Mungu Ajibu Sala Ya Kornelio

10 Katika mji wa Kaisaria aliishi afisa mmoja wa jeshi ambaye alikuwa kamanda wa kikosi cha Italia, jina lake Kornelio. Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na jamii yake yote. Alitoa msaada kwa ukarimu kwa watu na kumwomba Mungu mara kwa mara.

Alasiri moja, mnamo saa tisa, malaika wa Mungu alimjia katika ndoto na kumwita, “Kornelio!” Kornelio akamtazama yule malaika kwa hofu akasema, “Ni nini Bwana?” Malaika akasema, “Sala zako na sadaka ulizotoa kwa maskini zimefika mbinguni, na Mungu amezikumbuka. Sasa tuma watu Jopa wakamlete Simoni ait waye Petro. Yeye hivi sasa anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi kando ya bahari.” Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye ali poondoka, Kornelio aliwaita watumishi wake wawili na mlinzi wake mmoja aliyekuwa mcha Mungu, na baada ya kuwasimulia mambo yote yaliyotokea, akawatuma waende Jopa.

Kesho yake, walipokuwa wanaukaribia mji, Petro alipanda juu ghorofani kuomba mnamo saa sita. 10 Alipokuwa akisali aliona njaa akatamani kupata chakula. Lakini wakati kilipokuwa kinaan daliwa, alisinzia akaota ndoto. 11 Akaona katika ndoto mbingu zimefunguka na kitu kama shuka kubwa ikishushwa kwa ncha zake nne. 12 Ndani ya ile shuka walikuwemo aina zote za wanyama na nyoka na ndege. 13 Kisha sauti ikamwambia Petro, “Inuka, uchinje na ule mnyama ye yote umpendaye kati ya hawa.” 14 Petro akajibu, “La Bwana! Sijawahi kula cho chote ambacho kimetajwa na sheria zetu za Kiyahudi kuwa ni kichafu.” 15 Ile sauti ikarudia kusema naye mara ya pili, “Usiite cho chote alichokitakasa Bwana kuwa ni kichafu.” 16 Hii ilitokea mara tatu, ndipo ile shuka ikarudishwa mbinguni.

17 Petro alikuwa bado akijiuliza maana ya mambo haya aliyoy aona, wakati wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio walipofika kwenye nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi. 18 Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.

19 Wakati huo Petro alikuwa akifikiria juu ya ile ndoto, Roho Mtakatifu akamwambia, “Wako watu watatu wamekuja kukuta futa. 20 Shuka chini ukaonane nao na usione shaka kwenda nao kwa kuwa nimewatuma kwako.” 21 Petro akashuka, akawaendea wale watu akawaambia, “Mimi ndiye mnayemtafuta. Mnataka nini?” 22 Wao wakamjibu, “Tumetumwa na Kamanda Kornelio ambaye ni mtu mwema anayemcha Mungu na kusifiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagi zwa na malaika wa Mungu akukaribishe nyumbani kwake, ili asiki lize maneno utakayomwambia.” 23 Petro aliwakaribisha walale kwake. Kulipokucha akaandamana nao pamoja na baadhi ya ndugu waamini wa pale Jopa.

Petro Nyumbani Kwa Kornelio

24 Kesho yake wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwan goja pamoja na ndugu zake na marafiki wa karibu ambao alikuwa amewaalika. 25 Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akapiga magoti. 26 Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama! Mimi ni mwanadamu tu.” 27 Petro alipokuwa akizungumza naye aliingia ndani ambapo alikuta watu wengi wamekusanyika. 28 Petro akawaambia, “Mnajua kwamba sheria ya Wayahudi hairu husu Myahudi kuwatembelea au kuchangamana na watu wa mataifa men gine kama hivi nifanyavyo. Lakini Mungu amenionyesha kwamba nisimwone mtu ye yote kuwa mchafu au asiyefaa. 29 Ndiyo sababu ulipotuma nije sikusita. Kwa hiyo naomba unieleze kwa nini ume niita.” 30 Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa mchana. Mara akatokea mtu aliyevaa nguo za kung’ara akasimama mbele yangu. 31 Akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na Mungu, naye amekumbuka msaada wako kwa maskini. 32 Basi tuma watu waende Jopa wakamwite Simoni aitwaye Petro. Yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko sehemu za pwani.’ 33 Ndio sababu nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vizuri kuja. Basi sasa tuko hapa wote mbele ya Mungu kuyasikiliza yote ambayo Mungu amekuamuru kutuambia.”

