Add parallel Print Page Options

Yesu Apelekwa kwa Gavana Pilato

(Mk 15:1; Lk 23:1-2; Yh 18:28-32)

27 Mapema asubuhi, viongozi wote wa makuhani na viongozi wazee walikutana na kuamua kumwua Yesu. Wakamfunga kamba, wakamwondoa na kwenda kumkabidhi kwa Pilato, gavana wa Kirumi.

Yuda Ajiua

(Mdo 1:18-19)

Baada ya kumkabidhi Yesu, Yuda aliona kila kitu kilichotokea na kujua kuwa wameamua kumwua Yesu. Naye alihuzunika sana kutokana na kile alichokifanya. Hivyo alirudisha vile vipande thelathini vya sarafu vya fedha kwa wakuu wa makuhani na viongozi wazee. Yuda aliwaambia, “Nimetenda dhambi. Nimemsaliti kwenu mtu asiye na hatia ili auawe.”

Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Hilo halituhusu. Ni tatizo lako, siyo letu sisi.”

Hivyo Yuda akavitupa vipande thelathini vya fedha Hekaluni, kisha akatoka akaenda kujinyonga.

Viongozi wa makuhani wakaviokota vile vipande vya fedha Hekaluni. Wakasema, “Sheria yetu haituruhusu kuweka fedha hii katika hazina ya Hekalu, kwa sababu fedha hii imelipwa kwa ajili ya kifo, ni fedha yenye damu.” Hivyo wakaamua kutumia fedha hiyo kwa kununulia shamba linaloitwa Shamba la Mfinyanzi kwa ajili ya kuwazikia wageni wanapokufa wakiwa ziarani katika mji wa Yerusalemu. Ndiyo sababu eneo hilo bado linaitwa Shamba la Damu. Hili lilitimiza maneno ya nabii Yeremia aliposema:

“Walichukua sarafu thelathini za fedha. Hicho ni kiasi ambacho Waisraeli waliamua kulipa kwa ajili ya uhai wake. 10 Walizitumia sarafu hizo thelathini za fedha kununulia shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniamuru.”[a]

Gavana Pilato Amhoji Yesu

(Mk 15:2-5; Lk 23:3-5; Yh 18:33-38)

11 Yesu alisimama mbele ya Gavana, Pilato, ambaye alimwuliza Yesu, “Wewe ni mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akajibu, “Waweza kusema hivyo.”

12 Lakini viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi walipomshutumu, hakusema kitu.

13 Hivyo Pilato akamwambia, “Husikii mashtaka haya yote wanayokushtaki wewe? Kwa nini hujibu?”

14 Lakini Yesu hakujibu kitu, gavana alishangaa sana.

Pilato Ajaribu Kumwachia Huru Yesu

(Mk 15:6-15; Lk 23:13-25; Yh 18:39-19:16)

15 Kila mwaka wakati wa Pasaka, gavana angemwachia huru mfungwa mmoja yeyote ambaye watu wangetaka aachiwe huru. 16 Wakati huo alikuwepo mtu gerezani aliyejulikana kuwa ni mtu mbaya. Mtu huyu aliitwa Baraba.

17 Kundi la watu lilipokusanyika, Pilato aliwaambia, “Nitamwacha huru mtu mmoja. Mnataka nani nimwache huru: Baraba au Yesu aitwaye Masihi?” 18 Pilato alijua kuwa viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu walikuwa wanamwonea wivu.

19 Pilato alipokuwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akamtumia ujumbe uliosema, “Usifanye jambo lolote juu ya huyo mtu. Hana hatia. Nimeota ndoto juu yake usiku, na ndoto hiyo imenihangaisha sana.”

20 Lakini viongozi wa makuhani na viongozi wazee wa Kiyahudi waliwaambia watu waombe Baraba aachiwe huru na Yesu auawe.

21 Pilato akasema, “Nina Baraba na Yesu. Je, mnataka nimwache huru yupi?”

Watu wakajibu, “Baraba!”

22 Pilato akauliza, “Sasa nimfanye nini Yesu, aitwaye Masihi?”

Watu wote wakasema, “Mwue msalabani!”

23 Pilato akauliza, “Kwa nini mnataka nimwue Yesu? Amefanya kosa gani?”

Lakini walipaza sauti wakisema, “Mwue msalabani!”

