Add parallel Print Page Options

1-3 Sauli aliridhia kuwa kuuawa kwa Stefano lilikuwa jambo jema. Baadhi ya wacha Mungu walimzika Stefano, wakaomboleza na kumlilia kwa sauti kuu.

Matatizo Kwa waamini

Kuanzia siku hiyo Wayahudi walianza kulitesa sana kanisa na waamini katika mji wa Yerusalemu. Sauli pia alijaribu kuliharibu kanisa. Aliingia katika nyumba za waamini, akawaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Waamini wote walikimbia kutoka Yerusalemu, mitume peke yao ndiyo walibaki. Waamini walikwenda mahali tofauti tofauti katika Uyahudi na Samaria. Walitawanyika kila mahali, na kila walikokwenda waliwahubiri watu Habari Njema.

Filipo Ahubiri Katika Samaria

Filipo[a] alikwenda katika mji mkuu wa jimbo la Samaria na kuwahubiri watu kuhusu Masihi. Watu wa Samaria walimsikiliza Filipo na kuona miujiza aliyotenda. Wote walisikiliza kwa makini yale aliyosema. Watu wengi miongoni mwao walikuwa na mapepo, lakini Filipo aliyakemea mapepo na yaliwatoka watu. Mapepo yalipiga kelele nyingi yalipokuwa yanawatoka watu. Walikuwepo pia watu wengi waliopooza na walemavu wa miguu pale. Filipo aliwaombea na wote walipona. Kulikuwa furaha kubwa katika mji ule wa Samaria siku ile!

Mtu mmoja aliyeitwa Simoni alikuwa anaishi katika mji huo. Kabla Filipo hajaenda huko, Simoni alikuwa akifanya uchawi na kuwashangaza watu wote wa Samaria. Alijigamba na kujiita mtu mkuu. 10 Watu wote, kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliamini yale aliyosema Simoni. Walisema, “Mtu huyu ndiye anayeitwa ‘Nguvu Kuu ya Mungu.’” 11 Simoni aliwashangaza watu kwa muda mrefu kwa uchawi wake na watu wote wakawa wafuasi wake. 12 Lakini Filipo alipowahubiri watu Habari Njema kuhusu Ufalme wa Mungu na Nguvu za Yesu Kristo. Wanaume na wanawake waliamini alichosema Filipo na wakabatizwa. 13 Simoni mwenyewe aliamini, na baada ya kubatizwa, alikaa karibu na Filipo. Alipoona miujiza na matendo makuu ya ajabu yaliyofanyika kupitia Filipo, alishangaa.

14 Mitume mjini Yerusalemu, waliposikia kuwa watu wa Samaria wameupokea Ujumbe wa Mungu, waliwatuma Petro na Yohana kwenda kwa watu wa Samaria. 15 Petro na Yohana walipofika, waliomba ili Roho Mtakatifu awashukie waamini wa Samaria. 16 Watu hawa walikuwa wamebatizwa katika jina la Bwana Yesu, lakini Roho Mtakatifu alikuwa bado hajamshukia hata mmoja wao. Na hii ndiyo sababu Petro na Yohana waliomba. 17 Mitume hawa wawili walipoweka mikono yao juu ya watu, Roho Mtakatifu aliwashukia.

18 Simoni aliyekuwa mchawi alipoona Roho Mtakatifu anatolewa kwa watu kwa kuweka mikono juu yao. Aliwapa pesa mitume. 19 Akasema, “Nipeni na mimi nguvu hii ili nitakapoweka mikono yangu juu ya mtu yeyote, atampata Roho Mtakatifu.”

20 Petro akamwambia Simoni, “Wewe pamoja na pesa zako mwangamie kwa sababu unadhani unaweza kununua karama kutoka kwa Mungu kwa pesa. 21 Huwezi kushirikiana nasi katika kazi hii. Moyo wako si safi mbele za Mungu. 22 Badili moyo wako! Achana na mawazo haya maovu na umwombe Bwana. Yumkini atakusamehe! 23 Kwa kuwa ninaona umejaa wivu mwingi nawe ni mfungwa wa uovu.”

24 Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili haya uliyosema yasinipate.”

25 Ndipo wale mitume wawili waliwaambia watu waliyoona Yesu akitenda. Wakawaambia ujumbe wa Bwana. Kisha wakarudi Yerusalemu. Wakiwa njiani kurudi, walipitia katika miji mingi ya Wasamaria na kuwahubiri watu Habari Njema.

Filipo Amfundisha Mtu Kutoka Ethiopia

26 Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jiandae na uende kusini katika barabara ya jangwani inayoteremka kutoka Yerusalemu kwenda Gaza.”

27 Filipo alijiandaa na kwenda. Akiwa njiani alimwona mwanaume kutoka Ethiopia. Alikuwa towashi na ofisa muhimu wa Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa na mweka hazina mkuu wa malkia. Mtu huyu alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu. 28 Na alikuwa anarudi Ethiopia. Alikuwa ameketi katika gari lake la kukokotwa na farasi akiwa anasoma kitabu cha nabii Isaya.

29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye gari hilo na uwe karibu yake.” 30 Hivyo Filipo akaenda karibu na gari, akamsikia mtu yule akisoma kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamwuliza, “Unaelewa unachosoma?”

31 Yule mtu akajibu, “Nitaelewaje? Ninahitaji mtu wa kunifafanulia.” Ndipo akamwomba Filipo apande garini na aketi pamoja naye. 32 Sehemu ya Maandiko aliyokuwa anasoma ilikuwa hii:

“Alikuwa kama kondoo
    anayepelekwa kwa mchinjaji.
Alikuwa kama mwana kondoo asivyopiga kelele
    anapokatwa manyoya yake.
    Hakusema kitu.
33 Alidhalilishwa,
    na kunyimwa haki zake zote.
Maisha yake duniani yamekoma.
    Hivyo hakutakuwa simulizi yoyote kuhusu wazaliwa wake.”(A)

34 Afisa[b] akamwambia Filipo, “Tafadhali niambie, nabii anazungumza kuhusu nani? Anazungumza kuhusu yeye mwenyewe au mtu mwingine?” 35 Filipo akaanza kuzungumza. Alianzia na Andiko hili na kumwambia mtu yule Habari Njema kuhusu Yesu.

36 Walipokuwa wanasafiri waliyakuta maji mahali fulani. Afisa akasema, “Tazama! Hapa kuna maji! Nini kinanizuia nisibatizwe?” 37 [c] 38 Ndipo Afisa akaamuru gari lake lisimame. Wote wawili, Filipo na Afisa, wakatelemka wakaingia kwenye maji na Filipo akambatiza towashi. 39 Walipotoka kwenye maji, Roho wa Bwana akamchukua Filipo; afisa hakumwona Filipo tena. Afisa aliendelea na safari yake kurudi nyumbani, akiwa mwenye furaha sana. 40 Lakini Filipo alionekana katika mji ulioitwa Azoto. Alikuwa akienda kwenye mji wa Kaisaria. Aliwahubiri watu Habari Njema katika miji yote wakati anasafiri kutoka Azoto kwenda Kaisaria.

Footnotes

  1. 8:5 Filipo Siyo mtume aliyeitwa Filipo.
  2. 8:34 Afisa Kwa maana ya kawaida, “towashi”. Pia katika mstari wa 36,38,39.
  3. 8:37 Nakala zingine za baadaye za Matendo zimeongeza mstari wa 37: Filipo akajibu, “Ikiwa unaamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa. Ofisa akasema, ‘Ninaamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.’”