Add parallel Print Page Options

Nani ni Mkuu Zaidi?

(Mk 9:33-37; Lk 9:46-48)

18 Wakati huo huo wanafunzi wake wakamjia Yesu na kuuliza, “Nani ni mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu?”

Yesu akamwita mtoto mdogo, akamsimamisha mbele yao. Kisha akasema, “Ukweli ni huu, ni lazima mbadilike katika namna mnavyofikiri na muwe kama mtoto mdogo. Msipofanya hivi hamtaingia katika ufalme wa Mungu. Aliye mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu ni yule anayejinyenyekeza kama mtoto huyu.

Unapomkubali mtoto mdogo kama huyu kama aliye wangu, unanikubali mimi.

Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi

(Mk 9:42-48; Lk 17:1-2)

Ikiwa mmoja wa watoto hawa wadogo ananiamini, na mtu yeyote akasababisha mtoto huyo kutenda dhambi, ole wake mtu huyo. Ingekuwa bora mtu huyo kufungiwa jiwe la kusagia shingoni mwake na kuzamishwa katika kina kirefu baharini. Nawasikitikia watu wa ulimwengu kwa sababu ya mambo yanayofanya watu watende dhambi. Mambo haya lazima yatokee, lakini ole wake mtu yeyote anayeyafanya yatokee.

Mkono au mguu wako ukikufanya utende dhambi, ukate na uutupe. Ni bora ukapoteza kiungo kimoja cha mwili wako na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na mikono au miguu miwili na ukatupwa katika moto wa milele. Jicho lako likikufanya utende dhambi, ling'oe na ulitupe. Ni bora kwako kuwa na jicho moja tu na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na macho mawili na ukatupwa katika moto wa Jehanamu.

Yesu Atumia Simulizi ya Kondoo Aliyepotea

(Lk 15:3-7)

10 Iweni waangalifu, msidhani kuwa watoto hawa wadogo si wa muhimu. Ninawaambia kuwa watoto hawa wana malaika mbinguni. Na hao malaika daima wako pamoja na Baba yangu mbinguni. 11 [a]

12 Mtu akiwa na kondoo 100, lakini mmoja wa kondoo akapotea, atafanya nini? Atawaacha kondoo wengine 99 kwenye kilima na kwenda kumtafuta mmoja aliyepotea. Sawa? 13 Na akimpata kondoo aliyepotea, atafurahi kwa sababu ya kondoo huyo mmoja kuliko kondoo wengine 99 ambao hawakupotea. Ninaweza kuwathibitishia, 14 Kwa namna hiyo hiyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi mmoja wa watoto hawa wadogo apotee.

Mrekebishe Kila Anayekosea

(Lk 17:3)

15 Ikiwa mmoja wa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akifanya kosa kwako,[b] umwendee na umwambie kile alichokukosea. Ufanye hivi mnapokuwa ninyi wawili tu. Ikiwa mtu huyo atakusikiliza, basi umemsaidia na umfanye kuwa kaka ama dada yako tena. 16 Lakini ikiwa mtu huyo atakataa kukusikiliza, mrudie ukiwa pamoja na ndugu wengine wawili waaminio. Ndipo watakuwepo watu wawili au watatu watakaoweza kueleza kile kilichotokea.[c] 17 Ikiwa mtu aliyetenda dhambi atakataa kuwasikiliza, ndipo uliambie kanisa. Na akikataa kulisikiliza kanisa, mchukulie kama ambavyo ungemchukulia mtu asiyemfahamu Mungu au mtoza ushuru.

18 Ninawahakikishia kuwa mnapotoa hukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Na mnapotoa msamaha, nao utakuwa msamaha wa Mungu.[d] 19 Kwa namna nyingine, ikiwa watu wawili waliopo duniani watakubaliana kwa kila wanachokiombea, Baba yangu wa mbinguni atatenda kile wanachokiomba. 20 Ndiyo, ikiwa watu wawili au watatu wanaoniamini watakusanyika pamoja, mimi nitakuwa pamoja nao.”

Simulizi Kuhusu Msamaha

21 Kisha Petro akamwendea Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu akiendelea kunikosea, ninapaswa kumsamehe anaponikosea mara ngapi? Mara saba?”

22 Yesu akamjibu, “Ninakwambia, ni lazima umsamehe zaidi ya mara saba. Ni lazima uendelee kumsamehe hata kama atakukosea saba mara sabini.[e]

23 Ninawaambia kwa sababu ufalme wa Mungu unafanana na mfalme aliyetaka kupata taarifa kutoka kwa watumishi wake. 24 Mtumishi aliyekuwa anadaiwa na mfalme tani 300[f] za fedha aliletwa kwake. 25 Hakuwa na fedha za kutosha kulipa deni lake. Hivyo mfalme aliamuru kila kitu anachomiliki mtumishi yule kiuzwe ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake.

26 Lakini mtumishi alipiga magoti na kumsihi mfalme akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’ 27 Mfalme alimhurumia. Hivyo akamsamehe yule mtumishi deni lote na akamwacha aende akiwa huru.

28 Lakini mtumishi huyo alipoondoka, alimwona mtumishi mwingine aliyekuwa anamdai sarafu mia za fedha. Akamkaba shingo yake na akasema, ‘Nilipe pesa ninayokudai!’

29 Mtumishi anayedaiwa akapiga magoti na kumsihi akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’

30 Lakini mtumishi wa kwanza alikataa kumvumilia. Alimwambia hakimu kuwa alikuwa anamdai pesa, na mtumishi yule alitupwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa deni lake. 31 Watumishi wengine walipoona hili, walimhurumia mtumishi aliyefungwa gerezani. Hivyo walienda na kumwambia mfalme kila kitu kilichotokea.

32 Ndipo mfalme alimwita msimamizi wa kwanza na kumwambia, ‘Wewe ni mbaya sana! Ulinisihi nikusamehe deni lako, na nilikuacha ukaondoka bila kulipa kitu chochote! 33 Hivyo ulipaswa kumpa mtu yule mwingine anayetumika pamoja nawe rehema ile ile niliyokupa mimi.’ 34 Mfalme alikasirika sana. Hivyo alifungwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa kila kitu anachodaiwa.

35 Mfalme huyu alifanya kama ambavyo Baba yangu wa mbinguni atawafanyia ninyi. Ni lazima umsamehe ndugu au dada yako kwa moyo wako wote, usipofanya hivyo, Baba yangu wa mbinguni hatakusamehe wewe.”

Footnotes

  1. 18:11 Nakala zingine za Kiyunani zimeongeza mstari wa 11: “Mwana wa Adamu amekuja kuokoa waliopotea.” Tazama Lk 19:10.
  2. 18:15 kwako Nakala bora za kale za Kiyunani hazina neno “kwako”.
  3. 18:16 Ndipo watakuwepo … kile kilichotokea Tazama Kum 19:15.
  4. 18:18 mnapotoa msamaha … wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “chochote mtakachokifunga hapa duniani kitakuwa kimefungwa mbinguni, na chochote mtakachokifungua kitakuwa kimefunguliwa mbinguni”.
  5. 18:22 saba mara sabini Ni idadi kubwa sana ya makosa, ikiwa na maana kuwa msamaha haupaswi kuwekewa kiwango.
  6. 18:24 tani 300 Kwa maana ya kawaida, “talanta 10,000”. Talanta 1 ilikuwa kama kilo 27 hadi 36 za sarafu za dhahabu, fedha, ama za shaba.