Add parallel Print Page Options

Yesu Amefufuka Kutoka Mauti

(Mk 16:1-8; Lk 24:1-12; Yh 20:1-10)

28 Alfajiri mapema siku iliyofuata baada ya siku ya Sabato, yaani siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu alikwenda kuliangalia kaburi.

Ghafla malaika wa Bwana akaja kutoka mbinguni, na tetemeko kubwa likatokea. Malaika alikwenda kaburini na kulivingirisha jiwe kutoka kwenye mlango wa kaburi. Kisha akaketi juu ya jiwe. Malaika alikuwa anang'aa kama miali ya radi. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. Askari waliokuwa wanalinda kaburi walimwogopa sana malaika, walitetemeka kwa woga na wakawa kama watu waliokufa.

Malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope. Ninajua mnamtafuta Yesu, aliyeuawa msalabani. Lakini hayupo hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu, kama alivyosema. Njooni mwone mahali ulipokuwa mwili wake. Nendeni haraka mkawaambie wafuasi wake, ‘Yesu amefufuka kutoka kwa wafu. Amekwenda Galilaya na atafika huko kabla yenu. Na mtamwona huko.’” Kisha malaika akasema, “Sasa nimewaambia.”

Hivyo wanawake wakaondoka haraka kaburini. Waliogopa sana, lakini walijawa na furaha. Walipokuwa wanakimbia kwenda kuwaambia wafuasi wake kilichotokea, ghafla Yesu alisimama mbele yao. Akasema, “Salamu!” Wanawake wakamwendea wakamshika miguu na wakamwabudu. 10 Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie wafuasi wangu[a] waende Galilaya, wataniona huko.”

Taarifa ya Kufufuka Yesu Yawafikia Viongozi wa Kiyahudi

11 Wanawake wakaenda kuwaambia wafuasi. Na wakati huo huo baadhi ya askari waliokuwa wanalinda kaburi waliingia mjini. Walikwenda kuwaambia viongozi wa makuhani kila kitu kilichotokea. 12 Ndipo makuhani wakakutana na viongozi wazee wa Kiyahudi na kufanya mpango. Wakawalipa wale askari pesa nyingi 13 na kuwaambia, “Waambieni watu kuwa wafuasi wake walikuja usiku na kuuiba mwili mlipokuwa mmesinzia. 14 Gavana atakaposikia juu ya hili, tutazungumza naye ili msiadhibiwe.” 15 Hivyo wale askari wakachukua pesa na kuwatii makuhani. Na jambo hili[b] bado linasambaa miongoni mwa Wayahudi hata hivi leo.

Yesu Azungumza na Wafuasi Wake

(Mk 16:14-18; Lk 24:36-49; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)

16 Wale wafuasi kumi na mmoja walikwenda Galilaya, kwenye mlima ambao Yesu aliwaambia waende. 17 Wakiwa mlimani, wafuasi wale walimwona Yesu na wakamwabudu. Lakini baadhi ya wafuasi hawakuwa na uhakika kama alikuwa Yesu. 18 Kisha Yesu akawajia na akasema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Hivyo nendeni ulimwenguni kote mkawafanye watu kuwa wafuasi wangu. Mkiwabatiza katika jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. 20 Wafundisheni kutii kila kitu nilichowaambia. Na tambueni hili: Niko pamoja nanyi daima. Na nitaendelea kuwa pamoja nanyi hata mwisho wa wakati.”

Footnotes

  1. 28:10 wafuasi wangu Kwa maana ya kawaida, “ndugu zangu”.
  2. 28:15 jambo hili Uongo kuwa mwili wa Yesu uliibwa usiku na wafuasi wake.