24 Pilato akaona hakuna jambo ambalo angefanya ili kubadili nia yao. Kiukweli ilionekana wazi kuwa kungetokea fujo. Hivyo alichukua maji na kunawa mikono yake[b] mbele yao wote. Akasema, “Sina hatia na kifo cha mtu huyu. Ninyi ndio mnaofanya hili!”

25 Watu wakajibu, “Tutawajibika kwa kifo chake sisi wenyewe na hata watoto wetu!”

26 Kisha Pilato akamwachia huru Baraba. Na akawaambia baadhi ya askari wamchape Yesu viboko. Kisha akamkabidhi Yesu kwa askari ili akauawe msalabani.

Askari wa Pilato Wamdhihaki Yesu

(Mk 15:16-20; Yh 19:2-3)

27 Kisha askari wa Pilato wakamchukua Yesu mpaka kwenye nyumba ya gavana, kikosi kizima cha wale askari kikakusanyika pamoja kumzunguka Yesu. 28 Wakamvua nguo zake na kumvalisha kivazi chekundu.[c] 29 Kisha wakatengeneza taji kutokana na matawi ya miiba na kuiweka kwenye kichwa chake na wakaweka fimbo kwenye mkono wake wa kulia. Kisha kwa kumdhihaki, wakainama mbele zake. Wakasema, “Tunakusalimu, mfalme wa Wayahudi!” 30 Walimtemea mate. Kisha wakachukua fimbo yake na kuanza kumpiga nayo kichwani. 31 Baada ya kumaliza kumdhihaki, askari walimvua kivazi chekundu na kumvalisha nguo zake. Kisha wakamwongoza kwenda kuuawa msalabani.

Yesu Awambwa Msalabani

(Mk 15:21-32; Lk 23:26-43; Yh 19:17-19)

32 Askari walipokuwa wanatoka mjini wakiwa na Yesu, walimwona mtu mmoja kutoka Kirene aliyeitwa Simoni, na wakamlazimisha kuubeba msalaba wa Yesu. 33 Walifika mahali palipoitwa Golgotha. (Yaani “Eneo la Fuvu la Kichwa”.) 34 Askari walimpa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo.[d] Lakini alipoionja, alikataa kuinywa.

35 Askari walimgongomea Yesu msalabani, kisha wakacheza kamari ili wagawane nguo za Yesu. 36 Askari walikaa pale ili kumlinda. 37 Wakaweka alama juu ya kichwa chake kuonesha mashtaka dhidi yake yaliyosema: Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.

38 Wahalifu wawili waligongomewa kwenye misalaba pamoja na Yesu, mmoja aliwekwa upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto wa Yesu. 39 Watu waliokuwa wakipita pale walitikisa vichwa vyao na kumtukana Yesu matusi 40 kwa kusema, “Ulisema ungeweza kubomoa Hekalu na kulijenga tena katika siku tatu. Jiokoe mwenyewe! Teremka chini kutoka kwenye huo msalaba ikiwa kweli wewe ni Mwana wa Mungu!”

41 Viongozi wa Makuhani, walimu wa sheria, na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwepo pale pia. Nao pia walimdhihaki Yesu kama watu wengine walivyofanya. 42 Walisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa yeye mwenyewe! Watu husema kuwa yeye ni mfalme wa Israeli. Ikiwa yeye ni mfalme, ashuke kutoka msalabani. Ndipo tutamwamini. 43 Alimtumaini Mungu. Hivyo Mungu amwokoe sasa, ikiwa hakika Mungu anamtaka. Yeye mwenyewe alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’” 44 Hata wale wahalifu wawili waliokuwa misalabani upande wa kulia na wa kushoto wa Yesu walimtukana.

Yesu Afariki

(Mk 15:33-41; Lk 23:44-49; Yh 19:28-30)

45 Ilipofika adhuhuri, giza liliifunika Israeli yote kwa muda wa masaa matatu. 46 Yapata saa tisa alasiri Yesu alilia kwa sauti kuu akisema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” yaani “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha peke yangu?”(A)

47 Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hili wakasema, “Anamwita Eliya.”[e]

48 Mtu mmoja alikimbia haraka akaenda kuchukua sponji, akaijaza siki, akaifunga kwenye fimbo na akanyoosha fimbo ili kumpa Yesu sponji ili anywe siki. 49 Lakini wengine walisema, “Usimjali. Tunataka tuone ikiwa Eliya atakuja kumsaidia.”

