Add parallel Print Page Options

Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya

(Mk 9:2-13; Lk 9:28-36)

17 Siku sita baadaye, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo na akapanda nao kwenye mlima mrefu. Walikuwa peke yao huko. Wafuasi wake hawa walipokuwa wakimwangalia, Yesu alibadilika. Uso wake ukawa angavu kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama mwanga. Ndipo wanaume wawili waliozungumza naye wakaonekana wakiwa pamoja naye. Walikuwa Musa na Eliya.

Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tuko hapa. Ukitaka, nitajenga vibanda vitatu,[a] kimoja kwa ajili ya heshima yako, kingine kwa ajili ya heshima ya Musa na kingine kwa ajili ya heshima ya Eliya.”

Petro alipokuwa akizungumza, wingu jeupe liliwafunika. Sauti ikatoka katika wingu na akasema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda, ninafurahishwa naye. Mtiini yeye!”

Wafuasi waliokuwa na Yesu walipoisikia sauti hii waliogopa sana na wakaanguka chini. Lakini Yesu akawaendea na kuwagusa. Akasema, “simameni, msiogope.” Wafuasi wakatazama juu, wakaona kuwa Yesu yuko peke yake.

Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanateremka kutoka mlimani, akawaamuru akisema: “Msimwambie mtu yeyote yale mliyoyaona mlimani. Subirini mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu. Ndipo mtaweza kuwaambia watu juu ya kile mlichokiona.”

10 Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Kwa nini walimu wa sheria wanasema ni lazima Eliya aje[b] kabla ya Masihi kuja?”

11 Yesu akajibu, “Wako sahihi kusema ni lazima Eliya aje, na ni kweli kuwa Eliya ataweka mambo yote kama yanavyopaswa kuwa. 12 Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja. Watu hawakumjua yeye ni nani, na walimtendea vibaya, wakafanya kama walivyotaka. Ndivyo itakavyokuwa hata kwa Mwana wa Adamu. Watu hao punde tu watamletea mateso Mwana wa Adamu.” 13 Ndipo wafuasi wakaelewa kuwa Yesu aliposema kuhusu Eliya, alikuwa anazungumza juu ya Yohana Mbatizaji.

Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu

(Mk 9:14-29; Lk 9:37-43a)

14 Yesu na wafuasi walirudi kwa watu. Mtu mmoja akamjia Yesu na kuinama mbele zake. 15 Akasema, “Bwana, umwonee huruma mwanangu. Anateswa sana na kifafa alichonacho. Anaangukia kwenye moto au maji mara kwa mara. 16 Nilimleta kwa wafuasi wako, lakini wameshindwa kumponya.”

17 Yesu akajibu, “Ninyi watu mnaoishi katika nyakati hizi cha kizazi kisicho na imani. Maisha yenu ni mabaya sana! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kijana hapa.” 18 Yesu akamwamuru pepo aliye ndani ya kijana, na pepo akamtoka na yule kijana akapona.

19 Kisha wafuasi wakamjia Yesu wakiwa peke yao. Wakasema, “Tulijaribu kumtoa pepo kwa kijana, lakini tulishindwa. Kwa nini tulishindwa kumtoa pepo?”

20 Yesu akajibu, “Mlishindwa kumtoa pepo kwa sababu imani yenu ni ndogo sana. Niaminini ninapowaambia, imani yenu ikiwa na ukubwa wa mbegu ya haradali mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ondoka hapa na uende kule,’ nao utaondoka. Nanyi mtaweza kufanya jambo lolote.” 21 [c]

Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake

(Mk 9:30-32; Lk 9:43b-45)

22 Baadaye, wafuasi walipokusanyika pamoja Galilaya, Yesu aliwaambia, “Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwenye mamlaka ya watu wengine, 23 watakaomwua. Lakini atafufuliwa kutoka kwa wafu siku ya tatu.” Wafuasi waliposikia kuwa Yesu angeuawa walihuzunika sana.

Yesu Afundisha Kuhusu Kulipa Kodi

24 Yesu na wafuasi wake walikwenda Kapernaumu. Walipofika huko watu waliokuwa wakikusanya ushuru wa Hekalu[d] wakamwendea Petro na kumwuliza, “Je, mwalimu wenu hulipa kodi ya Hekalu?”

25 Petro akajibu, “Ndiyo, hulipa.”

Petro akaingia katika nyumba alimokuwa Yesu. Kabla Petro hajazungumza jambo lolote, Yesu akamwambia, “Wafalme wa dunia huchukua kila aina ya kodi kutoka kwa watu. Lakini ni akina nani ambao hutoa kodi? Je, ni jamaa wa familia ya mfalme? Au watu wengine ndiyo hulipa kodi? Unadhani ni akina nani?”

26 Petro akajibu, “Watu wengine ndiyo hulipa kodi.”

Yesu akasema, “Basi wana wa mfalme hawapaswi kulipa kodi. 27 Lakini kwa kuwa hatutaki kuwaudhi watoza ushuru hawa, basi fanya hivi: Nenda ziwani na uvue samaki. Utakapomkamata samaki wa kwanza, mfungue kinywa chake. Ndani ya kinywa chake utaona sarafu nne za drakma mdomoni mwake. Ichukue sarafu hiyo mpe mtoza ushuru. Hiyo itakuwa kodi kwa ajili yangu mimi na wewe.”

Footnotes

  1. 17:4 vibanda vitatu Au “mahema matatu.” Neno hilo limetafsiriwa “hema takatifu” katika Agano la Kale. Hapa limetumika kwa maana ya mahali pa ibada.
  2. 17:10 lazima Eliya aje Tazama Mal 4:5-6.
  3. 17:21 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 21: “Lakini pepo wa aina hii hutoka kwa kufunga na kuomba.”
  4. 17:24 ushuru wa Hekalu Sarafu za kiyunani, drakma Mbili (pia katika mstari wa 27).