Add parallel Print Page Options

Yesu Ajaribiwa na Shetani

(Mk 1:12-13; Lk 4:1-13)

Kisha Roho Mtakatifu akamwongoza Yesu hadi nyikani ili akajaribiwe na Shetani. Baada ya Yesu kufunga kwa siku arobaini mchana na usiku, akaumwa njaa sana. Mjaribu[a] akamwendea na akasema, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, basi yaamuru mawe haya yawe mikate.”

Yesu akajibu, “Maandiko yanasema, ‘Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila Neno linalotoka katika kinywa cha Mungu.’”(A)

Kisha Shetani alimwongoza Yesu mpaka mji mtakatifu wa Yerusalemu na akamweka juu ya mnara wa Hekalu. Akamwambia Yesu, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe mpaka chini! Kwani Maandiko yanasema,

‘Mungu atawaamuru malaika zake wakusaidie,
na mikono yao itakupokea,
    ili usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe.’”(B)

Yesu akamjibu, “Pia, Maandiko yanasema, ‘usimjaribu Bwana Mungu wako.’”(C)

Kisha Shetani akamwongoza Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima ulio mrefu sana na kumwonyesha falme zote za ulimwengu na vitu vya kupendeza vilivyomo ndani. Shetani akamwambia Yesu, “Ukiinama na kuniabudu, nitakupa vitu hivi vyote.”

10 Yesu akamjibu Shetani akamwambia, “Ondoka kwangu Shetani! Kwani Maandiko yanasema, ‘Umwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake!’”(D)

11 Baada ya hayo, Shetani akamwacha. Ndipo malaika wakaja kumhudumia.

Yesu Aanza Kazi yake Galilaya

(Mk 1:14-15; Lk 4:14-15)

12 Yesu aliposikia kuwa Yohana alikuwa amefungwa gerezani, alirudi katika wilaya ya Galilaya. 13 Lakini aliondoka Nazareti. Alikwenda kuishi Kapernaumu, mji ulio kando kando ya Ziwa Galilaya katika eneo la Zabuloni na Naftali. 14 Hili lilitokea ili kutimiza maneno aliyosema nabii Isaya:

15 “Sikilizeni, enyi nchi ya Zabuloni na Naftali,
    nchi iliyo kando ya barabara iendayo baharini,
    ng'ambo ya Mto Yordani!
    Galilaya, wanapokaa Mataifa.
16 Watu wanaoishi katika giza ya kiroho,
    nao wameiona nuru iliyo kuu.
Nuru hiyo imeangaza kwa ajili yao wale
    wanaoishi katika nchi yenye giza kama kaburi.”(E)

17 Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaambia watu ujumbe wake unaosema, “Mbadili mioyo yenu na maisha yenu pia, kwa sababu Ufalme wa Mungu umewafikia.”

Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi

(Mk 1:16-20; Lk 5:1-11)

18 Yesu alipokuwa akitembea kando ya Ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni, aitwaye Petro na nduguye aitwaye Andrea. Ndugu hawa walikuwa wavuvi na walikuwa wanavua samaki kwa nyavu zao. 19 Yesu akawaambia, “Njooni, mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa aina nyingine. Nitawafundisha jinsi ya kukusanya watu badala ya samaki.” 20 Mara moja, Simoni na Andrea wakaziacha nyavu zao na kumfuata Yesu papo hapo.

21 Yesu akaendelea kutembea kutoka pale. Akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo. Walikuwa kwenye mashua pamoja na Zebedayo baba yao. Walikuwa wakiandaa nyavu zao za kuvulia samaki. Yesu akawaita wamfuate. 22 Mara moja wakaiacha mashua pamoja na baba yao na wakamfuata Yesu.

Yesu Afundisha na Kuponya Watu

(Lk 6:17-19)

23 Yesu alikwenda sehemu zote za Galilaya, akifundisha na akihubiri Habari Njema katika masinagogi kuhusu Ufalme wa Mungu. Aliponya magonjwa yote na madhaifu mengi ya watu. 24 Habari kuhusu Yesu zilienea katika nchi yote ya Shamu, na watu waliwaleta wale wote wenye kuteswa na magonjwa na maumivu mbalimbali. Baadhi yao walikuwa na mashetani, wengine walikuwa na kifafa na wengine walikuwa wamepooza. Yesu akawaponya wote. 25 Makundi makubwa ya watu walimfuata; watu kutoka Galilaya, na jimbo lililoitwa Miji Kumi,[b] Yerusalemu, Yuda na maeneo ng'ambo ya Mto Yordani.

Footnotes

  1. 4:3 Mjaribu Kwa maana ya kawaida, “Shetani”.
  2. 4:25 Miji Kumi Jimbo hili lilikuwa mashariki ya Ziwa la Galilaya na wakazi wake hawakuwa Wayahudi. Miji Kumi imejulikana pia kama Dekapoli.