Add parallel Print Page Options

Mafundisho ya Yesu Mlimani

(Lk 6:20-23)

Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda kwenye kilima na kukaa chini. Wanafunzi wake walimjia Yesu. Kisha Yesu akaanza kuwafundisha watu kwa akasema:

“Heri[a] kwa walio maskini na wenye kujua kwamba wanamhitaji Mungu.[b]
    Kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wao.
Heri kwa wenye huzuni sasa.
    Kwa kuwa watafarijiwa na Mungu.
Heri kwa walio wapole.
    Kwa kuwa watairithi nchi.[c]
Heri kwa wenye kiu na njaa ya kutenda haki.[d]
    Kwa kuwa Mungu ataikidhi kiu na njaa yao.
Heri kwa wanaowahurumia wengine.
    Kwa kuwa watahurumiwa pia.
Heri kwa wenye moyo safi,[e]
    Kwa kuwa watamwona Mungu.
Heri kwa wanaotafuta amani.[f]
    Kwa kuwa wataitwa watoto wa Mungu.
10 Heri kwa wanaoteswa kwa sababu ya kutenda haki.
    Kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wao.

11 Heri kwenu ninyi pale watu watakapowatukana na kuwatesa. Watakapodanganya na akasema kila neno baya juu yenu kwa kuwa mnanifuata mimi. 12 Furahini na kushangilia kwa sababu thawabu kuu inawasubiri mbinguni. Furahini kwa kuwa ninyi ni kama manabii walioishi zamani. Watu waliwatendea wao mambo mabaya kama haya pia.

Ninyi ni Kama Chumvi na Nuru

(Mk 9:50; 4:21; Lk 14:34-35; 8:16)

13 Mnahitajika kama chumvi inavyohitajiwa na wale waliopo duniani. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, haiwezi kufanywa chumvi tena. Haina manufaa yo yote isipokuwa hutupwa nje na kukanyagwa na watu.

14 Ninyi ni nuru inayong'aa ili ulimwengu uweze kuiona. Ni kama mji uliojengwa juu ya kilima unavyoonekana wazi. 15 Watu hawawashi taa na kuificha kwenye chungu. Bali huiweka kwenye kinara cha taa ili nuru iangaze kwa kila mtu. 16 Kwa namna hiyo hiyo mnapaswa kuwa nuru kwa ajili ya watu wengine. Hivyo ishini katika namna ambayo watakapoyaona matendo yenu mema, watamtukuza Baba yenu wa mbinguni.

Yesu Afundisha Kuhusu Sheria ya Musa

17 Msifikiri kwamba nimekuja kuiharibu Sheria ya Musa au mafundisho ya manabii. Sikuja kuyaharibu mafundisho yao bali kuyakamilisha. 18 Ninawahakikishia kuwa hakuna jambo litakaloondolewa katika sheria mpaka mbingu na nchi zitakapopita. Hakuna hata herufi ndogo ama nukta katika Sheria ya Musa itakayotoweka mpaka hapo itakapotimizwa.

19 Kila mtu anapaswa kutii kila amri iliyo katika sheria, hata ile isiyoonekana kuwa ya muhimu. Kila atakayevunja mojawapo ya amri hizi ndogo na kuwafundisha wengine kuzivunja atahesabiwa kuwa ni mdogo sana katika ufalme wa Mungu. Lakini kila anayeitii na kuwafundisha wengine kuitii sheria atakuwa mkuu katika ufalme wa Mungu. 20 Ninawambia, ni lazima muitii sheria ya Mungu kwa kiwango bora kuliko kile cha walimu wa sheria na Mafarisayo. La sivyo, hamtaweza kuingia katika ufalme wa Mungu.

Yesu Afundisha Kuhusu Hasira

21 Mmesikia kuwa hapo kale baba zetu waliambiwa, ‘Usimwue yeyote. Na yeyote atakayeua atahukumiwa.’(A) 22 Lakini ninawaambia, msimkasirikie mtu yeyote kwa sababu mkifanya hivyo mtahukumiwa. Na mkimtukana mtu yeyote, vivyo hivyo mtahukumiwa na baraza kuu. Na ukimwita mtu kuwa ni mjinga, utakuwa katika hatari ya kutupwa kwenye moto wa Jehanamu.

23 Unapokwenda kutoa sadaka yako madhabahuni na ukakumbuka kuwa kuna mtu ana jambo dhidi yako. 24 Unapaswa kuiacha sadaka yako kwenye madhabahu na uende kupatana na mtu huyo. Ukiisha patana naye ndipo urudi na kuitoa sadaka hiyo.

25 Akiwepo mtu anayetaka kukushtaki, patana naye haraka. Jitahidi kufanya hivyo kabla ya kufika mahakamani, hata kama bado mpo njiani. Usipofanya hivyo anaweza kukupeleka kwa hakimu. Na hakimu atakupeleka kwa walinzi watakaokufunga gerezani. 26 Ninakuhakikishia kuwa hautatoka huko mpaka umelipa kila kitu unachodaiwa.

