaoweza kuogelea, waruke majini kwenda nchi kavu. 44 Wengine walitumia mbao au vipande vya meli. Hivi ndivyo ambavyo watu wote walifika nchi kavu wakiwa salama.

Footnotes

  1. 27:9 siku ya Kiyahudi ya kufunga Siku ya Upatanisho, siku muhimu na takatifu ya Kiyahudi nyakati za miti kupukutisha majani yake. Huu ulikuwa wakati ambao dhoruba kali hutokea baharini.
  2. 27:17 pwani ya Sirti Kwa sasa bado ni pwani (Ghuba) ya Sirti katika nchi ya Libya, Afrika ya Kaskazini.
  3. 27:18 walitupa … shehena ya meli Walifanya hivi ili meli iwe nyepesi na isizame kirahisi.
  4. 27:28 futi mia moja na ishirini Kwa maana ya kawaida, “fatomu 20”, kama mita 40.
  5. 27:28 futi tisini Kwa maana ya kawaida, “fatomu 15”, kama mita 30.