Add parallel Print Page Options

Watu Saba Wachaguliwa kwa Kazi Maalumu

Watu wengi zaidi walipokuwa wafuasi wa Yesu. Wafuasi waliokuwa wakizungumza Kiyunani walianza kuwalalamikia wafuasi wenzao waliokuwa wanazungumza Kiebrania au Kiaramu. Walisema kuwa wajane wao walikuwa hawapewi mgao wao kutokana na kile wafuasi walikuwa wanapewa kila siku. Mitume kumi na mbili wakaita kundi lote la wafuasi pamoja.

Mitume wakawaambia, “Haitakuwa sahihi sisi kuacha kazi yetu ya kuwafundisha watu neno la Mungu ili tuwe wasimamizi wa ugawaji wa chakula kwa watu. Hivyo, kaka zetu na dada zetu, chagueni wanaume saba miongoni mwenu wenye ushuhuda mzuri, watu waliojaa hekima na Roho. Nasi tutawaweka kuwa wasimamizi wa kazi hii muhimu. Na hivyo itatuwezesha sisi kutumia muda wetu wote katika kuomba na kufundisha neno la Mungu.”

Kundi lote la waamini likakubaliana na wazo hili. Hivyo wakawachagua wanaume saba: Stefano (aliyejaa imani na Roho Mtakatifu), Filipo,[a] Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena, na Nikolasi (mtu wa Antiokia aliyeongoka na kufuata dini ya Kiyahudi). Kisha, wakawaweka watu hawa mbele ya mitume, nao mitume waliwaombea na kuweka mikono juu yao.

Neno la Mungu lilikuwa linawafikia watu wengi zaidi. Kundi la wafuasi katika Yerusalemu likawa kubwa sana. Hata idadi kubwa ya makuhani wa Kiyahudi waliamini na kutii.

Baadhi ya Wayahudi Wampinga Stefano

Mungu alimpa Stefano nguvu ya kutenda maajabu makuu na miujiza katikati ya watu. Lakini baadhi ya Wayahudi pale waliotoka katika sinagogi la Watu Huru,[b] kama lilivyoitwa. Kundi hili lilijumuisha Wayahudi kutoka Kirene, Iskanderia, Kilikia na Asia. Walianza kubishana na Stefano. 10 Lakini Roho Mtakatifu alimwezesha kuzungumza kwa hekima. Maneno yake yalikuwa na nguvu hata Wayahudi hawa hawakuweza kubishana naye.

11 Hivyo wakawaambia baadhi ya watu waseme, “Tumemsikia Stefano akimtukana Musa na Mungu!” 12 Jambo hili liliwakasirisha sana watu, wazee wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Wakamkamata Stefano na kumpeleka mbele ya Baraza Kuu.

13 Wayahudi wakawaleta baadhi ya watu kwenye mkutano ili kusema uongo kuhusu Stefano. Watu hawa walisema, “Daima mtu huyu husema maneno kinyume na mahali hapa patakatifu na kinyume na Sheria ya Musa. 14 Tulimsikia akisema kwamba Yesu kutoka Nazareti atapaharibu mahali hapa na kubadilisha yale ambayo Musa aliyotuambia kufanya.” 15 Kila mtu aliyekuwa kwenye mkutano wa baraza alikuwa akimshangaa Stefano kwani uso wake ulionekana kama uso wa malaika.

Footnotes

  1. 6:5 Filipo Siyo mtume aliyeitwa Filipo.
  2. 6:9 Watu Huru Wayahudi waliokuwa watumwa au ambao baba zao walikuwa watumwa, lakini wao walikuwa huru.