Yesu Afundisha Kuhusu Uzinzi

27 Mmesikia ilisemwa kuwa, ‘Usizini’.(B) 28 Lakini ninawaambia kuwa mwanaume akimwangalia mwanamke na akamtamani, amekwisha kuzini naye katika akili yake. 29 Jicho la kuume likikufanya utende dhambi, liondoe na ulitupe. Ni bora kupoteza sehemu moja ya mwili wako kuliko mwili wako wote ukatupwa Jehanamu. 30 Na mkono wako wa kuume ukikufanya utende dhambi, uukate na kuutupa. Ni bora kupoteza sehemu moja ya mwili wako kuliko mwili wako wote kutupwa Jehanamu.

Yesu Afundisha Kuhusu Talaka

(Mt 19:9; Mk 10:11-12; Lk 16:18)

31 Ilisemwa pia kuwa, ‘Kila anayemtaliki mkewe ni lazima ampe hati ya talaka.’(C) 32 Lakini ninawaambia kuwa, kila atakayemtaliki mkewe kutokana na sababu isiyohusiana na uzinzi, anamfanya mke wake kuwa mzinzi. Na kila atakayemwoa mwanamke aliyetalikiwa, atakuwa anazini.

Yesu Afundisha Kuhusu Kiapo

33 Pia, mmesikia hapo kale baba zetu waliambiwa, ‘Unaweka kiapo, usishindwe kutimiza kile ulichoapa kufanya. Timiza kiapo ulichoweka mbele za Bwana.’ 34 Lakini ninawaambia mnapoweka ahadi, msiape kwa jina la mbingu, kwa sababu mbingu ni kiti cha enzi cha Mungu. 35 Na usiape kwa jina la dunia kwa sababu, dunia ni mahali pa kuweka miguu yake. Wala msiape kwa jina la mji wa Yerusalemu, kwa sababu nao ni mali yake Mungu, aliye Mfalme Mkuu. 36 Pia usiape kwa jina la kichwa chako kana kwamba ni uthibitisho kuwa utatimiza kiapo, kwa sababu huwezi kuufanya hata unywele mmoja wa kichwa chako kuwa mweusi au mweupe. 37 Sema ‘ndiyo’ tu kama una maana ya ndiyo na ‘hapana’ tu kama una maana ya hapana. Ukisema zaidi ya hivyo, utakuwa unatoa kwa Yule Mwovu.

Yesu Afundisha Kuhusu Kisasi

(Lk 6:29-30)

38 Mmesikia ilisemwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’(D) 39 Lakini ninawaambia msishindane na yeyote anayetaka kuwadhuru. Mtu akikupiga shavu la kulia mgeuzie na la kushoto pia. 40 Mtu akitaka kukushitaki ili akunyang'anye shati, mpe na koti pia. 41 Askari akikulazimisha kwenda naye maili moja,[g] nenda maili mbili pamoja naye. 42 Mpe kila anayekuomba, usimkatalie anayetaka kuazima kitu kwako.

Wapende Adui Zako

(Lk 6:27-28,32-36)

43 Mmesikia ilisemwa kuwa, ‘Wapende rafiki zako(E) na wachukie adui zako.’ 44 Lakini ninawaambia wapendeni adui zenu na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. 45 Mkifanya hivi mtakuwa watoto halisi walio kama Baba yenu wa mbinguni. Yeye huwaangazia jua watu wote, bila kujali ikiwa ni wema au wabaya. Huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46 Ikiwa mnawapenda wale wanaowapenda ninyi, kwa nini mpate thawabu toka kwa Mungu? Hata watoza ushuru hufanya hivyo. 47 Na ikiwa mnakuwa wema kwa rafiki zenu tu, ninyi si bora kuliko wengine. Hata watu wasiomjua Mungu ni wakarimu kwa rafiki zao pia. 48 Ninalosema ni kuwa, mkue hata kufikia upendo kamili[h] alionao baba yenu wa Mbinguni kwa watu wote.

Footnotes

  1. 5:3 Heri Maana yake ni baraka kuu.
  2. 5:3 maskini … wanamhitaji Mungu Kwa maana ya kawaida, “maskini wa roho”, ama wenye uhitaji wa kiroho.
  3. 5:5 watairithi nchi Wataurithi ulimwengu ujao yaani ufalme wa Mungu unaokuja.
  4. 5:6 wenye kiu na njaa ya kutenda haki Kwa maana ya kawaida, “wenye njaa na kiu ya kutenda haki zaidi ya kitu kingine chochote”.
  5. 5:8 wenye moyo safi Au wenye mawazo safi ama wenye kukusudia mema moyoni, ama wenye nia njema moyoni.
  6. 5:9 wanaotafuta amani Au “wapatanishi wa watu waliofarakana”.
  7. 5:41 maili moja Kama kilomita moja na nusu.
  8. 5:48 kamili Neno “kamilifu”, hapa lina maana “imeendelezwa kwa ukamilifu”, na inaelezea aina ya upendo ambao watoto wanaweza kujifunza kutoka kwa baba.