Hotuba Ya Petro

34 “Ndipo Petro alianza kwa kusema, “Sasa naamini ya kuwa Mungu hana upendeleo. 35 Yeye huwakubali watu wa kila taifa wam chao na kutenda haki. 36 Huu ndio ujumbe ambao Mungu aliwapele kea watu wa Israeli, kuhusu Habari Njema za amani kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye ni Bwana wa wote. 37 Ninyi bila shaka mnafa hamu mambo yaliyotokea sehemu zote za Yudea, kuanzia Galilaya tangu wakati wa mahubiri ya Yohana Mbatizaji. 38 Mnafahamu jinsi Mungu alivyompa Yesu wa Nazareti Roho Mtakatifu na uwezo, na jinsi alivyozunguka kila mahali akifanya mema na kuponya wote waliokuwa wakiteswa na nguvu za shetani, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye. 39 Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyofanya katika nchi ya Wayahudi na Yerusalemu. Walimwua kwa kumtundika msalabani. 40 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu. 41 Hakuonekana kwa watu wote, lakini alionekana kwa mashahidi ambao Mungu aliwachagua, yaani sisi ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake. 42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote, na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyechaguliwa na Mungu kuwahukumu walio hai na wafu. 43 Manabii wote walishuhudia juu yake, kwamba kila mtu amwami niye atasamehewa dhambi katika jina lake.”

Mataifa Wapokea Roho Mtakatifu

44 Petro alipokuwa akisema maneno hayo, Roho Mtakatifu ali washukia wote waliokuwa wakisikiliza. 45 Wale Wayahudi waamini waliokuwa wamekuja na Petro walishangaa sana kuona kuwa Mungu aliwapa watu wa mataifa kipawa cha Roho Mtakatifu. 46 Kwa kuwa waliwasikia wakisema kwa lugha mpya na kumtukuza Mungu kwa ukuu wake. Ndipo Petro akasema, 47 “Je, kuna mtu anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.” 48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.

Petro na Kornelio

10 Kulikuwa mtu aliyeitwa Kornelio katika mji wa Kaisaria. Mtu huyu alikuwa ofisa wa kikosi kilichoitwa “Kikosi cha Kiitalia” katika jeshi la Rumi. Alikuwa mcha Mungu. Yeye na watu wengine wote walioishi katika nyumba yake walikuwa wanamwabudu Mungu wa kweli. Alitoa pesa zake nyingi kuwasaidia maskini miongoni mwa Wayahudi na daima alimwomba Mungu kwa kufuata utaratibu kama ilivyokuwa. Mchana mmoja yapata saa tisa, kwa uwazi na dhahiri Kornelio aliona maono. Alimwona malaika kutoka kwa Mungu akimwendea na akamwambia, “Kornelio!”

Akiwa anashangaa na kuogopa, Kornelio akasema, “Unataka nini, bwana?”

Malaika akamwambia, “Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako unazowapa maskini. Anakukumbuka kwa yote uliyotenda. Tuma baadhi ya watu sasa waende katika mji wa Yafa wakamlete mtu anayeitwa Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. Anakaa kwa mtu ambaye naye pia anaitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko kwenye ufukwe wa bahari.” Malaika aliyeongea na Kornelio akaondoka. Ndipo Kornelio aliita watumishi wake wawili na askari mmoja. Askari alikuwa mcha Mungu, mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. Kornelio akawaelekeza kila kitu watu hawa watatu kisha akawatuma kwenda Yafa.

Siku iliyofuata wakati wa adhuhuri walipokuwa wanaukaribia mji wa Yafa, Petro alipanda juu ya paa[a] kuomba. 10 Alihisi njaa na akataka chakula. Lakini walipokuwa wanamwandalia chakula ili ale, aliona maono. 11 Aliona mbingu zikifunguka na kitu kama shuka kubwa kikishushwa chini kutoka mbinguni kwa pembe nne. 12 Ndani yake mlikuwa aina zote za wanyama, watambaao na ndege. 13 Kisha sauti ikamwambia, “Petro simama uchinje chochote hapa kisha ule.”

14 Lakini Petro akasema, “Siwezi kufanya hivyo, Bwana! Sijawahi kula kitu chochote kisicho safi au kisicho stahili kutumiwa kwa chakula.”

15 Lakini sauti ikamwambia tena, “Mungu amekwisha vitakasa vitu vyote hivi. Usiseme havistahili kuliwa.” 16 Hili lilimtokea mara tatu. Kisha likachukuliwa mbinguni. 17 Petro alijiuliza maono haya yalikuwa na maana gani.

Watu ambao Kornelio aliwatuma walishaiona nyumba ya Simoni na walikuwa wamesimama mlangoni. 18 Waliuliza, “Je, Simoni Petro yuko hapa?”

19 Petro akiwa bado anafikiri kuhusu maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Sikiliza, kuna watu watatu wanakutafuta. 20 Inuka na ushuke chini. Nenda nao, usisite, kwa sababu nimewatuma.” 21 Hivyo Petro akashuka chini na kuwaambia, “Nafikiri mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja hapa?”

22 Wale watu wakasema, “Malaika mtakatifu amemwambia Kornelio akualike nyumbani mwake. Ni mtu mwema na hutenda kwa haki, na anamwabudu Mungu na Wayahudi wote wanamheshimu. Malaika alimwambia akualike nyumbani kwake ili asikilize yale utakayosema.” 23 Petro akawakaribisha ndani watu wale ili walale usiku huo.