50 Yesu akalia kwa sauti kuu tena, kisha akafa.[f]

51 Yesu alipokufa, pazia la Hekalu lilipasuka vipande viwili. Mpasuko wake ulianzia juu mpaka chini. Kulitokea pia tetemeko la ardhi na miamba ilipasuka. 52 Makaburi yalifunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa walifufuka kutoka kwa wafu. 53 Walitoka makaburini. Na baada ya Yesu kufufuliwa kutoka kwa wafu, walikwenda kwenye mji mtakatifu wa Yerusalemu, na watu wengi waliwaona.

54 Afisa wa jeshi na askari waliokuwa wanamlinda Yesu walitetemeka sana kwa kuogopa tetemeko la ardhi na kila walichokiona kikitokea. Wakasema, “Hakika alikuwa Mwana wa Mungu!”

55 Wanawake wengi waliomfuata Yesu kutoka Galilaya kumhudumia walikuwepo pale wakiangalia wakiwa wamesimama mbali na msalaba. 56 Miongoni mwao alikuwepo Mariamu Magdalena, Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu na pia mama yao Yakobo na Yohana[g] alikuwepo pale.

Yesu Azikwa

(Mk 15:42-47; Lk 23:50-56; Yh 19:38-42)

57 Jioni ile, mtu mmoja tajiri aliyeitwa Yusufu alikuja Yerusalemu. Alikuwa mfuasi wa Yesu kutoka katika mji wa Arimathaya. 58 Alikwenda kwa Pilato na akamwomba mwili wa Yesu. Pilato akawaamuru askari wampe Yusufu wa Arimathaya mwili wa Yesu. 59 Aliuchukua mwili na kuuvingirisha katika kitambaa mororo cha kitani safi. 60 Yusufu akauzika mwili wa Yesu katika kaburi mpya alilokuwa amelichonga kwenye mwamba mlimani. Kisha akalifunga kaburi kwa kuvingirisha jiwe kubwa kuziba mlango wa kaburi. Baada ya kufanya hivi, akaondoka. 61 Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu walikuwa wamekaa karibu na kaburi.

Kaburi la Yesu Lalindwa

62 Siku ile ilikuwa Siku ya Maandalizi. Siku iliyofuata, viongozi wa makuhani na Mafarisayo walimwendea Pilato. 63 Wakamwambia, “Mkuu, tunakumbuka kuwa yule mwongo alipokuwa hai alisema, ‘Nitafufuka kutoka kwa watu katika siku tatu.’ 64 Hivyo amuru ili kaburi lilindwe kwa siku tatu. Wafuasi wake wanaweza kuja na kujaribu kuiba mwili. Kisha wataweza kumwambia kila mtu kuwa alifufuka kutoka kwa wafu. Uongo huo utakuwa hatari zaidi ya hata waliyosema juu yake alipokuwa hai.”

65 Pilato akasema, “Chukueni baadhi ya askari, na mwende mkalinde kaburi kwa namna mnavyojua.” 66 Kisha walikwenda kaburini na kuliweka salama dhidi ya wezi. Walifanya hivi kwa kuliziba kwa jiwe langoni na kuwaweka askari wa kulinda kaburi.

Footnotes

  1. 27:9-10 Walichukua … alivyoniamuru Tazama Zek 11:12-13; Yer 32:6-9.
  2. 27:24 kunawa mikono yake Pilato alifanya hivi kama ishara kuwa hakuwa amekubaliana na hakushiriki jambo ambalo watu waliamua kufanya.
  3. 27:28 kivazi chekundu Pengine kilikuwa kivazi cha askari kilichoonekana kama mavazi ya zambarau yanayovaliwa na wafalme. Walimvalisha Yesu hiki kumdhihaki kwa kudai kuwa yeye ni mfalme.
  4. 27:34 nyongo Pengine ilitumika kama dawa ya kupunguza maumivu.
  5. 27:47 Anamwita Eliya Neno hili “Mungu wangu” (ni Eli kwa Kiebrania ama Eloi kwa Kiaramu) ilisikika kwa watu kama jina la Eliya. Nabii maarufu aliyeishi mikaka kama 850 KK.
  6. 27:50 akafa Kwa maana ya kawaida, “roho yake ikamwacha”.
  7. 27:56 Yakobo na Yohana Kwa maana ya kawaida, “wana wa Zebedayo”.