Siku iliyofuata Petro alijiandaa na kuondoka na wale watu watatu. Baadhi ya waamini katika mji wa Yafa walikwenda pamoja naye. 24 Siku iliyofuata walifika katika mji wa Kaisaria. Kornelio alikuwa anawasubiri na alikuwa amewakusanya jamaa na rafiki zake wa karibu nyumbani mwake.

25 Petro alipoingia ndani ya nyumba, Kornelio alimlaki kisha akaanguka miguuni kwa Petro na akamwabudu. 26 Lakini Petro akamwambia asimame. Petro akasema, “Simama! Mimi ni mtu tu kama wewe.” 27 Petro aliendelea kuzungumza na Kornelio. Ndipo Petro akaingia ndani na kuona kundi kubwa la watu wamekusanyika pale.

28 Petro akawaambia watu wale kuwa, “Mnaelewa kuwa ni kinyume na sheria yetu kwa Myahudi kushirikiana au kumtembelea mtu ambaye si Myahudi. Lakini Mungu amenionyesha kuwa nisimchukulie mtu yeyote kuwa yu kinyume na desturi za Kiyahudi. 29 Ndiyo sababu sikubisha watu wenu waliponiambia kuja hapa. Sasa, tafadhali niambieni kwa nini mmeniita hapa.”

30 Kornelio akasema, “Siku nne zilizopita, kama saa tisa mchana nilikuwa ninaomba ndani ya nyumba yangu. Ghafla akawepo mtu mmoja amesimama mbele yangu amevaa mavazi meupe yanayong'aa. 31 Akasema, ‘Kornelio, Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako kwa maskini. Anakukumbuka wewe na yote uliyofanya. 32 Hivyo tuma baadhi ya watu kwenye mji wa Yafa na wamwambie Simoni Petro kuja. Anakaa na mtu mwingine anayeitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko pembeni mwa bahari.’ 33 Hivyo nikawatuma kwako haraka. Imekuwa vizuri sana umekuja hapa. Sasa sote tupo hapa mbele za Mungu na tuko tayari kusikia kila kitu ambacho Bwana amekwamuru utuambie.”

Petro Ahubiri Katika nyumba ya Kornelio

34 Petro akaanza kwa kusema: “Hakika sasa ninaelewa ni kwa nini Mungu hawachukulii kundi fulani la watu kuwa bora kuliko wengine. 35 Anamkubali yeyote anayemwabudu na anayetenda haki. Haijalishi wanatoka katika taifa lipi. 36 Mungu amezungumza na watu wa Israeli. Aliwaletea Habari Njema kwamba amani imekuja kupitia Yesu Kristo ambaye ndiye Bwana wa watu wote.

37 Mnafahanu kilichotokea katika Uyahudi yote. Kilianzia Galilaya baada ya Yohana kuwaambia watu kuwa inawapasa kubatizwa. 38 Mnajua kuhusu Yesu kutoka Nazareti. Mungu alimfanya Masihi kwa kumpa Roho Mtakatifu na nguvu. Yesu alikwenda kila mahali akiwatendea mema watu. Akawaponya wale waliokuwa wakitawaliwa na yule Mwovu, akionyesha kuwa Mungu alikuwa pamoja naye.

39 Tuliona yote ambayo Yesu alitenda katika Uyahudi na katika mji wa Yerusalemu. Lakini aliuawa. Walimpigilia kwenye msalaba uliotengenezwa kwa mti. 40 Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, Mungu alimfufua na kumfanya aonekane wazi wazi. 41 Hakuonekana kwa Wayahudi wote, lakini alionekana kwetu sisi tu, ambao Mungu tayari alikwisha kutuchagua tuwe mashahidi. Tulikula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu.

42 Yesu alitwambia twende na kuwaeleza watu. Alituagiza tuwaeleza kwamba yeye ndiye ambaye Mungu amemchagua kuwa mwamuzi wa wote walio hai na wote walio kufa. 43 Na ya kwamba kila atakayemwamini Yesu, atasamehewa dhambi zake kupitia nguvu jina Lake. Manabii wote wanakubali kuwa jambo hili ni la kweli.”

Roho Mtakatifu Awashukia Watu Wasio Wayahudi

44 Petro alipokuwa bado anazungumza, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanamsikiliza. 45 Waamini wa Kiyahudi waliofuatana na Petro walishangaa kwamba Roho Mtakatifu amemiminwa kama zawadi hata kwa watu wasio Wayahudi. 46 Waliwasikia wakiongea lugha mbalimbali na kumsifu Mungu. Ndipo Petro akasema, 47 “Je, mtu yeyote anawezaje kuzuia watu hawa wasibatizwe katika maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea!” 48 Hivyo Petro akawaambia wambatize Kornelio pamoja na jamaa zake na rafiki zake katika jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba Petro akae nao kwa siku chache.

Footnotes

  1. 10:9 paa Nyakati za Biblia, nyumba zilikuwa na paa zilizosawa kama sakafu, zilizotumika kama vyumba vya ziada au sehemu za kufanyia mazungumzo.